Shirika la AGPAHI Lazindua Kambi ya Watoto na Vijana Mkoani Kilimanjaro
Watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya
Shinyanga na Simiyu wameweka kambi ya siku tano mkoani Kilimanjaro ili
kupatiwa maarifa mbalimbali yatakayowawezesha kukua na kuishi katika
matumaini chanya,Mwandishi wetu Kadama Malunde,anaripoti zaidi.
Kambi hiyo inayoitwa Kambi ya Ariel ni
ya sita kufanyika tangu shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids
Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya
Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi katika mikoa ya Shinyanga,Simiyu na
Geita lilipoanzishwa mwaka 2011.
Kambi hiyo imeanza siku ya Jumatatu,Juni 13,2016 katika hoteli ya Lutheran Uhuru mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo maafisa kutoka AGPAHI ,madaktari bingwa wa watoto,wataalaamu wa masuala ya kisaikolojia,wasimamizi wa watoto kutoka vituo vya afya na baadhi ya waandishi wa habari walihudhuria.
Akifungua
kambi hiyo, Mkurugenzi wa miradi wa shirika la AGPAHI Tanzania, Dr.
Amos Nsheha alisema malengo ya kambi hiyo ni kuwakutanisha watoto na
vijana wenye umri kati ya miaka 12 mpaka 19 ili kuwafundisha namna ya
kuwa wafuasi wazuri wa dawa na kujifunza kuhusu masuala ya ujana na VVU.
Aliyataja
malengo mengine kuwa ni kuwafundisha namna ya kukabiliana na msukumo
rika,stadi za maisha,namna ya kuzuia maambukizi ya VVU kwa watu
wengine,kubadilishana uzoefu na kufanya utalii wa ndani.
“Hii ni kambi ya 6,tumewahi kufanya kambi kama hii mkoani
Kilimanjaro,Mwanza na Kagera.Katika kambi hizi 6 tumefanikiwa kuwaita
vijana wanaoishi na VVU takribani 300.Vijana wanaohudhuria kambi
huchaguliwa kutoka kwenye vilabu vilivyoanzishwa kwenye mikoa
tunakofanya shughuli zetu, na mpaka sasa tuna vilabu 50 vya watoto na
vijana wenye umri kati ya miaka 6 hadi 19 na kwenye vilabu hivyo tuna
watoto na vijana takribani 2500”,alieleza Dr.Nsheha.
“AGPAHI ni asasi ya kitaifa isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa mwaka 2011
kwa msaada wa Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (EGPAF) kwa
lengo la kutokomeza Ukimwi kwa watoto nchini Tanzania,tukiwa na lengo la
kuwajali watoto wakue na kuishi kwenye matumaini chanya”,alieleza Dr.
Nsheha.
Akielezea historia ya jina la Shirika, Dr. Nsheha alisema,AGPAHI ilipewa
kwa heshima jina la Ariel Glaser, msichana aliyefariki kwa Ukimwi mwaka
1988 akiwa na umri wa miaka 8. Ariel aliambukizwa virusi vya Ukimwi na
mama yake Elizabeth Glaser (mwanaharakati wa Ukimwi kwa watoto
wachanga),aliyepata VVU baada ya kuongezewa damu wakati akijifungua na
bila kujua alimwambukiza binti yake Ariel wakati wa kumnyonyesha.
“Miongoni mwa kazi tunazofanya ni kupambana ili kuzuia maambukizi kutoka
kwa mama kwenda kwa mtoto na kutoa tiba kwa wale ambao tayari wanaishi
na VVU/Ukimwi pamoja na wazazi na familia kwa ujumla”, alieleza Dr.
Nsheha.
“AGPAHI imekuwa ikitekeleza miradi minne katika mikoa hii,ambayo ni
kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU,kutoa huduma
ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,kutoa
huduma ya uchunguzi wa awali na tiba ya saratani ya shingo ya kizazi na
kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango hasa kwa wagonjwa
wanaoishi na VVU”, alieleza Dr. Nsheha.
Alisema hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2015, AGPAHI imefanikiwa kupata
watu wanaoishi na VVU takribani 150,000 waliokuwa kwenye huduma ya
matunzo ,ambapo kati yao watoto wenye umri chini ya miaka 15 walikuwa
takribani 9000, waliokuwa kwenye dawa kati ya watu 150,000 ni wagonjwa
58,000 tangu kuanza kwa mradi wa tiba na matunzo kati yao wanaoendelea
kutumia dawa ni takribani 49,000.
“Lengo ni kuwafikia watu 110,000 kwenye matibabu,bado tuna jukumu kubwa
la kuwabaini watu walio na maambukizi ya VVU hasa watoto ,kwani ndiyo
kipaumbele chetu.Katika jitihada zetu tunajitahidi watoto waliozaliwa na
mama wenye VVU ,waweze kuishi maisha yao yote ili kufanikisha ndoto zao
za kimaisha na wawe na matumaini chanya”,alisema Dr. Nsheha.
Tangu kuanzishwa kwake,AGPAHI inafanya kazi zake katika mikoa ya
Shinyanga,Simiyu na Geita kwa kuunga mkono utoaji huduma kamilifu za
VVU/Ukimwi ikishirikiana na halmashauri 14 za wilaya pamoja na
hospitali,zahanati na vituo vya afya vya serikali na taasisi mbalimbali
zikiwemo za kidini.
AGPAHI inatekeleza majukumu yake kwa hisani ya watu wa Marekani kupitia
Centres for Disease Control and Preventation (CDC),shirika la misaada la
Marekani(USAID) chini ya mpango wa dharura wa rais wa Marekani dhidi ya
Ukimwi (PEPFAR), Mfuko wa idadi ya watu duniani (UNFPA) na mfuko wa
kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF).
Miongoni mwa malengo ya AGPAHI ni kuboresha afya ya watoto na familia
kwa kutokomeza VVU/Ukimwi kwa kujengea uwezo,utetezi,huduma za kinga na
tiba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kubuni na kutekeleza
mikakati muafaka kwa afya bora.
Angalia picha na matukio yaliyojiri katika Kambi ya Watoto na Vijana siku ya kwanza.
Mkurugenzi wa miradi ya shirika la AGPAHI Tanzania, Dr. Amos Nsheha akitoa hotuba ya ufunguzi wa Kambi ya Watoto na Vijana
Baadhi ya watoto kutoka mikoa ya Shinyanga Simiyu wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika ukumbi wa mkutano
Meneja Mawasiliano na Huduma za Jamii kutoka AGPAHI, Jane Shuma akitambulisha na kuwakaribisha wageni na washiriki wa kambi.
Watoto na vijana wakiwa ukumbini
Afisa miradi huduma unganishi kwa jamii kutoka AGPAHI, Cecilia Yona akizungumza ukumbini
Afisa miradi huduma unganishi kwa jamii AGPAHI, Richard Kambarangwe akisisitiza jambo
Daktari Bingwa wa Watoto, Dr.Rose Mende kutoka hospitali ya rufaa ya
Mkoa wa Arusha,Mount Meru akitoa maelezo kuhusu huduma za uchunguzi na
matibabu kwa watoto na vijana wakiwa kambini
Mmoja wa watoto akionesha kipaji chake cha kuimba
Watoto na vijana wakiimba wimbo wa pamoja ukumbini
Mshauri wa Masuala ya Kisaikolojia,Sherida Madanka kutoka Hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Shinyanga akitoa mada kuhusu stadi za maisha na
mabadiliko ya tabia kutokana na msukumo rika.
Kijana akichangia mada ukumbini
Kijana akiwasilisha kazi kwa niaba ya kikundi
Vijana wakitoa elimu kupitia igizo
Vijana wakifurahia uwepo wao kambini
Vijana wakicheza pamoja kambini
Vijana wakionesha mshikamano
Picha ya pamoja ya washiriki wa kambi
Shirika la AGPAHI Lazindua Kambi ya Watoto na Vijana Mkoani Kilimanjaro
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:05:00
Rating:
No comments: