Maduka, Magari yazuiwa kwa kutohudumia wanaCCM


Pemba. Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid amefunga maduka matatu ya rejareja na kusimamisha magari ya abiria kati ya Wete na Mtambwe kwa madai ya kutoa huduma kwa misingi ya ubaguzi wa kisiasa.

Pemba
Wafanyabiashara waliofungiwa ni Said Juma Seif, Titi Juma Othman wa Mtambwe na Hamad Haji wa Mchangamdogo.

Alisema wafanyabiashara hao wamelalamikiwa na wafuasi wa CCM, wakiwatuhumu kukataa kuwahudumia kutokana na itikadi zao za vyama. Rashid alisema baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kuwa wafanyabiashara hao wanawabagua wanaCCM.

“Tumelazimika kuyafungia maduka hayo matatu baada ya Serikali ya Wilaya kujiridhisha kwamba yanawabagua wanachama wa CCM,” alisema.

Akizungumzia hatua hiyo, Haji aliitaka Serikali kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kuchukua hatua akisema hahusiki na masuala ya kisiasa. Alisema hizo ni chokochoko za wabaya wake.

Usafiri wasitishwa Mkuu huyo wa wilaya, aliagiza kuzuiwa kwa magari yote ya kubeba abiria kwenye Barabara ya Wete – Mtambwe kwa madai hayohayo ya kuwabagua wanaCCM.

Alisema mbali ya hatua hiyo, atawasiliana na wizara husika ili kuchukua hatua kwa wahusika kwa kukiuka leseni. Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama zuio hilo alilosema ni la muda usiojulikana litayahusu magari ya Ruti B ambayo leo ndiyo yaliyotarajiwa kutoa huduma kwani yaliyozuiwa jana kwenda Mtambwe, nyumbani kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif ni ya Ruti A.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wete, Mmanga Juma Ali alisema katika utekelezaji wa agizo hilo hakutakuwa na huruma: “…Hatutaishia hapo wanaofanya ubaguzi huo watafikishwa mahakamani.”

Hata hivyo, baadhi wa wahuduma wa vyombo vya usafiri walisema si wao wanaowashusha, bali ni wananchi na kwamba dereva na konda hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa lengo lao ni kutafuta faida.

Maalim Seif atema cheche Wakati uongozi wa Wete ukichukua hatua hiyo, Maalim Seif ameendelea na ziara yake visiwani hapa aliwataka Wazanzibari kuonyesha kuwa wanaikataa Serikali ya Dk Ali Mohamed Shein.

Akizungumza na watendaji na viongozi wa CUF wa Wilaya ya Micheweni, Kaskazini Pemba, Maalim Seif aliwataka kutomtegemea yeye pekee kufanya hivyo.

“Tukikazana, Serikali hii itaondoka, ikiwa mnangoja Maalim Seif au Marekani kuiondoa, kwa sheria ya kimataifa haitawezekana kwani Marekani haiwezi kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar,” alisema Makamu huyo za zamani wa Rais wa Zanzibar, alijitoa kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 ambao Dk Shein aliibuka kidedea.

Uchaguzi huo ulikuwa wa marudio baada ya ule wa Oktoba 25 kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha siku ambayo alikuwa atangaze matokeo yote. Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali.

“CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka… tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema.

Aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mfano tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.

CUF yajipanga kwenda ICC Alisema kuna mwanasheria mzalendo ambaye ameanza kukusanya vielelezo mbalimbali kabla ya kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC dhidi ya viongozi wenye dhamana ya kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama wa raia.

Alisema tayari Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, wamepewa notisi ya kuarifiwa kufunguliwa mashtaka ICC kutokana na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu uliofanyika Zanzibar.

CCM yamjibu Akizungumzia kauli za Maalim Seif, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema chama chake hakina muda wa kujibizana na CUF baada ya kumalizika kwa uchaguzi na kwamba watakutana tena majukwaani na chama hicho kwenye uchaguzi wa 2020.

Baraza la wawakilishi kesho Wakati hayo yakiendelea Baraza la Wawakilishi linatarajiwa kuanza kesho Chukwani, nje kidogo ya mji wa Unguja. Macho na masikio ya wananchi yataelekezwa katika Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi ambao unaweza kutegua kitendawili cha rasilimali hiyo kubaki ndani au nje ya Muungano.

Katibu mpya wa Baraza hilo, Raya Issa Msellem alisema muswada huo utasomwa kwa mara ya kwanza na wajumbe watapata nafasi ya kuuchangia.

Chanzo: Mwananchi
Maduka, Magari yazuiwa kwa kutohudumia wanaCCM Maduka, Magari yazuiwa kwa kutohudumia wanaCCM Reviewed by WANGOFIRA on 08:44:00 Rating: 5
Powered by Blogger.