PM: Mji Mkuu Dodoma kuthibitishwa kisheria
SERIKALI inatarajia kupeleka bungeni muswada wa kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi ili uweze kuthibitishwa kisheria.
Muswada huo utawasilishwa katika bunge la Septemba mwaka huu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo jana mjini hapa wakati
akizungumza na viongozi wa serikali, Taasisi, Watendaji na wananchi wa
mkoa wa Dodoma kuelezea azma ya serikali kuhamia Dodoma.
Pia alitoa siku 14 kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)
kuwasilisha mapendekezo ya awali namna watakavyopendekeza mpango wa
serikali kuhamia Dodoma. Waziri Mkuu alisema katika bunge lijalo muswada
wa sheria ya serikali kuhamia Dodoma utapelekwa bungeni ili azma ya
Rais John Magufuli na serikali yake uwe na nguvu kisheria.
Pia aliendelea kueleza: “Kazi inayofuata serikalini baada ya tamko la
Rais Magufuli la serikali kuhamia Dodoma katika bunge lijalo ni
kuwasilisha muswada wa sheria bungeni kabla ya kuanzishwa sheria,
maamuzi kadhaa yamefanywa ikiwemo mikakati ya serikali ili kuimarisha
uhamiaji huo,” alisema.
“Uamuzi wa kuhamia Dodoma na kuufanya mji huo kuwa makao makuu ya
serikali imekuwa ni ndoto ya baba wa taifa na kudumu wakati wote wa
awamu za serikali zilizofuata na hadi sasa serikali ya awamu ya tano
utatekelezwa,” alisema.
Waziri Mkuu aliendelea kubainisha kwamba, “Rais John Magufuli na
Makamu wa Rais pamoja na viongozi wengine wa chama wamesimamia ndoto ya
baba wa taifa, na sasa inakwenda kutimia.
Alisema maagizo ya Rais ya Serikali kuhamia Dodoma ni halisi na
hakuna namna nyingine kwani maagizo yametolewa na ni wajibu wa kila
mmoja wetu kuyaamini na kuanza kuyatekeleza.
Aliendelea kusisitiza kwamba, “Mimi tayari niko Dodoma nina ofisi,
nina nyumba na hata ile kauli yangu ya miezi miwili niliyotoa jana mbele
ya Rais wakati wa sherehe za mashujaa, ililenga kwa watumishi wengine
walio chini yangu kujipanga kuhamia Dodoma lakini, mimi tayari nipo na
nitaendelea kufanya shughuli zangu nikiwa hapa Dodoma.
Alisema wageni wote watakaotaka kukutana na viongozi wakuu wa nchi,
wakiwamo makatibu wakuu, mabalozi na watendaji wengine itawabidi kufika
Dodoma.
Amesema, “wageni wote watakaomtaka Waziri Mkuu, pamoja na Makamu wa
Rais waje watukute Dodoma na hayo ndio maagizo ya Rais Magufuli,”
alisema. Alisema wizara zote zina nyumba, mawaziri na makatibu wakuu
wana nyumba na ofisi hapa Dodoma kwa hiyo haitakuwa kazi ngumu kwao
kuhamia Dodoma.
Waziri Mkuu alisema, Rais anapotoa maelekezo lazima yatimizwe ni utaratibu uliojengwa kwa watumishi wa umma.
Atoa siku 14
Alitoa siku 14 kwa serikali mkoa wa Dodoma kukaa na taasisi zake
hususani Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuandaa na kutoa
mpango kazi wake na kuuwasilisha kwa Waziri Mkuu ili aone
watakavyotekeleza mpango huo kwa haraka na ufasaha.
“Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna mtakavyotekeleza
naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi
yote.Baada ya siku 14 nipate mpango wenu,” alisema.
Mabalozi kujenga ofisi Dodoma
Alisema mabalozi wameonesha nia ya kujenga ofisi zao Dodoma na
wanaendelea kuzungumza nao ili makao makuu ya serikali yawe ni kweli na
kutambulika kote na wakitoka nje ya nchi watue kwanza Dodoma.
Maagizo kwa CDA
Alisema CDA itambue eneo la makazi ya serikali kuu kwa maana ya ofisi
za wizara na taasisi zake, makazi ya watumishi na huduma za biashara,
elimu na taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinatumika kwa haraka
tayari kwa matumizi.
Pia kuwepo kwa mfumo moja wa upatikanaji wa viwanja vya matumizi
mbalimbali na ujulikane uwe wazi bila urasimu na uwekwe kwenye mfumo wa
kompyuta na uuzaji wa viwanja uwe hivyo uwe wa kielektroniki kuepusha
udanganyifu wa madalali.
“Sitaki kusikia viwanja vinapatikana katika mfumo usio rasmi mpaka
wapitie kwa wakuu wa mikoa, wilaya, meya na kumfanya kila mtu anatoa
kiwanja,” alisema.
Pia alishauri serikali na taasisi zake na hasa zisizo za kibiashara
zielekezwe eneo jipya la makazi rasmi ya serikali na sio kuwapa viwanja
Dodoma huko ni kurudia makosa ya Dar es Salaam kwa kuchanganya serikali
na biashara na kusababisha foleni.
Waziri Mkuu aliitaka CDA na serikali ya mkoa kuhakikisha wanatenga
maeneo maalumu kwa ajili ya bandari kavu, kituo kikuu cha biashara, eneo
maalum la wajasiriamali kuendelea kuongeza eneo la viwanda na huduma
mbalimbali za biashara mahoteli, mabenki elimu na afya pamoja na
kuongeza kasi ya kupima viwanja kwa ajili ya makazi, viwanda na taasisi.
Aliwataka Tanroads kukarabati barabara zilizopo chini na kubuni
ringroads kwa ajili ya kuepusha foleni sizizo za lazima na kuzitaka
taasisi nyingine kuboresha huduma kama mamlaka ya majisafi na majitaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema atahakikisha anawasilisha mapendekezo ndani ya siku 10.
HABARI LEO
PM: Mji Mkuu Dodoma kuthibitishwa kisheria
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:33:00
Rating:
No comments: