Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Yamkuta na Kesi ya Kujibu Mshitakiwa Kesi ya Mauaji ya Mwangosi

Mahakama kuu kanda ya Iringa imetupilia mbali ombi la wakili wa upande wa utetezi katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari marehemu Daudi Mwangosi inayomkabili askari wa jeshi la polisi kikosi cha kutuliza ghasia FFU mjini Iringa Pasificus Cleophace Simon. 

Awali wakili wa upande wa utetezi Rwezaura Kaijage aliwasilisha maombi kuitaka mahakama kumwachia huru mtuhumiwa, akieleza kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hauoneshi moja kwa moja kuhusika kwa mshitakiwa huyo katika kutenda kosa hilo la mauaji. 


Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania Mheshimiwa Dokta Paul Kiwhelo anayesikiliza kesi hiyo ,amesema ameridhishwa na hoja za mawakili wa upande wa Jamhuri zilizotolewa na mawakili wa serikali Sunday Hyera na Ladislaus Komanya waliopinga hoja za wakili huyo wa upande wa utetez.
Amesema  katika hatua hii mahakama hailazimiki kutazama kama ushahidi uliotolewa mahakamani unaweza kumtia hatiani mshitakiwa badala yake mahakama inatazama kama kwenye kesi iliyopo zipo tuhuma zinazomuhitaji mshitakiwa kuzijibu. 


Akitumia vifungu vya sheria pamoja na rejea za kesi mbalimbali zinazofanana na kesi hiyo zikiwemo za nje ya nchi pamoja na baadhi zilizowahi kuamuliwa na mahakama mbalimbali kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ,Jaji Kiwhelo amesema hoja ya kuwa na kesi ya kujibu ama kutokuwa na kesi ya kujibu ni utaratibu wa kawaida na unatumika mahala kwingi duniani kwakuwa kwenye kesi za jinai mtuhumiwa huwa hana hatia hadi pale mahakama inapomtia hatiani. 


Baada ya mahakama kutoa uamuzi wa kumuona mshitakiwa kuwa na kesi ya kujibu wakili wa upande wa Jamhuri Ladislaus Komanya ameikumbusha mahakama kuwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 293 (2) kifungu kidogo cha pili marejeo ya mwaka 2002 mahakama inao wajibu kumkumbusha mshitakiwa haki zake kabla ya kutoa utetezi wake mbele ya mahakama. 


Mahakama imepanga kuendelea na kesi hiyo hapo kesho baada ya mawakili wa pande zote kukubaliana ambapo mshitakiwa ataanza kujitetea mahakamani hapo.
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Yamkuta na Kesi ya Kujibu Mshitakiwa Kesi ya Mauaji ya Mwangosi Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Yamkuta na Kesi ya Kujibu Mshitakiwa Kesi ya Mauaji ya Mwangosi Reviewed by WANGOFIRA on 20:34:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.