WATEJA "GESTI" WAANDIKE MAJINA,SEHEMU WANAZOTOKA NA NAMBA ZA VITAMBULISHO VYAO




KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ametoa rai kwa wakazi wa jiji hilo na wageni wanaoingia jijini humo kutoka katika mikoa mbalimbali kupuuza taarifa za sauti zinazosambazwa kwenye mitandao ya jamii kuwa polisi wanawakamata hovyo wanaolala mchana kwenye nyumba za wageni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sirro leo, habari zinazosambazwa katika mitandao ya WhatsApp naTelegram, pamoja na zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti kuwa polisi wanawakamata watu hao kwa madai ya uzururaji na uzembe ni uvumi.

Kamanda Sirro alisema kwa nia ovu, taarifa hizo zimedai kuwa hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la 'Hapa Kazi Tu', jambo ambalo si la kweli.

“Ninawatoa hofu raia wema kuwa tunaendeleza operesheni kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria kwa kuendesha gesti bubu," amesema.

Amesema katika taarifa yake hiyo kuwa uchunguzi umebaini kuwepo na nyumba za kulala wageni zinazoendesha biashara kiholela kwa kuhifadhi wahalifu, wakiwemo wanawake na wanaume wanaouza miili yao (dada na kaka poa).

“Ni wajibu wa polisi kufanya ukaguzi mara kwa mara kwenye nyumba za wageni, hoteli, migahawa, vilabu vya vileo na kumbi za starehe zinazokesha," alisema na kuongeza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Sirro amewataka wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni kufuata taratibu za kupokea wageni kwa kuandika majina yao kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanazotoka na watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kwenye kituo chochote cha Polisi.

Aliwataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa na wajumbe wa Nyumba 10 wawajibike kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na kuwachukulia hatua stahiki wanaobainika kuwa ni wahalifu, ili kuimarisha usalama.

Imeandikwa na Sophia Mwambe-Habarileo
WATEJA "GESTI" WAANDIKE MAJINA,SEHEMU WANAZOTOKA NA NAMBA ZA VITAMBULISHO VYAO WATEJA "GESTI" WAANDIKE MAJINA,SEHEMU WANAZOTOKA NA NAMBA ZA VITAMBULISHO VYAO Reviewed by WANGOFIRA on 21:03:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.