JPM AZIGEUKIA KAMPUNI ZA SIMU
Rais John Magufuli akionesha sarafu maalumu ya Sh 50,000 baada ya kuizindua kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dar es Salaam jana. Kulia ni Gavana wa benki hiyo, Profesa Benno Ndulu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar, Khamis Mussa Omar. (Picha na Ikulu). | |
RAIS John Magufuli ameagiza kwa taasisi zinazosimamia fedha na kodi,
kuhakikisha kuwa serikali inakusanya kodi kwenye miamala ya fedha,
inayofanywa na taasisi hizo na kampuni za simu na za madini.
Aidha, ameagiza kuwa Sh bilioni saba zilizolipwa kwa pensheni hewa,
zirejeshwe mara moja huku akitoa ufafanuzi wa hatua ya serikali ya
kusitisha kwa muda ajira serikalini.
Rais Magufuli alisema hayo Dar es Salaam jana katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na uzinduzi wa sarafu maalumu
yenye thamani ya Sh 50,000 na vitabu viwili, kikiwemo vinavyozungumzia
masuala ya fedha na uchumi.
Uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam,
ulikwenda pamoja na kongamano lililojadili mada kuhusu namna ya kupata
fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya misaada na mikopo nafuu na athari
zake iliyowasilishwa na Profesa Justin Lin wa Chuo Kikuu cha Peiking,
China.
Rais Magufuli alisema takwimu zinaonesha katika mwezi mmoja wa Machi,
miamala iliyofanywa na kampuni za simu za mkononi ni ya zaidi ya Sh
trilioni 5.5, lakini alihoji ni kasi gani cha kodi kimeingia serikalini.
Alisema pamoja na kusimamia makusanyo ya kodi za serikali, pia
aliagiza BoT, Hazina na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
wajipange kuhakikisha mtambo wa kudhibiti makusanyo ya kodi, unafanya
kazi na kufuatilia usalama wa huduma za fedha.
Mbali na hilo, aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha serikali
inakusanya kodi zinazostahili kutoka kwenye kampuni za madini na
kufuatilia kwa karibu, kwa kuwa kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na
baadhi ya kampuni.
“Unakuta kampuni ipo nchini mwaka wa kwanza hadi wa 10, wanakwambia
hawapati faida lakini wanaendelea kuchimba dhahabu. Sasa eneo hilo
liangaliwe kwa karibu na kama kampuni inashindwa bora iondoke, ni heri
tubaki na dhahabu yetu hata miaka 1000 ijayo, watakuja kuchimba wengine
wakati sisi tumeshaoza. Visingizio vya kupata hasara kila mwaka, lakini
wanaendelea kuwepo, haiwezekani,” alisema.
Aliwataka watendaji hao kutokuwa na kigugumizi katika kusimamia
rasilimali kwa manufaa ya Taifa na kwamba serikali ina imani kubwa na
BoT, hivyo wakisimamia vizuri uchumi utaimarika.
Pensheni hewa
Aidha, aliwataka viongozi wa taasisi hizo pia kushirikiana katika
kudhibiti malipo kwa watumishi hewa, ambayo sasa imefikia kwenye utoaji
wa pensheni hewa. Alisema anazo taarifa kuna wafanyakazi hewa 2,800,
ambao wamelipwa pensheni hewa ya Sh bilioni saba kupitia Benki ya NMB,
na kuagiza fedha hizo zifuatiliwe na benki hiyo izirejeshe mara moja.
“Wakati nazungumzia watumishi hewa ndani ya serikali wamefikia 12,446
na kwamba inawezekana idadi hiyo ikaongezeka na sasa watumishi hao
wamelipwa pensheni shilingi bilioni saba,” alisema.
Rais Magufuli alisema wakati serikali inahakiki wafanyakazi hewa,
Utumishi waliendelea kuajiri wapya, jambo ambalo kwa sasa amelisimamisha
kwa miezi miwili ili kutoa nafasi ya kushughulikia changamoto hiyo.
Kusitishwa ajira
“Nilisema ajira mpya zisimame kwa mwezi mmoja na nusu lakini
haitazidi miezi miwili, nawaomba watumishi msivunjike moyo kwa kuwa
serikali imegundua kosa lazima lirekebishwe, lazima tujipange. Hata
kupandisha vyeo tumesimamisha kwa muda huo baadae tutaendelea, tunataka
kujenga nidhamu,” alisema.
Pia aliitaka BoT kufuatilia kwa karibu utendaji wa benki na kuchukua
hatua kwa benki, ambazo hazifanyi kazi vizuri hata kama zinamilikiwa na
serikali.
“Benki mojawapo ni Twiga Bancorp, haifanyi kazi vizuri, inajiendesha
kwa hasara na serikali imekuwa ikiipatia fedha kila mwaka za uendeshaji.
Hasara imefikia shilingi bilioni 18. Naomba Katibu Mkuu Hazina na BoT
mfuatilie kama imeshindwa kujiendesha ifungwe.
“Katika utawala wangu sitabembeleza, nataka watu wafanye kazi kama
benki haizalishi ni afadhali ikafungwa kuliko kuendelea kuitia hasara
serikali. Kuna benki nyingine nayo ambapo inapigiwa debe na wanasiasa
tena wa CCM lakini nayo haifanyi vizuri,” alisema.
Alisema kwa kuwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, sio mwanasiasa,
anapaswa kufanya kazi yake bila kujali kama benki ni mali ya serikali au
la, na kuwaacha wanasiasa waendelee na yao.
Aidha, aliagiza BoT kufuatilia suala la akaunti zilizolala kwenye
benki kwa kuwa wakati mwingine fedha zinakaa mpaka watu wanapanga
kuzitorosha. “Najua kwenye akaunti hizo kuna fedha nyingi, kuna akaunti
moja ina Sh bilioni 23. Nataka mfuatilie na mimi nafuatilia kwa karibu,”
alisema.
Pia aliwataka BoT kufuatilia kwa karibu maduka ya kubadilisha fedha
ili wafanye biashara halali na yasitumike vibaya kutorosha fedha ama
kutakatisha fedha haramu zikiwemo za wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Mfumuko wa bei
Alisema kwamba jukumu kubwa la BoT ni kudhibiti mfumuko wa bei na
katika kipindi cha miaka ya 1990 hadi mwaka huu, Benki Kuu imefanya kazi
kubwa ya kupunguza mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 hadi asilimia 5.2.
Hata hivyo, alisema kupungua huko kunaonekana vizuri kwenye takwimu,
lakini katika uhalisia wa maisha ya watu bado kuna changamoto kubwa; na
wakati mwingine wananchi wanaona kama mfumuko wa bei umeongezeka hadi
kufikia asilimia 70.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza watendaji wa BoT wakiongozwa na
Gavana Ndulu, kuhakikisha hiyo asilimia iliyopungua inaonekana kwenye
maisha ya wananchi wa kawaida kwa maana ya bei za bidhaa kupungua.
Aliwapongeza wafanyakazi wa BoT chini ya uongozi wa Profesa Ndulu kwa
mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 50, ikiwemo kuongeza
benki kutoka tatu hadi 54 ambazo zimeendelea kufanya kazi na kutoa
mikopo.
Fedha vijijini
Hata hivyo, alisema kuna haja ya BoT kuhakikisha huduma za fedha
zinafikishwa vijijini ambako kuna zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania
badala ya kubaki mijini, ambako kwa sehemu kubwa wanafanya biashara na
serikali.
Alisema pia taasisi za fedha zimeendelea kutoa mikopo na kutoza riba
kubwa, ambapo sehemu kubwa ya wakopaji wamejikuta wakishindwa kuendelea
na wengine kufilisika kutokana kulipa fedha nyingi za riba kwenye
mikopo.
JPM AZIGEUKIA KAMPUNI ZA SIMU
Reviewed by WANGOFIRA
on
21:00:00
Rating:
No comments: