CHAKUA yapinga ongezeko tozo ya abiria UBT


 Sehemu ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam
CHAMA cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua) kimesema hakikubaliani na ongezeko la tozo ya abiria katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo (UBT) iliyoanza Julai mosi mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Chakua, Haasan Mchanjama alisema, kuongezeka kwa tozo kabla ya kituo kuboreshwa ni kuwaumiza wananchi na abiria wanaotumia kituo hicho.

“Hatukubaliani na hatujapendezewa na kitendo cha ongezeko la tozo huku kituo kikiwa hakina huduma za msingi, mantiki ya ongezeko la tozo inamaanisha huduma za msingi zinapatikana,” alisema Mchanjama.

Alisema licha ya kuongezeka kwa tozo hiyo bado abiria wanapoingia katika kituo hicho wanalipia huduma za msingi ikiwemo choo, huku abiria na wananchi wakiendelea kuumia kwa kukosa sehemu za kupumzika pindi wawapo katika kituo hicho.

“Tunajaribu kuwasiliana na wadau wengine kuona namna tunaweza kufanya kuhusu ongezeko hili, tozo katika kituo hicho ilianza muda mrefu lakini hakuna maboresho yoyote, tunahoji fedha hizo walizipeleka wapi?” alisisitiza.

Hivi karibuni Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam iliongeza tozo katika kituo hicho, akizungumza Mkuu wa kitengo cha itifaki na uhusiano wa Halmashauri ya Jiji, Gaston Makwembe alisema awali kituo hicho kilikuwa kikisimamia uendeshaji wa shughuli zote za kituo kwa kutumia Sheria Ndogo ya Mwaka 2004 ya Kituo Kikuu cha Mabasi, hivyo kwa sasa inaanza kutumika Sheria Ndogo ya Mwaka 2009 ambayo imefuta matumizi ya sheria ya Mwaka 2004.

Alisema sheria hiyo ndogo ya mwaka 2009 inawataka wasindikizaji wote wa abiria watakaoingia katika kituo hicho kulipia Sh 300 badala ya Sh 200 iliyokuwepo awali.

Chanzo HABARI LEO
CHAKUA yapinga ongezeko tozo ya abiria UBT  CHAKUA yapinga ongezeko tozo ya abiria UBT Reviewed by WANGOFIRA on 20:16:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.