Wanawake walia Magufuli ‘kuwabania’ katika uteuzi

Mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa kijinsi nchini yamesema uteuzi wa nafasi muhimu za uongozi serikalini unaofanywa na Rais John Magufuli, hauzingatii hali halisi ya uwakilishi wa kijinsia. 

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mashirika hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema licha ya kupiga kelele tangu uteuzi wa Baraza la Mawaziri kuwa haukuzingatia usawa huo, bado hali inaonekana kuwa tete kwa upande wa wanawake. 

Alisema katika baraza hilo, kati ya mawaziri 19, wanne pekee ndiyo wanawake sawa na asilimia 21.1 ya mawaziri wote ikilinganishwa na uteuzi wa baraza la Serikali ya Awamu ya Nne ambalo lilikuwa na mawaziri wanawake 10 sawa na asilimia 33.3. 

Alisema manaibu waziri kati ya 16 waliopo, wanawake ni watano sawa na asilimia 31.25. 

“Ukiangalia upande wa makatibu wakuu, walioteuliwa ni 29 kati ya hao, wanaume ni 26 sawa na asilimia 89.7 huku wanawake wakipungua kutoka watano sawa na asilimia 21.7 ya mwaka 2014 hadi kufikia watatu sawa na asilimia 10.3 kwa sasa,” alisema Liundi. 

Alisema uteuzi wa wanawake katika nafasi hizo umepungua kwa asilimia 10. Katika nafasi ya wakuu wa mikoa, Liundi alisema idadi ya wanawake imeshuka zaidi, kati ya wakuu wa mikoa 26 Tanzania Bara, 21 ni wanaume sawa na asilimia 80 na wanawake ni watano sawa na asilimia mbili.
Kadhalika, alisema idadi ya wakuu wa wilaya imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari mwaka jana ambako wanawake walikuwa asilimia 35.07: “Kwa maana nyingine, hapa uteuzi umepungua kwa asilimia saba.” 
Liundi alisema mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe na Singida haina wawakilishi wanawake kwa nafasi ya ukuu wa wilaya. 

“Hii iko hata kwenye nafasi za makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, hatuoni idadi ya wanawake ikiongezeka na badala yake inashuka,” alisema. 

Mwakilishi wa Taasisi ya Women Fund Tanzania (WFT), Dk Dinna Mbaga alisema Tanzania ni kati ya mataifa duniani yaliyoridhia na kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu ikiwamo ushiriki katika ngazi zote za uamuzi, lakini haitekelezi mikataba hiyo kwa ridhaa mpaka isukumwe na asasi za kiraia jambo linaloleta ukakasi. 

Alisema miongoni mwa mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR: 1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979), Mpango kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo na Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). 

Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo alisema Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya 2025, imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwa na jamii yenye maono ya kimaendeleo na utamaduni wezeshi kwa wanawake na makundi mengine.
Wanawake walia Magufuli ‘kuwabania’ katika uteuzi Wanawake walia Magufuli ‘kuwabania’ katika uteuzi Reviewed by WANGOFIRA on 00:11:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.