RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 30


Mtunzi:ENEA FAIDY

....Dorice aliendelea Julia huku matone yake ya machozi yakiwa damu. Ghafla akajikuta ana uwezo wa ajabu ambao hajawahi kuufikiria kuwa nao hata siku moja. Alijibadilisha sura na kuwa kiumbe wa kutisha, macho yalikuwa kama ya paka, uso wake ukawa mweusi tii kama mkaa, kucha zake zikawa ndefu sana na meno yake mawili yalichomoza nje ya kinywa chake. Mansoor alicheka kicheko kikali cha kutisha huku sauti ya kicheko chake ikiambatana na mwangwi. Radio zikapiga mfululizo Dorice akatoweka ghafla na kumuacha Mansoor. 

Pete aliyokuwa amevalishwa Dorice ilimpa uwezo mkubwa na wa ajabu. Alipata uwezo wa kupotea na kujibadilisha kadri atakavyo lakini sharti kubwa alilotakiwa kufanya ilikuwa ni lazima arudi tena kwa Mansoor baada tu ya kumaliza kazi yake inayompeleka duniani.

Dorice alikuwa ametokeza katika eneo lenye Giza Giza lilitawaliwa sauti za wadudu. Palikuwa na utulivu mkubwa sana , kwani eneo lile halikukaliwa na mtu yeyote zaidi ya ndege, wadudu na wanyama wadogo wadogo. Dorice alibaki anajishangaa, alijiuliza amefika vipi eneo lile akiwa peke yake bila Mansoor.

"Ina maana nimekuwa na nguvu za kijini?" Alijiuliza Dorice. Ghafla upepo mkali ukapuliza eneo lile, Dorice alitazama huku na kule ili kujua nani alikuwa mgeni wake kwa wakati ule. Ghafla Mansoor akajitokeza akiwa anacheka kicheko cha kutisha sana kisha akapiga hatua za taratibu kumsogelea Dorice.

"Kwanini umefika huku?" Aliuliza Mansoor kwa ghadhabu.
"Sijui nimefikaje" alijibu Dorice.
"Muda wako wa kuondoka kwenye himaya yangu bado Dorice, nilikuwa na jaribu kukupa ladha ya vile utakavyokuwa baada ya wakati kutimia" alisema Mansoor.
"Kwahiyo unataka nirudi?"
"Ndio.. Tunarudi wote".

"Hapana Mansoor sitaki kurudi tena Kule" alisema Dorice.
"Ni lazima urudi maana bado sijakupa maelekezo"
"Hayo maelekezo nipe hapa hapa"
"Haraka haraka ilimfanya chura apate ngozi ya mabaka"
"Hata hivyo siwezi kurudi".

Yalizuka mabishano makali baina ya Dorice na Mansoor kwani Dorice hakutaka kurudi kwenye himaya ya Mansoor tena. Alitaka aachwe huru na arudi kwao, lakini mkongwe ni mkongwe tu licha ya mabishano Yale Mansoor aliibuka mshindi baada ya kumchukua Dorice kinguvu kwa kutumia uwezo mkubwa wa kijini alionao. Katika eneo walilokuwepo ukatokea upepo mkali na kuwavuta wote wawili kisha ndani ya muda mfupi walijikuta wametokea katika himaya ya akina Mansoor. Dorice alikasirika sana.

*****

"Mama mbona sikuelewi" aliuliza mlinzi kwa hofu huku akimtazama Mama Eddy kwa woga.
"Wewe!" Alisema mama Eddy akiwa amevimba kama mbogo huku akimsonta mlinzi yule kwa kidole chake na kumfanya mlinzi yule atawaliwe na hali ya sintofahamu.
"Nimefanya nini mama?".

"Kaa mbali na Eddy... Nakusisitiza Tena kaa mbali na Eddy la sivyo utakiona cha mtema kuni paka shume wewe!"alisema Mama Eddy huku akipiga hatua na kutaka kuondoka.

Alitembea kwa hatua chache tu kisha akamgeukia tena mlinzi na kumuonya vikali kuwa asiwe karibu na Eddy. Mlinzi yule hakuelewa mwanamke yule ana maana gani kumwambia vile. Alibaki na maswali mengi kichwani mwake huku akimsindikiza kwa macho mwanamke yule aliyejongea taratibu machoni mwake baada ya kuingia ndani ya jumba la kifahari la Mr Alloyce. Mlinzi aliachana na mwanamke yule kisha akaendelea na kazi zake za kupunguza maua.

Mama Eddy aliingia ndani na kumkuta Mr Aloyce akiwa ameketi kwenye sofa huku uso wake ukidhihirisha furaha kubwa aliyonayo moyoni mwake. Alifurahia sana kurudi kwa mkewe katika familia yao ili waendelee kuijenga na kuidumisha furaha yao ikiwa ni pamoja na kutafuta tiba ya tatizo la mtoto wao wa pekee.

"Mwanangu yuko wapi?" Aliuliza Mama Eddy huku akitabasamu. Baba Eddy alinyanyua kichwa chake na kupaza sauti yake akimwita mwanaye. Bila kuchelewa Eddy alirudi sebuleni na kumkumbatia mwanamke yule aliyedhani ni mama yake. 

"Mama bora umerudi.. Tulikuwa wapweke sana humu ndani!" Alisema Eddy na kumfanya mwanamke yule atabasamu kwa furaha.
"Nimerudi mwanangu" alisema mwanamke yule. Familia ile ikarejewa na furaha iliyokuwa imepotea ndani ya muda mfupi uliopita.

Wakiwa wameketi sebuleni pale kwa utulivu wa hali ya juu, ghafla simu ya Mr Aloyce iliita, akaitoa mfukoni na kuangalia nani alimpigia. Alipotazama tu akaona namba aliyoisevu "Shem Dar" akashtuka kidogo kisha akapokea.

"Ndio..ndio shemeji!" Alisema.
"Nipo njiani na sio muda nafika hapo nyumbani" ilisikika sauti ya Dada yake Mama Eddy.
"Unakuja hapa kwangu?"
"Ndio.. Si ulisema kuna matatizo!"
"Mh Haya karibu"

Baada ya mazungumzo hayo simu ikakatika ndipo Mr Aloyce akaona si vyema kumficha mkewe kuhusu jambo lile. Akamweleza kila kitu kuhusu chanzo cha Dada yake kufika nyumbani kwao.

"Ulimwambia kuna tatizo gani?" Alisema mama Eddy kwa mshangao.
"Nilimwambia tu kuna tatizo na sikumweleza ni tatizo gani. "
"Vizuri! Akija hapa usimweleze chochote kuhusu suala la Eddy" alisema Mama Eddy. Kauli hiyo ilimshtua Mr Aloyce kwani hakuona haja ya kumficha shemeji yake kuhusu jambo lile.

"Kwanini nisimwambie? Hujui kama anaweza kutusaidia.. Pengine hata kwa ushauri..." Alisema Baba Eddy.
"Nimesema usimwambie chochote.." Alisema Mama Eddy na kuinuka kitini kisha akaondoka sebuleni pale na kuwaacha Mr Aloyce na Eddy.

Mr Aloyce alibaki na mshangao sana kwani alikumbuka jinsi ambavyo Mama Eddy wanavyopatana na kuelewana kama mapacha iweje Leo amfiche matatizo yake?. Alishindwa kuelewa sababu akabaki kimya kitini pale. 

*****
 
 Mama Pamela na mwanaye waliendelea kuusubiri usingizi uwachukue ili kupambazuke haraka. Usingizi ulichelewa sana kuwachukua lakini haukuwaacha kabisa. Baada ya kuusubiri kwa muda mrefu wakiwa na hofu kupita kiasi hatimaye usingizi ukawapitia. Kila mmoja alilala fofofo kutokana na uchovu pamoja na mihangaiko mingi iliyosababishwa na mauzauza ya usiku ule.

Hatimaye kukapambazuka lakini bado wanafamilia ile walikuwa wapo katikati ya usingizi. Mlango wa chumba iligongwa na kumfanya mama Pamela ashtuke usingizini na kusikiliza nani aligonga.

"Mama" sauti nyororo ya Doreen ilipenya masikioni mwa Mama Pamela ikiwa na wingi wa adabu na upole uliokithiri. Bila kusita mama Pamela Aliitikia wito na kumsikiliza Doreen anahitaji nini.

"Hauendi kazini? Pia Dada Pamela haendi shule?" Aliuliza Doreen.
"Hatuendi... Wote tupo likizo.." Alijibu Mama Pamela .
"Sawa mama.. Nilifikiri mmesahau.. Ngoja niendelee na kazi"
"Hebu njoo kwanza.." Mama Pamela alimwita Doreen na kutaka aingie chumbani.
"Abee mama" Doreen aliitika kwa heshima na kusogelea karibu kabisa na kitanda cha Mama Pamela.

"Hivi usiku ulilala salama?"
"Ndio kwani vipi?" Aliuliza Doreen kwa mshangao.
"Mh! Kweli?"
"Ndio.. Kwani nini kilitokea"
"Duh basi kama ulikuwa salama sawa... Hakuna tatizo!" Alisema mama Pamela.

Doreen alijifanya kushangaa kupita kiasi, lakini hakuuliza zaidi. Aliachana nao na kwenda jikoni kuandaa chai.Alichemsha maji na kuweka majani ya chai. Na baada ya kuhakikisha imechemka vizuri akaiipua vizuri kisha akatemea mate halafu akaiweka kwenye chupa ya chai huku akicheka.

"Mtakoma mwaka huu..." Alijisemea Doreen kisha akapeleka chai mezani. Akarudi jikoni na kuchemsha maini ya ng'ombe lakini alipokuwa akichemsha maini yale alichanganya na maji Fulani yaliyokuwa kwenye kichupa Fulani kidogo.

"Na mtakula sana uchafu wangu... Huu mkojo tu! Bado vingine vinakuja" alisema Doreen kwa sauti ya chini.Maini Yale yalichemka vizuri na kutoa harufu ya kuvutia sana. Baada ya kuyaivisha vizuri akachukua mayai ns kuyakaanga vizuri kisha akapeleka mezani na kuandaa vizuri.

Majira ya saa tatu asubuhi Mama Pamela na mwanae waliamka. Wakaoga na kwenda chumba cha kulia chakula.
"Doreen kumbe umeshaandaa kila kitu" alishangaa Mama Pamela.
"Ndio mama! Karibuni" Aliitikia Doreen.
"Asante.." Alisema mama Doreen huku akiketi na kusogeza karibu mikate, akaipaka blueband.

"Mbona wewe huji kula?" Alimuuliza Doreen.
"Mimi tayari.. Hivyo ni kwaajili yako na dada Pamela"
"Oh sawa.. Mwite Dada yako aje kula maana ni mvivu kweli" alisema mama Pamela huku akianza kukishughulikia chakula kile. Punde tu Pamela naye akaenda mezani pale na kuanza kula.

Wakati huo Doreen alikuwa pembeni yao akiwatazama jinsi wanavyokula chakula kile kichafu. Aliwasikitikia sana moyoni mwake lakini wao walimmwagia sifa tele kwa utamu wa chakula kile. Kila mmoja alimsifu Doreen kwa kumwambia ni fundi wa Mapishi.

"Doreen mwanangu.. Nataka nikuulize kitu" alisema Mama Pamela huku akimeza funda moja la chai na kutua kikombe taratibu kwenye meza nzuri na safi ya kioo. Kauli ile ilimshtua kidogo Doreen na kumfanya amuulize vizuri mama Pamela.
"Kitu gani mama?"

ITAENDELEA.......
RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 30 RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 30 Reviewed by WANGOFIRA on 01:06:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.