Mtatiro Amtaka Profesa Lipumba Apumzike Uongozi

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro amesema hana mpango wa kugombea nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho, licha ya kuwepo kwa msukumo mkubwa wa kumtaka agombee.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Mtatiro alisema kwa kipindi kirefu amekuwa akipata msukumo kutoka kwa viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya, wabunge, wafuasi na makada wa chama hicho kumtaka ashiriki katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya uenyekiti.

“Katika kipindi chote cha misukumo hiyo nimekuwa nikiwajibu wahusika wote kuwa “sina nia ya kuchukua uongozi wa juu wa chama” kwa sababu bado nahitaji muda wa kujiimarisha,” alisema Mtatiro katika taarifa yake.

Alisema hata aliposhauri kuwa Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anapaswa kupumzika wapo walioona kuwa anatumia nafasi hiyo kuutaka uenyekiti wa CUF jambo ambalo alisema si kweli.

Aidha, Mtatiro alisisitiza kuwa hajawahi kuwa na nia ya kuutaka uenyekiti wa CUF lakini hadi sasa msimamo wake ni kuwa haungi mkono Profesa Lipumba kurudi katika nafasi yake kwa sababu siasa za sasa zinahitaji viongozi wapya na wanaoweza kutazama mambo kisasa kwa mahitaji ya kizazi kipya.

“... Na kwa sababu Profesa Lipumba anayo heshima kubwa kwa CUF na watanzania, ni muhimu zaidi alinde heshima yake na abaki kuwa mshauri mkuu wa chama. CUF ya sasa inahitaji mwenyekiti imara anayeweza kukisimamia chama na kikajijenga lakini pia mwenye uwezo na ushawishi wa kufanya siasa za ushirikiano na haki,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Mtatiro alisema anawatakia kila la heri wanachama wa CUF ili waweze kuchagua mwenyekiti mzuri kwa ajili ya kukiendeleza chama hicho, na kusisitiza kuwa jukumu lake litaendelea kukisaidia chama katika masuala mbalimbali ya kiushauri.
Mtatiro Amtaka Profesa Lipumba Apumzike Uongozi Mtatiro Amtaka Profesa Lipumba Apumzike Uongozi Reviewed by WANGOFIRA on 00:12:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.