MIKAKATI YA AWAMU YA TANO KUBORESHA MASLAHI YA WAALIMUNA, BARAKA NGOFIRA

Walimu ni miongoni mwa wafanyakazi wa serikali ambao kwa muda mwingi wamekuwa wakiilalamikia serikali kuhusu mazingira na hata maslahi yao. Kwani wengi wamekuwa wakiishi mazingira magumu na hivyo kupelekea kupungua kwa ufanisi wa kazi zao.

Naandika makala haya nikijua fika maisha halisi wanayoyaishi waalimu hususani wale waishio vijijini, wengi wao wakiishi nyumba ambazo hazina hadhi nyingi zikiwa na mchwa ambao kwa namna moja ama nyingine huwasaidia kutunza karatasi za wanafunzi au daftari pale wanapozisahau.


Shule nyingi hazina nyumba za walimu jambo linalopelekea walimu wengi kujibana kwenye nyumba ambazo zipo. Au wengine kuishi kama wanafunzi wa bweni kwa kuishi kwenye chumba kimoja walimu wawili au zaidi. Jambo linalopelekea kukosa faragha miongoni mwao kwani hayo ya maisha ya kuishi hivyo yashapita, lakini kwa sababu ya kuipenda kazi yao hawana jinsi kufanya hivyo ili waweze kupata tonge la ugali.

Naandika makala haya kwanza kuwapongeza na kuwashukru walimu wa simiyu ambao wameishi jikoni kwa zaidi ya miaka miwili sasa, lakini kamwe hawakuthubutu kuacha kazi , kuomba uhamisho au kutishia kugoma kama wenzao katika maeneo mengine wafanyavyo. Kwangu mimi nawawaambia hongereni sana kwa ujasiri mkubwa mliokuwa nao wa kuishi ndoto zetu za kuwa walimu na si kama wengine ambao naweza kusema walishtuka wakajikuta wamekuwa walimu. Ambao kimsingi ndo wale wanaokuwa mstari wa mbele kudai mishahara pale inapochelewa hata kwa siku moja.

 Wamekuwa mfano wa kuigwa na kielelezo chema kwa wale wote walio kwenye fani ya ualimu na nyingine za serikali na binafsi kwa kujua shida iliyonayo serikali yetu ambayo kwa awamu hii,  Mungu akimjalia uzima Rais wetu Dr. Magufuli naamini kuwa mtajengewa mazingira bora ya kazi. Kwani kinachonifurahisha ni kwamba ameyaishi maisha ya ualimu kama kazi yake ya kwanza kuifanya miaka ile ya 1980 kabla hajaenda bungeni.

Kinachonipa ujasiri tena wa kuandika makala haya ni uchaguzi wa Prof. Ndalichako kuwa waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Kwani naye anaijua vyema hali halisi ya walimu kwani na yeye amekuwa mwalimu kwa hili sina shaka kabisa. Kuwa atajitahidi kwa kadri awezavyo kulishawishi bunge kumpa bajeti kubwa kwa ajili ya kujenga mazingira yaliyo rafiki kwa walimu.

Na si kwamba nawapigia debe walimu au kwa sababu nimetokea katika familia ya kiualimu, la hasha! Penye ukweli lazima tulonge pasipo hata kupepesa macho, ni lazima tuambizane ukweli wa mambo yalivyo.

Japo tunategemeana lakini mwalimu bado ataendelea kuwa mwalimu na mtu wa muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote. Hata kama ukibisha ukweli utabaki pale pale mwalimu anatutoa kwenye wimbi la ujinga na kutufanya tuwe welevu na baadaye wengine ugeuka na kuwadharau hasa walimu wa shule za msingi ambao kimsingi ndiyo waliowafanya wafike hapo walipo.

Jambo ambalo kiukweli ukikaa na kulitafakari kwa kina tena mara mbilimbili utagundua thamani aliyonayo mwalimu katika jamii zetu. Nakumbuka maadui watatu ambao Hayati Baba wa Taifa hili Mwalimu J.K Nyerere alisema nchi hii inakabiliwa na maadui watatu ambao ni Ujinga, Umaskini na Maradhi. Sasa kama utamdharau mwalimu nani atautoa ujinga vichwani mwetu?

Mwingine anaweza sema nitaenda kujisomea maktaba au kwenye mtandao kwa sababu ya kukua kwa teknolojia na kusahau enzi zile alizokuwa anakimbia na vizibo vya soda akifundishwa kuhesabu, pia kipindi kile anaandika chini akijifunza kuandika “a, e, i, o na u”.

Pia kwa wale waliokuwa na akili nzito ya kushika wanasahau jinsi ambaavyo walitandikwa japo kidogo na kuambiwa hii ni “a au ni u” au kuhesabu namba 1 mpaka 10. Ambaye pasipo shaka yeyote vilimpa shida sana kukariri lakini leo utashangaa anakuambia mwalimu hana faida kwangu kisa tu yeye si mwalimu.

Ebu tugeuze mielekeo ya mawazo yetu ili tuiunge mkono serikali yetu ya awamu ya tano ambayo ninaamini ina dhamiri ya dhati kabisa ya kuondoa ujinga kwa watanzania wote. Na kamwe ujinga hauwezi kuondoka pasipo walimu kutengenezewa mazingira mazuri ya kufanyia kazi, ikiwemo mishahara mizuri, kujengewa nyumba ambazo watishi na kufurahia kazi yao.

Narudia kuwapongeza sana walimu wawili wa Simiyu waliovumila kuishi jikoni kwa muda wa miaka miwili na zaidi pia wale ambao wanavumila kuishi na michwa ndani ya nyumba zao ambayo inawasaidia kutunza karatasi na madaftari ya wanafunzi pale wanaposahau au kudondoka chini, bila kuwasahau wale wanaoishi nyumba zilizo sawa na mapango ambazo ukiziangalia kwa nje hauwezi kuamini kuna binadamu anayeishi ndani ya jengo hilo.

Huu ndio uvumilivu na uthamani wa kazi ninaouandikia makala haya waswahili husema “Heshima kazi” au “Acha kazi uone uthamani wake”. Haya ndiyo maisha halisi ya walimu ambao wamemfundisha kila mtu ambaye kwa namna moja ama nyingine anaajiona aana umuhimu mkubwa kwenye jamii kuliko mwalimu wake.

Hivyo basi ni ombi langu kwa wadau wa Elimu nchini Tanzania waunganishe nguvu na watanzania wote kuhamasishana kujenga nyumba za walimu ili walimu wanapoajiriwa waweze kuishi maisha yenye uafadhali. Ambayo itawasaidia kuwajengea moyo wa wao kujituma na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kujengewa mazingira rafiki. Kwani hata wataalamu wa masuala ya kitaaluma wanashauri kuwa ili ufanisi wa kazi uwe wa weredi zaidi, mazingira bora ya kufanyia kazi ni muhimu zaidi ili kuongeza mazao na mapato ya kazi wanazozifanya.

Pia nina imani kubwa na serikali ya awamu ya tano chini ya waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Ndalichako ambaye kitaaruma ni mwalimu. Kuwa maisha bora ya walimu yataboreshwa ili waweze kuongeza ufanisi wa kazi zao za kuondoa ujinga kwa watoto na wadogo zetu ambao kesho na kesho kutwa watakuwa viongozi wakubwa kwenye nchi yetu na duniani kwa ujumla.

Kwa sababu pia dhamira ya serikali ya awamu ya tano ni kujenga Tanzania yenye wataalamu waliobobea kutokana na Elimu inayopatikana kutoka kwenye Shule na Vyuo vya hapa nchini. Ni imani yangu kuwa waziri mwenye dhamana atapambana vilivyo ili kuhakikisha kuwa tunajenga Tanzania ya watu wenye Fikra chanya na watu wanaofikri mara mbilimbili ili kuvuta mataifa mengine ya duniani yaweze kuleta watu wao kuja kusoma hapa nchini. Kama sisi tupelekavyo wataalamu nje ya nchi kwenda kusoma na kupata ujuzi mbalimbali na kuja kuutumia hapa nchini.

Hivyo ni ombi langu kwa waanaanchi na wadau wa elimu kuunga mkono serikali kwa kujitolea kwa mioyo ya dhati, kama tulivyoshiriki kwenye ujengaji wa shule na maabara za shule za sekondari. Tufanye hivyo kwa kushirikiana kujenga nyumba za walimu ili wajapo kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi wafanye kazi na si kila siku kulalamika. Kwani muda wa malalamiko umeshapita na Sasa ni Kazi Tu. Ili wale wasioweza kazi wakae pembeni na wa kazi waendelee tuijenge Tanzania iliyo imara na kuwa mfano wa kuigwa.


Makala haya yameandaliwa na mwanafunzi wa Mawasiliano kwa Umma katika Shule Kuu ya Uhandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901, 0716216249 au barua pepe ya barakangofira@gmail.com
MIKAKATI YA AWAMU YA TANO KUBORESHA MASLAHI YA WAALIMU MIKAKATI YA AWAMU YA TANO KUBORESHA MASLAHI YA WAALIMU Reviewed by Unknown on 11:18:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.