Serikali: Hatuna ushahidi wa kuzihukumu shule za Feza, Hivyo Hatuwezi Kuzifunga


SERIKALI imesema haina ushahidi wa kutosha kuzitia hatiani shule za Feza nchini zinazodaiwa kumilikiwa na mmoja wa wananchi wa Uturuki anayetuhumiwa kujihusisha na ugaidi na kuitaka Serikali ya Uturuki kuwasilisha taarifa zenye ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma hizo.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga.

Alisema walipokea madai kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini kuwa shule hizo zinamilikiwa na mmoja wa wananchi wa nchi hiyo anayejihusisha na ugaidi.

Balozi Mahiga alisema katika madai ya ubalozi huo, shule hizo ni miongoni mwa miradi inayomilikiwa na mtuhumiwa huyo na kwamba, baadhi ya walimu wake hutumia mbinu za kigaidi kufundisha wanafunzi.

Akijibu tuhuma hizo, Balozi Mahiga alisema serikali kabla ya kutoa kibali kwa mwekezaji au mfanyabiashara yeyote kuendesha shughuli zake nchini, vyombo vya usalama nchini, hufanya upelelezi wa kina na wamejiridhisha kwamba wafanyabiashara wa Uturuki waliopo nchini wanafanya biashara halali.

“Ni kweli tumepokea tuhuma kutoka kwa Ubalozi wa Uturuki nchini kuhusu shule za Feza kwamba ni sehemu ya makundi ya kigaidi, lakini hatuwezi kuzitia hatiani shule hizo hadi tuletewe ushahidi wa kutosha,”alisema Balozi Mahiga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Feza, Habib Miradji alisema shule hizo ni za asasi iliyosajiliwa kisheria na Serikali ya Tanzania hivyo ni mali ya Tanzania na endapo kuna kitu au tatizo ni lazima wawasiliane na serikali na watafika kukagua ili kama kuna lolote baya hatua zichukuliwe.

Aidha alisema kwamba shule hazijafungwa.
Serikali: Hatuna ushahidi wa kuzihukumu shule za Feza, Hivyo Hatuwezi Kuzifunga Serikali: Hatuna ushahidi wa kuzihukumu shule za Feza, Hivyo Hatuwezi Kuzifunga Reviewed by WANGOFIRA on 00:36:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.