MAALIM SEIF KUNGURUMA TENA MAREKANI
Na Mwandishi wetu, Philladelphia
Makamo wa Kwanza Mstaafu wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, anatazamiwa kunguruma tena
chini Marekani wiki hii.
Gwiji huyo wa siasa ambaye aliwasili jijini Philladelphia hapo jana,
anatarajiwa kuwakhutubia Watanzania katika Mkutano wa hadhara
utakaofanyika Jumamosi hii katika jiji la Boston.
Katibu huyo Mkuu wa CUF pamoja na ujumbe anaofuatana nao aliwasili
nchini humu akitokea Uingereza baada ya kukamilisha ziara yake ya Ulaya
iliyochukua muda wa zaidi ya wiki moja.
Akiwa Ulaya Maalim Seif alitembelea Uiengerza na kufanya mikutano na
Maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Uingereza, Vyama vya kisisasa na
Taasisi mbalimbali.
Baadaye alielekea nchini Ubelgiji ambako alifanya ziara kwenye Makao
Makuu ya Umoja wa Ulaya na kufikisha madai ya Wazanzibari ya kurejeshewa
haki yao ya Kidemokrasia.
Aidha alitembelea nchini Uholanzi ambako pamoja na mambo mengine,
alikutana na maofisa wa Mahakama ya Ukhalifu ya Kimataifa na kufikisha
kilio cha Wazanzibari dhidi ya Uvunjaji wa Haki za Binadamu unaendelea
Visiwani Zanzibar.
Ziara hiyo ya Ulaya ilikuja katika kile maofisa wa CUF walichokielezea
kuwa ni awamu ya pili ya ziara za nje za mwanasiasa huyo mkongwe katika
juhudi za kutafuta uungwaji mkono wa Kimataifa kwa mgogoro wa Kisiasa
Zanzibar.
Maalim Seif ambaye anafuatana na Mkuuwa Watumishi katika Ofisi ya Katibu
Mkuu wa CUF Bwana Issa Kheir Hussein, yupo nchini Marekani kuitikia
mwaliko wa kuhudhuria kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Democratic
ulioanza jana jijini Philladelphia, mkutano ambao unatazamiwa kumpitisha
Bi Hillary Clinton kuwa mgombea wa Urais wa Marekani kwa kuoitia tiketi
ya Chama hicho.
Katika mkutano wake wa hadhara na Watanzania, Maalim Seif, aliyekuwa
mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha CUF katika uchaguzi Mkuu
uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, anatazamiwa kuzungumzia zoezi zima
la uchaguzi huo uliofutwa, na kusisitza madai ya Chama chake ya
kurejeshewa haki yao waliyoporwa katika uchaguzi huo, na mwenendo mzima
wa Demokrasia nchini Tanzania.
Itafaa kukumbusha kuwa hii ni mara ya pili kwa Maalim Seif kuzuru
Marekani katika kipindi cha chini ya miezi miwili. Mwezi uliopita,
Maalim Seif alikuwepo nchini humu na kufanya mazungumzo na viongozi wa
Kisiasa na mashirika binafsi, na kutembelea Umoja wa Mataifa ambako
alifikisha madai ya Chama chake ya ukandamizaji wa demokrasia nchini
Tanzania. Aidha alizungumza na Watanzania waishio nchini Marekani katika
jiji la Washington.
MAALIM SEIF KUNGURUMA TENA MAREKANI
Reviewed by WANGOFIRA
on
08:58:00
Rating:
No comments: