Sita wauawa katika shambulio dhidi ya mabasi Kenya

Watu sita wameuawa nchini Kenya baada ya washambuliaji wanaoshukiwa kuwa wa kundi la itikadi kali la Al-Shabaab kuyafyatulia risasi mabasi mawili kaskazini mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Somalia.
Inspekta Jenerali mkuu wa Polisi IGP Joseph Boinnet, amesema maafisa wa jeshi hilo walioko kwenye eneo la tukio walikuta watu sita wakiwa wamepigwa risasi na kuuawa, na kuongeza kuwa msako dhidi ya magaidi hao ulikuwa unaendelea.
Boinnet alisema watu wengine wawili wamejeruhiwa, lakini mratibu wa usalama wa kanda ya Kaskazini-Mashariki Mohammed Saleh alisema watu wengi walijeruhiwa. Haikubainika bado iwapo wahanga wa shambulio hilo walikuwa raia au maafisa wa polisi waliokuwa wanatoa ulinzi katika mabasi hayo.
Shambulio hilo la Ijumaa asubuhi limetokea karibu na El Wak katika kaunti ya Mandera, eneo maskini la vijiji katika nchi hiyo ambako mashambulizi ya maafa sawa na hilo katika siku za nyuma yamedaiwa na kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda.

Kamishna wa kaunti ya Mandera Fredrick Shisia ameliambia shirika la habari la Reuters, kuwa shambulio hilo lilitokea majira ya saa tatu na nusu asubuhi ya Ijumaa, wakati mabasi hayo yakisafiri kwenda mjini Mandera kutoka mji mkuu Nairobi.

CHANZO: DW
Sita wauawa katika shambulio dhidi ya mabasi Kenya Sita wauawa katika shambulio dhidi ya mabasi Kenya Reviewed by WANGOFIRA on 20:37:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.