Watu 11 wafa ajalini Morogoro
WATU 11 wamekufa papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali
mbili tofauti zilizotokea sehemu moja, zikihusisha basi la abiria,
lililopamia malori mawili ya mizigo yaliyogongana uso kwa uso na kuungua
moto eneo la Dakawa – Veta, wilayani Kilosa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema mjini
hapa jana kuwa ajali ya kwanza, malori mawili ya mizigo yaligongana uso
kwa uso juzi saa 12 jioni na kuwaka moto.
Katika ajali hiyo ya juzi jioni, lori la mizigo aina ya Scania ambalo
namba za mbele hazikutambuliwa, lakini tela lake ni namba T 704 CEC,
likitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, liligongana uso
kwa uso na lori aina ya Fuso yenye namba za usajili T 963 BLW,
lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Matei alisema katika ajali hiyo, watu watano walipoteza
maisha papo hapo kwa kuungua moto mpaka ikashindikana kuwatambua,
akiwemo dereva wa bodaboda aliyekuwa pembeni mwa barabara na pikipiki
yake katika eneo la tukio.
Wengine waliokufa papo hapo na kushindwa kutambulika kwa mujibu wa
Kamanda Matei, ni madereva wa malari hayo na wasaidizi wao wawili; mmoja
kwa kila lori.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, ni kutokana na gari ndogo iliyokuwa
mbele ya Fuso hilo kusimama ghafla na kusababisha dereva wa Fuso kupita
pembeni bila kuangalia mbele na kugongana uso kwa uso na Scania yenye
shehena ya mafuta na kusababisha malori hayo kuwaka moto.
Wakati malori hayo yakiwa eneo la tukio, jana alfajiri kulitokea
ajali nyingine ambapo basi la abiria mali ya Kampuni ya Otta Classic
yenye namba za usajili T 201 DGK aina ya Higer, lilipamia moja ya malori
yaliyokuwa yamepata ajali katika eneo hilo na kuua watu sita papo hapo
na kujeruhi wengine 44.
Kamanda Matei alisema kati ya majeruhi hao, sita hali zao ni mbaya na
walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro kupatiwa matibabu
zaidi. Alisema ajali hiyo ilitokea saa 10 alfajiri ya Julai Mosi mwaka
huu, wakati basi hilo likitokea Bukoba mkoani Kagera kwenda Dar es
Salaam.
Waliokufa katika ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda Matei ni dereva wa
basi hilo, msaidizi wake, kondakta na abiria wengine watatu.
Alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Yassin Mgongolwa (41) dereva wa
basi hilo, Veronica Jeremia ambaye ni kondakta, Said Shomari Simba (30)
dereva msaidizi na abiria Lilian Paul (34), Jonia Kokumbuga na mwamamke
mwingine mwenye umri kati ya miaka 30 -35, ambaye hajatambulika.
Miili ya marehemu hao na maiti zilizoungua na kushindwa kutambuliwa,
imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Kamanda Matei alisema kabla ya basi hilo kupata ajali, lilisimamishwa
na askari wa usalama barabarani, lakini dereva alikaidi na kupitiliza
na baada ya muda likapata ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, ambaye pia alifika eneo
la tukio hilo jana, alisema miili iliyoungua, itatambuliwa kwa kutumia
vinasaba (DNA) na kuwataka ndugu na jamaa zao kuwa na subira wakati
utambuzi huo utakapofanyika.
Alilipongeza Jeshi la Polisi mkoa na vikosi vya Zimamoto na wananchi
wa vijiji vya karibu na eneo la ajali kwa kusaidia kuzima moto na kuokoa
majeruhi wa ajali hiyo.
CHANZO HABARI LEO
Watu 11 wafa ajalini Morogoro
Reviewed by WANGOFIRA
on
21:55:00
Rating:
No comments: