WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AWAMU YA NNE ANUNG'UNIKA DHIDI YA KIKWETE NA ANNE MAKINDA. 


ALIYEKUWA Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu ya nne, Ezekiel Maige,

Amedai kuwa kitendo cha Serikali yao chini ya Rais Jakaya Kikwete kufuata kasi ya upepo unakovuma na uonevu wa Spika Anne Makinda dhidi yake ndiyo chanzo cha yeye kuenguliwa uwaziri kwa kashfa ya vitalu vya uwindaji na usafirishaji wa wanyama hai mwaka 2012.

Maige aliyeshika nafasi ya unaibu waziri mwaka 2008 hadi 2010 akiwa na Waziri Shamsa Mwangunga na kisha kuwa waziri kamili kuanzia Novemba 27, 2010 hadi Mei, 2012, alisema hadi wakati akijiuzulu, alisema ushahidi wa anachokisema ni ukweli kuwa hakuna mahala alikopewa nafasi ya kujieleza kuhusiana na tuhuma hizo.

Alisema cha kusikitisha, ni ukweli kwamba hatua za kumuwajibisha zilichukuliwa kutokana na mazingira ya wakati huo ya “kufuata upepo” unakovuma na pia kunyimwa kwake fursa ya kujieleza bungeni na aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Makinda.

Alisema kutokana na yote hayo, ndipo alipojikuta akipoteza uwaziri na hadi sasa amebaki na siri nzito moyoni kuhusiana na mambo hayo na pia vitendo vya ujangili.

Maige aliondolewa uwaziri na Rais Kikwete baada ya taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kumtuhumu kuwa alihusika katika kugawa vitalu vya uwindaji kwa kampuni hewa 16. Aliponzwa pia na uuzaji wa wanyama hai wakiwamo twiga.

"Bahati mbaya, sisi tuliosimamia sheria tuliondolewa kwa hila. Na bahati mbaya, kwa mazingira ya wakati ule, upepo ukivuma sana unakwenda hivyo hivyo… Ila hivi sasa (chini ya Rais John Magufuli) mambo yamebadilika… kuna usimamizi wa sheria," alisema Maige.

MAKINDA ALIVYOMPONZA
Akielezea kile kilichotokea kabla ya kuachia uwaziri, Maige alisema Makinda alishiriki kwa kiasi kikubwa katika kuondolewa kwake uwaziri kutokana na kile anachodai kuwa spika huyo mstaafu alimkandamiza kwa kutompa muda wa kujitetea bungeni baada ya tuhuma kadhaa kuelekezwa kwake kuhusiana na ugawaji wa vitalu vya uwindaji.

Alisema kabla ya kuondolewa, aliomba apewe fursa ya kuelezea ukweli wa suala hilo, lakini kwa bahati mbaya mazingira kuhusiana na jambo hilo yalijaa harufu ya rushwa na hujuma zilienea dhidi yake hadi bungeni ambako mwishowe hakupata nafasi hata ya kusikilizwa.

"Nilisema bungeni kwamba jambo lolote linalowasilishwa bungeni ni lazima liwe limepitia kwenye kamati. Na huko kwenye kamati ni lazima majadiliano yawe yamekamilika… nilisema yote yaliyojadiliwa bungeni sikuwahi kuitwa na kamati kujibu tuhuma zinazoelekezwa,"alisema Maige na kuongeza:

"Bungeni nikasema, Mheshimiwa Spika, utaratibu hauruhusu hili jambo kujadiliwa maana sijaitwa kwenye kamati… lakini Spika kwa sababu alikuwa na vionjo vyake, ana malengo yake, alisema kamati inaruhusiwa kufanya kazi kama inavyopenda, wewe changia kama mchangiaji.”

Maige aliongeza kuwa baada ya hapo, alifanya jitihada za kuzungumza na mawaziri wenzake, hasa aliyekuwa akishughulikia Sera, Uratibu na Bunge ili asaidiwe kupata nafasi ya kutosha ya kujieleza bungeni lakini jitihada zake hizo pia hazikufanikiwa.

"Nikasema tena na mawaziri wenzangu, nikimzungumzia Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, nikamwambia usimame usaidie hili suala maana mimi hapa sizungumzi kama Maige, ninazungumza kama Waziri wa Serikali… naomba uliombe Bunge lisitishe mjadala ili nikaandae majibu kama Waziri. Nilipewa dakika 10 za kuchangia kama mchangiaji wa kawaida," alisema.

"Sijaona Waziri, tena mlengwawa tuhuma, anachangia kwa dakika kumi. Zimekuja skendo za ajabu ajabu kama Escrow, Waziri husika amepewa zaidi ya saa moja na dakika 20, anaeleza msimamo wa Serikali. Lakini mimi nilipewa dakika kumi, nilijaribu kueleza (lakini) muda sikupata,"alisema.

Akieleza zaidi, Maige alisema kuwa jitihada zake za kutaka kuelezea upande wake kuhusiana na tuhuma dhidi yake ziliendelea kugonga mwamba hata pale alipozungumza na waandishi wa habari nje ya Bunge.

"Kwenye kamati sikupata muda, bungeni sikupata muda, niliyozungumza nje ya bunge, waandishi nao wakaingia kwenye mkumbo kuwa ninalilia uwaziri, kwani alizaliwa kuwa Waziri...matokeo yake nimebaki na siri nzito juu ya yote ambayo ninayajua kuhusu yaliyosemwa dhidi yangu,"alisema.

Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala kuanzia mwaka 2005, alisema tuhuma zilizoelekezwa kwake ni pamoja na zile zilizohusiana na utoroshaji wa twiga.

Alipotakiwa afichue siri hiyo nzito aliyo nayo kuhusiana na utoroshaji wa twiga na kuwapo kwa vitendo vya ujangili nchini, Maige alisema hawezi kufanya hivyo sasa na ataendelea kubaki kimya.

"Ningeweza kusema, lakini sikupewa nafasi ya kuzungumza. Kwa maana hiyo nitaendelea kubaki kimya. Nitaendelea kunyamaza maadamu muda wa kusema haukuwapo na sijawahi kupewa… namshukuru Mungu, namwachia yeye (Mungu), nabaki na siri yangu," alisema.

AJUAVYO KUHUSU VITALU

Katika mahojiano hayo, Maige alizungumzia pia tuhuma kwamba aligawa vibaya vitalu vya uwindaji kwa kuzipendelea kampuni hewa.

Alisema kama Spika angempa nafasi wakati huo, jambo hilo pia angelieleza kwa kina. Hata hivyo, anashukuru kuwa hadi sasa ukweli ungali ukijidhihirisha kwa kuwa walipita mawaziri wawili wa Maliasili na Utalii kabla serikali ya awamu ya nne haijamaliza muda wake na hakuna hata mmoja aliyekutana na kampuni hewa na kuzitaja kwa nia ya kutekeleza agizo la kamati.

"Wakati ule upepo ukivuma sana unakwenda hivyo hivyo,” alisema Maige, akikumbushia kuenguliwa kwake nafasi ya uwaziri baada ya shinikizo kali bungeni.

Akieleza zaidi, Maige alisema akiwa Naibu Waziri mwaka 2009, walitengeneza sheria ya wanyamapori namba tano ya 2009, anayoamini kuwa ina mambo mazuri.

Alitaja baadhi ya yale yaliyoelezwa na sheria hiyo kuwa ni kutoa nafasi za upendeleo kwa Watanzania, jambo ambalo anafurahi kuona kuwa hivi sasa linasisitizwa pia na Serikali ya awamu ya tano, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanawezeshwa kumiliki uchumi wao.

"Ukifuatilia, utabaini kuwa wakati huo kelele zilikuwa nyingi kwenye ugawaji wa vitalu vya uwindaji na sababu kubwa ni makampuni makubwa ya kibepari yaliyomiliki vitalu kwa miaka mingi hayakupata. Yalipokosa, yakaanza kulalamika kuwa Maige amekosea, amependelea na wengine wakalidanganya Bunge," alisema.

"Hadi leo nimebaki najiuliza… kwenye sekeseke langu, hoja ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni kwamba Maige amegawa vitalu kwa kampuni hewa 16 na zinyang'anywe na awajibishwe," alisema na kuongeza:

"Leo nawapa changamoto… Maige ameondoka, Balozi Khamis Kagasheki alipewa kazi… waulizwe mawaziri waliokuja baada yangu, walikuta kampuni ngapi hewa na kuzinyang'anya vitalu? Kwa kifupi, hakuna kampuni hata moja ambayo ilithibitika haikuwa na sifa, haikushiriki kwenye tangazo, haikukaguliwa na kamati na haikupewa marks (alama) za kustahili kugawiwa kitalu.

Utaratibu tuliokuwa tumeweka kwenye kanuni kila muombaji ni lazima akaguliwe, apate marks hadi 100 na itakayopata chini ya 50 imefeli."

Kwa mujibu wa Maige, pamoja na maneno yote, uongozi wake ulitumia nguvu kubwa kuwapa kipaumbele Watanzania kwakuwa mwaka 2005/2006, kati ya kampuni 46, nne ndiyo zilikuwa za Kitanzania na walivyogawa mwaka 2011, katika kampuni 60 zilizopata, 51 zilikuwa ni za Kitanzania.

"Matokeo yake waliokosa ndiyo waliendelea kupiga kelele. Baadhi wakaja bungeni, wakatoa rushwa kwa wabunge, wakafanya semina kwenye ukumbi mmoja hapa Dodoma.

Niliwahi kusema bungeni kwamba waliweka wakala wa kuchangishana fedha, wakaweka mshawishi aje kuwahonga wabunge ili wapige kelele wazungu warudishiwe vitalu, Aprili 16, mwaka 2012, saa 7:00 mchana… na kweli wakapinga na Waziri akaondolewa,"

Maige alisema: " lengo lao halikuwa Waziri kuondolewa bali warudishiwe vitalu. Ameondoka Maige, akaja Kagasheki ameondoka, akaja (Lazaro) Nyalandu akaondoka, sasa kaja rafiki yangu Profesa (Jumanne) Maghembe, waulize mawaziri wote watatu … kwa nini hawajazinyang'anya vitalu hizo kampuni hewa za mfukoni? "

Maige alisisitiza kuwa umma ulipotoshwa na wengine wakashiriki katika dhambi ya kushabikia na kwamba, mizozo inayoikabili sekta ya uwindaji inaendelea kuizorotesha.

"Wakati naondoka serikalini, Idara ya Wanyamapori hasa eneo la uwindaji, tulikusanya zaidi ya Sh. bilioni 30 … leo makusanyo siyo zaidi ya Sh. bilioni 15, na itaendelea kushuka. Wakati ukusanyaji unateremka kiwango cha ujangili kinaongezeka, utakabilianaje na ujangili wakati huohuo rasilimali fedha inazidi kushuka?”

UJANGILI

Akizungumzia ujangili, Maige alisema pamoja na yote yaliyosemwa, yeye hakuwahi kuwa na kashfa yoyote kuhusiana na mambo hayo.

"Katika kipindi nilichokuwa Waziri hakukuwa na kashfa ya kukamatwa kwa meno ya tembo yaliyotoka nchini. Pamoja na kuongezeka kwa rekodi ya ujangili, kwa miaka miwili tuliudhibiti,"

Maige alisema siri iliyowapa mafanikio ni kuwa karibu na watumishi wa ngazi ya chini na kwamba hata leo, askari wanyamapori wa pori la Kigosi Moyowosi, askari wanyamapori wa Uwanda Game Reserve, walishirikishwa kwa kuelezwa kinachoendelea serikalini hasa ukosefu wa fedha na kuwashirikisha namna gani wanaweza kuendelea na kazi.

"Wengi walituelewa walishirikiana na wadau wengine ambao walikuwa wanaisaidia serikali na tulifanikiwa kudhibiti ujangili,"alisema.

NINI CHA KUFANYA?
Maige alisema kadri aonavyo, msimamo wa Waziri Maghembe hivi sasa ni mzuri kwa kuwa anasimamia sheria na anapaswa kuungwa mkono na kila mmoja kwa sababu hapo kabla,
vitendo vya uvunjifu wa sheria vilivyopigiwa kelele bado viliendelea.

MISITU

Maige alisema baadhi ya mafanikio wakati wa uwaziri wake kabla ya kuondolewa ni pamoja na kubadili sheria za kiusimamizi na kiutendaji na ukusanyaji wa mapato kwenye sekta zote.

"Wapo wengi wanajitahidi kusahau au kujifanya hawaoni, lakini tumefanya kazi. Sekta ya misitu ikiwa idara, ilikuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi zake kwa sababu uvunaji wa miti uliokuwapo haukuwa na udhibiti na ulifika hadi kwenye mashamba ya miti ya serikali, hakukuwa na upandaji,"alisema.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, chini ya uongozi wake, walianzisha tozo maalumu ya kutunza mashamba inayolipwa na wavunaji wa misitu, magogo kwa ajili ya kusaidia shughuli za ufyekaji wa shamba, upandaji miti, palizi na kuzima moto pindi unapotokea.

Alisema kuwa walianzisha mchakato wa kufanya idara ya misitu iwe ni Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), lengo likiwa ni kuisaidia idara hiyo ipate uhuru wa kukusanya mapato, kuajiri watumishi kama taasisi kulingana na bajeti na maamuzi ya bodi zao, na pia kuanzisha mfuko maalumu wa kusaidia juhudi za upandaji miti kwenye jamii (Tanzania Forest Fund).

"Matunda yake yanaonekana na bado kwenye sekta ya misitu kuna kazi kubwa ya kufanya. Tulifikiri kushirikisha sekta binafsi katika upandaji miti kwani yapo maeneo ya hifadhi ya misitu lakini ni nyika ,miti imekwisha. Mfano Ruvu North na Ruvu South yenye zaidi ya hekta 20,000, sasa yamebaki nyika tu,"alisem na kuongeza:

"Tulifikiria kushirikisha sekta binafsi ili wapande miti, wanauza halafu Serikali inapata mrabaha kwenye ardhi yake kwa miaka 30 au 40 kuliko kuwa na eneo la hifadhi ambalo halina misitu. Hilo ni eneo muhimu la kuangaliwa."

CHANGAMOTO ZILIZOPO

Waziri huyo wa zamani alisema kuna migogoro ya mipaka ya hifadhi na mannufaa ya wananchi walioko jirani na hifadhi. Kwa sababu hiyo, ipo haja ya kutazama upya sheria ili kuongeza nafasi ya wananchi walio jirani kunufaika na hifadhi.

Alisema sheria ya wanyamapori imeeleza kuwa baada ya sheria kupita, Waziri mwenye dhamana ya wanyamapori atapitia upya mipaka yote ya hifadhi ili kuangalia yaliyovamiwa kiasi kisichohimilika yafutwe.

"Tuna game control area 43. Ila kiuhalisia maeneo hayo hayapo, yamebaki jina. Mfano Wilaya ya Monduli, Simanjiro, asilimia 60 ya Kasulu na Longido ni 'game control area'… sheria mpya ya wanyamapori ya 2009 inazuia watu kuingia, hivyo ni muhimu Waziri aangalie na kufuta lakini hakuna lililofutwa kwa sababu hajapata muda wa kufuatilia,"alisema na kuongeza:

"Wakati wangu tulianza kwa kuunda tume chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Chuo cha wanyamapori cha Pasiansi. Walitengeneza ripoti ila hadi sasa sijui kilichotokea. Nadhani hii ingekuwa suluhisho zuri la kupunguza migogoro kati ya wananchi na wahifadhi,"alisema.

UTALII
Kwa mujibu wa Maige, kiwango cha utalii nchini ni kidogo kulinganisha na nchi washindani wenye vivutio kama vya Tanzania wakiwamo Kenya na Afrika Kusini.

Akitolea mfano, alisema bajeti ya mwaka huu ya Kenya ni zaidi ya mara 10 ya Tanzania na kwamba kwa mwaka huu, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imetengewa Sh. bilioni 5 huku wao wakitenga dola za Marekani milioni 30 (Sh. bilioni 60).

"Katika mazingira haya, sisi tuna bilioni 5, ukijumlisha na kinachotengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Ngorongoro ndiyo inafikia Sh. bilioni 10. Kuna changamoto za kuzishughulikia ili kuvutia watalii zaidi ili kushindana na wenzetu, Afrika Kusini bajeti yao ni bilioni 120 na wanapata watalii wengi zaidi,"alisema.

TAHADHARI UANZISHWAJI VAT
Alisema kwa kipindi hiki chenye ushindani mkubwa kibiashara na vivutio vikiwa havijaendelezwa, ni vyema vivutio vya nje ya hifadhi vikaangaliwa licha vivutio vya kijiografia na wanyama, hadhani kwamba haikuwa muda muafaka kuongeza tozo ya ongezeko la thamani (VAT), kwenye huduma za utalii zitaongeza gharama na kufanya utalii wa Tanzania kuwa mghali.

"Hatuna uwezo wa kushindana na Kenya maana hatuna huduma nyingi. Gharama zitakuwa kubwa, hatuna ndege nyingi zinazoleta wageni wa kimataifa. 


Kuna hatari ya kukuta wageni wanatoka duniani wanakuja Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta na kuingia kwenye magari wanafanya utalii Masai Mara na kuingia Serengeti. Kama alipanga kukaa siku kumi atatumia saba Kenya na tatu Tanzania,"alisema.

Aidha, alishauri TTB kupewa nguvu kisheria katika kukusanya tozo kama ilivyo kwa mamlaka nyingine za usimamizi ili waibue vivutio vipya na kutangaza vivutio zaidi kama kimondo cha Mbozi.

TUHUMA JUMBA LA KIFAHARI
Wakati akipoteza uwaziri mwaka 2012, miongoni mwa mambo yaliyoibuka na kuzua gumzo ni madai kwamba Maige amejenga nyumba kubwa ya kifahari iliyotajwa kuwa na thamani ya dola za Marekani 700,000, na kwamba fedha alizotumia kukamilisha mradi huo ni dalili kwamba yeye siyo msafi.

Akizungumzia suala hilo, Maige alisema kuwa taarifa hizo wakati huo ni muendelezo wa kile alichodai kuwa ni jitihada za ‘wabaya’ wake kumzulia mambo kwa sababu ukweli wa nyumba hiyo ni kwamba, thamani yake ni dola za Marekani 410,000 na siyo 700,000.

"Ile nyumba mpaka sasa hivi siyo yangu… ni ya Benki ya CRDB. Ukienda kwa Msajili wa Hati huwezi kukuta jina langu. Kimsingi, toka nizaliwe sijawahi kushika fedha hizo. 


Nilichokifanya ni kutumia mkopo wa ubunge kumlipa muuzaji dola za Marekani 200,000, zilizobaki zikalipwa na benki, kutoka benki kwenda kwa muuzaji. Na sasa nalipa kila mwezi zaidi ya Sh. milioni 4.5," alifafanua na kuongeza: 

"Mpaka nitakapomaliza deni hilo ambalo ni miaka 12 ndipo nyumba itakuwa yangu. Hata leo nikitaka mkopo siwezi kutumia nyumba kuweka dhamana maana hati sina. 

Vyombo vya uchunguzi haviwezi kumuacha mtu amepiga (ameiba) waziwazi na kihuni hivyo… na kumuacha. Hilo suala lilitumika pia kama sehemu ya kuniondoa, " alisema Maige.NIPASHE
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AWAMU YA NNE ANUNG'UNIKA DHIDI YA KIKWETE NA ANNE MAKINDA. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AWAMU YA NNE ANUNG'UNIKA DHIDI YA KIKWETE NA ANNE MAKINDA. Reviewed by Unknown on 20:35:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.