Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni Aagiza Magari yanayokamatwa yakisafirisha wahamiaji haramu yataifishwe


Serikali imeiagiza Idara ya Uhamiaji kuhakikisha inasimamia sheria kwa kuyakamata na kuyataifisha magari yote yanayotumika kusafirisha wahamiaji haramu kutoka nje ya nchi.

Pia, serikali imewaonya wanaojihusisha na mtandao wa kusafirisha wahamiaji haramu kuacha mara moja na kutafuta kazi nyingine za kufanya kwani serikali iko makini kudhibiti wahamiaji haramu.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alipotembelea mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga mwishoni mwa wiki, ili kujionea changamoto zilizopo mpakani na kuelewa hali halisi.

Masauni aliwatahadharisha watumishi wa Idara hiyo kuwa endapo gari litakamatwa katika eneo lolote nchini likiwa na wahamiaji haramu kupitia mpaka huo, watakuwa wameidanganya Serikali na kuidhihirishia kuwa majukumu yao yatakuwa yamewashinda.

Alisema pamoja na kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na idara hiyo ya uhamiaji Namanga kudhibiti wahamiaji haramu, bado zipo njia za panya zinazotumiwa na wahamiaji hao mmoja mmoja kwa kushirikiana na Watanzania wachache wanaofanya kazi ya kuwavusha kwa kulipwa ujira kinyume cha sheria.

Aliitaka idara hiyo kutumia vitendea kazi vichache ilivyonavyo pamoja na waumishi wachache waliopo ili kudhibiti mianya inayotumiwa na wahamiaji hao. Pia, aliagiza doria za mara kwa mara na kuimarisha ukaguzi ndani ya magari ili kubaini wahamiaji haramu.

Alisema idara hiyo inafanya kazi kwenye mazingira magumu kutokana na uhaba wa vitendea kazi, ukubwa wa eneo la mpaka hivyo akatoa wito kwa wananchi kusaidia kuwafichua wahamiaji haramu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema idara hiyo inakabiliwa na changamoto zilizopo mpakani hapo kutokana na ukubwa wa eneo la mpaka hivyo inashindwa kudhibiti eneo hilo kikamilifu.

Awali, Mkuu wa idara hiyo katika eneo hilo la Namanga, Abdalah Katimba, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa watumishi na vitendea kazi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni Aagiza Magari yanayokamatwa yakisafirisha wahamiaji haramu yataifishwe Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni Aagiza Magari yanayokamatwa yakisafirisha wahamiaji haramu yataifishwe Reviewed by WANGOFIRA on 21:13:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.