MWANASHERIA MKUU WA TBS AHUKUMIWA JELA MIAKA MITANO
Baada ya kuachiwa huru siku ya Jumatano
na kukamatwa tena, jana aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54) amehukumiwa kulipa faini
ya Sh milioni 13.9 au kifungo jela miaka mitano baada ya kusomewa upya
mashtaka na kukiri.
Bitaho alifikishwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana
asubuhi na kusomewa mashitaka nane likiwemo la kufanya kazi nchini bila
kibali na kutoa taarifa za uongo.
Bitaho ambaye ni Raia wa Burundi, alifutiwa mashtaka yake, na baadae
kukamatwa, alisomewa hukumu hiyo, na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria
Nongwa.
Akisoma hukumu hiyo Nongwa alisema kuwa mahakama imesikiliza maombi ya
pande zote mbili na kwamba katika kosa la kwanza hadi la saba mshitakiwa
atatakiwa kulipa faini ya Sh laki tano au kifungo jela kuanzia miaka
miwili hadi mitatu na kwamba kosa la nane mshitakiwa atatakiwa kulipa
faini ya Sh milioni 10 au kifungo jela miaka mitano.
Alisema, kwa taratibu zilizopo, baada ya mshitakiwa kukutwa na hatia
anatakiwa kupelekwa Uhamiaji na kurudishwa nchini kwao ili aombe uraia
wa Tanzania upya.
Kabla hukumu hiyo kusomwa, Wakili wa utetezi, Aloyce Komba alidai kuwa
mshitakiwa hakuwahi kuvunja sheria ya kijinai kwani alikuwa mwaminifu
na hakuwahi kutoa siri ya nchi licha ya ukimbizi wake.
Komba pia aliongeza kuwa, tangu mteja wake apate kashfa hiyo,
ameathirika kiuchumi kwa kuwa alitakiwa kustaafu miaka sita ijayo
lakini sasa anakosa mapato yake.
‘’Naomba mahakama isitoe adhabu kubwa kwa mteja wangu kwani pamoja na
ukimbizi wake, kutokana na vita za mara kwa mara zinazotokea nchini
Burundi, mshitakiwa ameanzisha kituo cha kulelea watoto yatima wa
Tanzania na Burundi hivyo amekuwa na msaada,’’alidai Komba.
Akimsomea maelezo ya awali (PH), baada ya kukiri mashtaka yake,
Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Method Kagoma alidai wazazi wa Bitaho
waliingia nchini mwaka 1958 na kisha kurudi tena mwaka 1972 huku yeye
Bitaho akiwa mtoto mdogo.
Aliidai baada ya kukua, mshitakiwa huyo alijiunga na elimu ya msingi,
sekondari na vyuo hapa nchini na kwamba mwaka 2001 aliajiriwa na TBS
kama mwanasheria.
Katika mashitaka yake inadaiwa Mei 19, mwaka huu maeneo ya Ofisi ya
Uhamiaji iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa mkimbizi na Raia
wa Burundi, alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa uhamiaji.
Alidaiwa kuwa alijitambulisha kuwa ni raia wa Tanzania na kuonesha
Kitambulisho cha Taifa chenye jina lake ambacho alikipata kinyume na
sheria huku akijua kwamba anajiongezea kosa.
Kagoma alidai, Oktoba 19, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere wilayani Ilala Dar es Salaam, akiwa mkimbizi na Raia wa
Burundi, alishindwa kutimiza masharti yaliyotolewa Septemba 11, 2013 na
Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ambapo alishindwa kurejesha hati ya kusafiria
aliyoipata isivyohalali.
Imeendelea kudaiwa kuwa, Juni 22, 2011 katika Ofisi za Uhamiaji za Mkoa,
alitoa taarifa za uongo katika fomu ya kuombea hati ya kusafiria CT5
(Ai) yenye namba 05381440 kwa lengo la kupata hati hiyo.
Aidha mshtakiwa Bitaho anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa kutoa kiapo
kuonesha kuwa baba yake ni raia wa Tanzania kitu ambacho sio kweli na
kwamba alitoa barua kutoka Ofisi ya Kata ya Yombo Vituka
iliyomtambulisha kuwa ni Mtanzania kwa lengo la kupata hati ya
kusafiria.
Mshitakiwa Bitaho alitoa pia barua ya kuajiriwa aliyoambatanisha na fomu
ya maombi ya hati ya kusafiria kuonesha ni Mtanzania kitu ambacho
alijua si kweli.
Aidha anadaiwa kujipatia kadi ya kupigia kura kinyume na sheria na
kwamba Mei 19 na pia amejihusisha na kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS
bila kuwa na kibali.
MWANASHERIA MKUU WA TBS AHUKUMIWA JELA MIAKA MITANO
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:44:00
Rating:
No comments: