Lowassa Awapa Chadema ‘ukweli mchungu'


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewataka viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokatishwa tamaa na hali ya kisiasa nchini hususan marufuku za mikutano yao ya kisiasa pamoja na misukosuko mingine wanayopitia.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ameyasema hayo jana jijini Arusha alipokutana na Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri zinazoongozwa na Chama hicho. 

Aliwataka wasiogope bali washikamane zaidi na kutambua ukweli kuwa hakuna Serikali yoyote duniani inayovipenda vyama vya upinzani.

Alisema kuwa Chama hicho kinatakiwa kujikita katika kushikamana na wananchi zaidi kwani uchaguzi wa mwaka jana ulionesha dhahiri kuwa wana imani na vyama vya upinzani na hadi sasa bado wananchi wana imani kubwa nao.

“Kuna uanaharakati na kuna siasa. Chama chetu cha Chadema ni hodari sana, tume-graduate. Tumevuka ngazi ya uanaharakati. Uanaharakati ni mzuri lakini unafika mahali unavuka ngazi katika kitu kingine ambacho ni chama cha siasa,” alisema.

“Chama cha siasa kazi yake ni kukamata dola. Hakuna kitu kingine duniani. Kwahiyo mnapokaa hapa mnajipanga kukamata dola na sio kitu kingine. Maandamano ni process tu, na sisi tumekaa hapa kutafuta namna ya kukamata dola, wanataka hawataki wanajua hilo. 

"Na wenyewe watakazana kuzuia tusikamate dola. Mliona walivyotufanyia kwenye uchaguzi, kwa gharama yoyote. Na sisi kwa gharama yoyote tutataka tuwanyang’anye dola na ndio tunakuwa chama cha siasa,” aliongeza.

Alisema kuwa CCM wanahofu kwakuwa bado wanakumbuka walichokipata wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na akawataka Chadema kutofanya kazi kwa mazoea bali kukijenga chama kuanzia ngazi za mashina na matawi.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliwataka Chadema pamoja na vyama vingine vya upinzani kulinda Ukawa kwani ndio chanzo kikuu cha mafanikio yao. Alisema wanapotofautiana wakae chini na kutafuta ufumbuzi.

“Ndugu zangu tulinde umoja wetu na tuhakikishe kuwa Ukawa inaendelea kuwapo hasa. Umoja wetu ndio nguzo kubwa na tutumie busara kukosoana. Tunapokosea tuache maneno ya mitaani. Tuwalinde viongozi wetu,” alisema.

Mwanasiasa huyo mkongwe alitoa wito kwa viongozi hao wa halmashauri kuhakikisha wanafanya kazi nzuri na kuwaletea maendeleo wananchi ili wasione ‘bora CCM’. 

Aliwataka kuhakikisha hawaangalii maslahi binafsi bali maslahi ya wananchi na kujieupusha na migogoro na viongozi wa CCM watakaotaka kuwakwamisha katika shughuli zao.
Lowassa Awapa Chadema ‘ukweli mchungu' Lowassa Awapa Chadema ‘ukweli mchungu' Reviewed by WANGOFIRA on 00:14:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.