Serikali: Hakuna Sababu Ya Kuagiza Transforma Za Umeme Wakati Zinatengenezwa Nchini


Serikali imeliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutoagiza transfoma nje ya nchi na badala yake kutumia zinazotengenezwa hapa nchini na kampuni ya Tanalec.

Agizo hilo limetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini, Mhe. Daimu Iddi Mpakate aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa pesa kukamilisha miradi ya umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Dkt. Kalemani alisema uzalishaji wa transforma ni mkubwa ikilinganishwa na mahitaji ya bidhaa hizo kwa mwezi, hivyo hakuna sababu ya kuagiza transforma hizo kwa bei kubwa wakati zinapatikana hapa nchini.

Kuhusu suala la kugharamia nguzo kwa Mpango wa REA Dkt. Kalemani alisema mteja hatakiwi kutozwa gharama yoyote ziadi ya Tshs. 27,000 fedha ya kuunganishiwa umeme kwa mpango huu.Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali inatekeleza Mradi wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Tunduru na kazi hii inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016.

Alisema Kazi ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa Kilomita 293. 2, na ujenzi wa njia nyingine yenye msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 76.1 na ufungaji wa transfoma 38 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,330

“Gharama ya Mradi kwa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Wilaya ya Tunduru ni Tsh. Bilioni 32.56,” alisema Dkt Kalemani na kuongeza kuwa mkandarasi amekwishalipwa bilioni 27.22 sawa na asilimia 83.6 ya fedha.

Dkt. Kalemani amesema kuwa katika Wilaya ya Tunduru ni vijiji vinne ambavyo vimeunganishiwa miundombinu ya umeme na kufanyiwa majaribio kabla ya kuwashiwa umeme.

Kwa mujibu wa Dkt. Kalemani mkandarasi anaendelea kufunga transforma na Mita za Luku katika vijiji 34 vilivyosalia kwa Wilaya ya Tunduru ili viweze kupatiwa huduma ya umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
Serikali: Hakuna Sababu Ya Kuagiza Transforma Za Umeme Wakati Zinatengenezwa Nchini Serikali: Hakuna Sababu Ya Kuagiza Transforma Za Umeme Wakati Zinatengenezwa Nchini Reviewed by WANGOFIRA on 20:06:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.