India yaipatia Tanzania dola milioni 500 za Kimarekani kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo

India imeipatia Tanzania dola za Kimarekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina nchi hizi mbili.

Hayo yamesemwa leo  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia mgeni wake , Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi,Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Tunaishukuru India ambayo imeonyesha utayari wa kushirikiana nasi kiuchumi katika kilimo, TEHAMA, maji, Elimu, Afya na Ulinzi,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amesema ushirikiano wetu na India utatoa fursa kwa Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda kwani katika ziara hii Waziri Mkuu ameambatana na wafanyabiashara takriban 50 ambao wanaangalia fursa za kibiashara hapa nchini.

“India ni mdau wetu mkubwa wa  kibiashara  na uhusiano huu umekuwa ukikua kwani mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini India yameongezaka toka thamani ya  dola za kimarekani milioni 187 mwaka 2005 hadi dola bilioni 1.29 mwaka 2015,”alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa India itatoa fedha kwa nchi ya Tanzania kwa ajili ya kilimo cha Dengu ambayo ni fursa ya ajira kwa watanzania na kuinua kipato cha wananchi.

Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na miradi ya India ikiwemo mradi unaojulikana kama Making India, mradi ambao unatumia malighafi zinazopatikana nchini na kutumia nguvu kazi ya nchini ambao utapunguza tatizo  la ajira katika Taifa la Tanzania.

Amebainisha kuwa India iko tayari kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya gesi ikizingatiwa kuwa aina mbali mbali za gesi zinazidi kugunduliwa hapa nchini. Katika suala la gesi India iko tayari kutoa utaalamu na wataalamu kwa ajili miradi ya gesi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa India , Mhe. Narendra Modi ameishukuru Tanzania kwa ukarimu alioupata hapa nchini na akaahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili.
 
Amesema India italeta watu wake, utaalaamu na teknolojia yake kwa Tanzania, jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa kiuchuni kati India na Tanzania.

Waziri Mkuu huyo amemaliza ziara yake ya kiserikali  ya siku mbili nchini na kuondoka kuendelea na ziara katika nchi nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.
India yaipatia Tanzania dola milioni 500 za Kimarekani kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo India yaipatia Tanzania dola milioni 500 za Kimarekani kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo Reviewed by WANGOFIRA on 20:57:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.