Mtanzania akamatwa na kilo 74 za ‘unga’ India



Kamishna wa Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa. Picha na Maktaba 

Dar es Salaam. Maofisa uhamiaji wa Uwanja wa Ndege wa Mumbai, India wamemkamata Mtanzania, Fatma Chambo Basil akiwa na kilo 74 za dawa za kulevya aina ya methaqualone alizokuwa akizisafirisha kuleta nchini.
Kwa mujibu wa tovuti ya Gazeti la Indian Post, kiasi hicho cha dawa za kulevya ni kikubwa kuliko vyote vilivyowahi kukamatwa katika uwanja huo wa ndege.
Kamishna wa Uhamiaji wa Mumbai, Milind Lanjewar alisema Chambo alikamatwa jana kwa kukiuka Sheria ya Kuzuia Usafirishwaji wa Dawa za Kulevya ya India.
Kamishna Lanjewar alisema Chambo alikamatwa akiwa anaelekea Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya shirika la Qatar.
“Alikamatwa baada ya upekuzi na uchunguzi wa kina kwenye mizigo yake, uchunguzi huo ulisaidia kugundua dawa hizo aina ya methaqualone,” Lanjewar alisema.
Akizungumzia kukamatwa kwa Chambo, Kamishna wa Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa alisema hana taarifa kuhusu tukio hilo lakini akaahidi kufuatilia jinsi alivyoondoka nchini na kupeleleza taarifa zake zote ikiwamo anakoishi, hati yake ya kusafiria na nyendo zake.
“Huo ni mzigo mkubwa, ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya. Sisi huwa tunawaonya kila siku kuhusu kubeba dawa za kulevya na sasa wanakamatwa nchi nyingine,” alisema.
Kadhalika, Nzowa alisema imezuka tabia kwa Watanzania kuvuka na kwenda India kununua dawa za kulevya aina ya ephedrine na methaqualone na kisha kuzileta nchini kabla ya kuzipeleka Afrika Kusini.
Alisema dawa hizo zinalimwa na kuzalishwa India kwa ajili ya matumizi ya tiba lakini watu wamekuwa wakizitumia vibaya kama dawa za kulevya.
Akizungumzia hali ya dawa za kulevya nchini, Nzowa alisema juhudi zinafanywa na kitengo chake kuhakikisha nguli wa biashara hiyo wanakamatwa ili kuumaliza kabisa mtandao huo.
Mtanzania akamatwa na kilo 74 za ‘unga’ India Mtanzania akamatwa na kilo 74 za ‘unga’ India Reviewed by WANGOFIRA on 05:02:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.