RAIA WA CHINA AFARIKI DUNIA AKIPANDA MLIMA KILIMANJARO


RAIA wa China aliyetambulika kwa jina Zhu Yush (27), amekufa wakati akipanda Mlima Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa, Yush aliyekuwa akitalii nchini, alikufa Septemba 7, mwaka huu saa 7:00 mchana, katika eneo la Jiweni Kabamba katika tarafa ya Kibosho wilayani Moshi.

Mutafungwa alisema, mtalii huyo aliingia nchini Septemba 3, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), uliopo wilayani Hai. Alisema madhumuni ya kuingia nchini ni kupanda mlima huo ambao ni mrefu zaidi barani Afrika.

Alisema raia huyo alikuwa na hati ya kusafiria yenye namba E 43941406 na kwamba uchunguzi wa awali ulionesha kuwa kifo chake kilisababishwa na magonjwa yanayotokana na kubadilika kwa hali ya hewa.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC katika Manispaa ya Moshi, kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku taratibu za kuusafirisha mwili zikiendelea. Mwaka huu watalii wawili wamepoteza maisha kwenye ajali wakati wakifanya utalii.

Kifo cha kwanza kiliripotiwa kutokea mwaka huu, baada ya raia wa Afrika Kusini, Gululeth Zulu (38) kushindwa kupumua akiwa kwenye mwinuko wa juu ya mlima. Kifo hicho kilitokea Julai 18.
RAIA WA CHINA AFARIKI DUNIA AKIPANDA MLIMA KILIMANJARO RAIA WA CHINA AFARIKI DUNIA AKIPANDA MLIMA KILIMANJARO Reviewed by WANGOFIRA on 21:11:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.