Waziri Mkuu Afungua Duka la Bohari Kuu ya Dawa "MSD" Ruangwa, Kuhudumia Hospitali 524


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua duka la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia hospitali 524 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. 




Akizindua duka hilo leo (Jumamosi, Julai 16, 2016) Waziri Mkuu amesema duka hilo litaendelea kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu katika hospitali, vituo vya afya na zahanati katika wilaya ya Ruangwa pamoja na mikoa na wilaya za jirani. 



Duka hilo ni la sita kufunguliwa tangu Mhe. Rais Dk. John Magufuli alipotoa agizo kwa MSD kufungua duka la dawa ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo mengine yako katika mikoa ya Mwanza (Sekou Toure), Arusha (Mount Meru), Mbeya (karibu na hospitali ya mkoa) na Geita (hospitali ya wilaya ya Chato). 



“Duka hili litasaidia kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati na kwa gharama nafuu, hivyo nawaomba mlitumie duka hili,” amesema. 



Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa benki ya NMB, kikosi cha SUMA JKT na MSD kwa kufanikisha ujenzi wa duka hilo ambalo litaimarisha upatikanaji wa dawa kwa uharaka. 



Awali Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema kuanzishwa kwa duka hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa gharama nafuu , hivyo kuondoa usumbufu kwa wagonjwa wa kwenda kuzitafuta katika ya mbali na kwa bei kubwa.



“Nitoe mfano wa tofauti wa bei za dawa kati ya maduka yetu na mengine, dawa ya sindano ya diclofenac tunauza sh. 250 huku mitaani ni sh. 1,000 hadi 1,500 , ampliclox dozi moja MSD sh. 1,500 mtaani sh. 3,500 na Ciprofloxacin MSD sh. 100 na mtaani sh. 500 hadi 1,000,” amesema. 



Mkurugenzi huyo amesema lengo la maduka hayo si kuuza dawa reja reja, nia yao ni kuziuzia hospitali, vituo vya afya na Zahanati ili wagonjwa wanapokwenda huko kupatiwa huduma wasikose dawa kwa wakati. 



Akizungumzia kuhusu gharama za ujenzi wa duka hilo Bwanakunu mesema umegharimu sh.milioni 59 ambapo kati yake MSD imetoa sh. milioni 29 na benki ya NMB imetoa sh. milioni 30. 



“Mbali na gharama za ujenzi MSD tumenunua na kufunga vifaa vya TEHAMA kwa sh milioni 17 na mtaji wa dawa wa sh. milioni 37, ambapo imetenga sh. milioni 100 kwa ajili ya dawa za duka hilo.



Amesema duka hili litaendeshwa na kusimamiwa na MSD kwa muda wa mwaka mmoja na kisha wataikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa ajili ya kuliendeleza ambapo litaisaidia katika kuiongezea mapato.
Waziri Mkuu Afungua Duka la Bohari Kuu ya Dawa "MSD" Ruangwa, Kuhudumia Hospitali 524 Waziri Mkuu Afungua Duka la Bohari Kuu ya Dawa "MSD" Ruangwa, Kuhudumia Hospitali 524 Reviewed by WANGOFIRA on 20:49:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.