Jumba la Maajabu linavyovutia utalii Zanzibar

ZANZIBAR kuna vivutio vingi vya utalii lakini Jumba la Maajabu linaongoza kwa kuvutia watalii wengi kutokana na muundo wake. Jumba la Maajabu maarufu kama Beit-al- Ajaib kwa lugha ya Kiarabu ni miongoni mwa vitu vya kipekee vinavyopatikana katika visiwa vya Zanzibar. Jumba hilo limehifadhi kumbukumbu na kihistoria ndefu kuhusu ubunifu na maendeleo ya Zanzibar.
Jumba hilo lililojengwa miaka ya 1880 lipo barabara ya Mizingani karibu na ufukwe wa bahari ya Hindi na linaonekana kwa urahisi unapoingia Zanzibar kwa njia ya bahari. Jumba hilo lenye zaidi ya miaka 125 ni sehemu ya kivutio muhimu kwa watalii wanaofika Zanzibar kila siku kwa ajili ya kujifunza tamaduni, mambo ya kale na hatua za maendeleo katika jamii ya Waafrika. Zipo sababu nyingi zilizolifanya jumba kuwa la maajabu.
Mosi lina nguzo 40 zilizojengwa kwa ustadi mkubwa. Wajenzi wa jumba liho walitumia mchanganyiko wa utaalamu kutoka mataifa mbalimbali ingawa lilisimamiwa na utawala wa Sultan wa Kiarabu. Jumba hilo limepata umaarufu mkubwa kwa kuwa lilikuwa jengo la kwanza Afrika Mashariki na kusini mwa jangwa la Sahara kutumia umeme. Wakati huo watu walikuwa wakitumia kandili, vibatari na mishumaa kwa ajili ya kupata mwanga nyakati za usiku.
Pia wapo ambao walikoka moto mkubwa ili kupata mwanga ili kukamilisha shughuli zao kabla ya kulala. Lakini jumba hilo lilikuwa likiwaka taa ambazo zilibandikwa ukutani na nyingine zilining’inia kwa kutumia uzi mrefu uliotungukwa kwenye dari. Kwa kuwa mwanga wa taa hizo ulionekana kwa mbali ulisababisha watu wengi kupigwa na butwaa.
Taarifa za kuwepo kwa jumba lenye taa za ajabu zilisambaa katika ukanda wote wa Afrika Mashariki hivyo watu kutoka Kenya, Uganda na Tanzania hasa wavuvi walisafiri hadi Zanzibar kushuhudia maajabu ya jumba hilo. Jumba hilo la ghorofa lilikuwa ndio jengo la kwanza kuwa na lifti katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Tofauti na majengo mengine ambayo ilikuwa ni lazima kupanda ngazi ili ufike ghorofani wageni waliofika kwenye jengo hilo hawakupanda ngazi. Walikuwa wakiingia kwenye chumba kidogo kisha kubonyeza kitufe kinachotumia umeme kisha machine fulani humpandisha hadi ghorofa za juu. Mashine ikifika inasimama na mlango unapofunguka mgeni hujikuta kwenye ghorofa ya juu au chini.
Jambo hilo liliwafanya wageni na wenyeji kuwa na shauku kubwa ya kuingia kwenye jumba hilo kwa nia ya kujionea maajabu ya teknolojia ya kisasa ambapo mtu aliweza kujikuta akiwa ghorofani pasipo kusogeza mguu wake hata hatua moja.
Habari za kuwepo kwa lifti katika jengo hilo zilizua gumzo na maswali mengi miongoni mwa watu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Wavuvi na wasafiri hasa wafanyabiashara waliofika Zanzibar walikwenda kwenye jumba hilo kwa lengo la kuingia ndani ili waweze kushuhudia maajabu wanayoyasikia. Hata hivyo sio kila mtu aliruhusiwa kuingia kwenye jumba hilo kwa kuwa lilikuwa na hadhi kubwa pengine kuliko hata Ikulu. Waafrika wachache hasa viongozi na watumishi ndio walipata fursa ya kuingia ndani na walipotoka walisimulia maajabu waliyoona.
Mfumo wa maji taka na maji safi ya bomba ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha jumba hilo kuendelea kuonekana la maajabu. Wakati majengo mengine ya kifahari katika ukanda wa Afrika Mashariki yalikuwa na vyombo mbalimbali vya kuhifadhia maji, Jumba la maajabu lilikuwa la kwanza kuwa na bomba zinazotiririsha maji ndani ya nyumba. Hata wataalamu waliofika katika jengo hilo walishangazwa na ubora na uzuri wa jengo hilo lililojengwa kwa mtindo wa kipekee.
Kwa mujibu wa historia ya Zanzibar, ubunifu wa jumba hilo ulifanywa na askari wa meli toka Scottland na lilijengwa na sultan Barghash bin Said katika mwaka wa 1883, kwa ajili ya ofisi yake. Hata hivyo matumizi ya jumba hilo yalikuwa yakibadilika kadiri miaka ilivyokuwa ikienda na jinsi tawala zilivyokuwa zikibadilika visiwani humo. Kati ya mwaka 1870 na 1888 jumba hilo lilitumika kwa ajili ya sherehe za kitaifa chini ya utawala wa kisultani.
Mwaka 1913 utawala wa kikoloni wa Waingereza ulibadilisha matumizi ya jumba hilo na kulifanya ofisi za Serikali za mitaa. Inaaminika kuwa hadi sasa hakuna jengo lolote la ofisi ya serikali za mitaa Tanzania bara na visiwani ambalo linakaribia kuwa na hadhi ya jumba hilo la maajabu Jumba hilo ni moja ya hazina ya historia iliyouwezesha Mji Mkongwe kuwa katika orodha ya urithi wa Dunia uliyohifadhiwa na Shirika la Kimataifa ya Maendeleo ya Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).
Pia jengo hilo limehifadhi kumbukumbu ya vita vilivyodumu kwa muda mfupi katika historia ya vita duniani. Vita hivi vilitokea Agosti mwaka 1896 na inadaiwa kuwa vilidumu kwa takribani dakika 45 tu hivyo kuifanya Zanzibar kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na vita ya muda mfupi kuliko vita nyingine zote. Kwa mujibu wa historia, vita hiyo ilitokea mara baada ya kifo cha ghafla cha Sultani Sayyid Hamid Thuwain bin Said ambaye alifariki tarehe Agosti 25, 1896.
Baada ya kifo hicho kijana machachari katika ukoo wa kifalme, Khalid bin Barghash (29) alijaribu kujitangaza mfalme kwa lengo la mrithi kiti cha Sultani Sultani Sayyid Hamid . Ingawa kijana huyo alikuwa kipenzi cha wenyeji wa Zanzibar hakuwa chagua la Waingereza ambao ndio waliyokuwa na jukumu la kulinda usalama wa Zanzibar kutokana na urafiki wa muda mrefu kati ya utawala wa Uingereza na utawala wa Kisultan ambao ulianzia Oman.
Inadaiwa kuwa urafiki huo ulianza pale Ufaransa ilipotoa tishio la kuiteka Muscat ambapo Seyyid Sultan bin Ahmed alianzisha urafiki na Waingereza kwa ajili ya ulinzi. Ili kupata ulinzi huo Waingereza walimtaka Seyyid Sultan bin Ahmed kutiliana saini mkataba wa kuiruhusu Uingerza kufanya biashara na kupitisha misafara ya meli zake katika eneo la Ghuba. Mkataba ulisainiwa katika mwaka 1798 na kutumika katika maeneo yote ambayo yalitawaliwa na Sultani Zanzibar ikiwamo.
Uingereza iliutumia urafiki huo ili kumshurutisha Seyyid Sultan bin Ahmed kuifunga biashara ya utumwa Zanzibar. Kuanzia wakati huo Waingereza waliweka ulinzi katika ardhi ya Zanzibar kwa kuzingatia utafiki wa muda mrefu kati ya Waingereza na Sultan wa Zanzibar. Hivyo Uingereza ilitumia uzoefu wake kuingilia mambo ya ndani ya familia ya Kisultani baada ya kifo cha Sultani Sayyid Hamid na walimlazimisha Khalid Bin Barghashi kuachia madaraka mara moja ili waweze kumsimika Hamoud bin Mohamed.
Waingereza walimpendelea Hamoud bin Mohamed na wakataka atawale kwa kuwa mpwa wa aliyekuwa Sultan wa Oman na mtu mwenye kupendelea zaidi maisha ya kisasa. Waingereza waliona wazi kuwa ilikuwa rahisi kwao kufanya kazi na Hamoud kuliko Khalid ambaye alikuwa na akili ya pekee ya kujitegemea na kuwainua watu wake kuliko kupendekeza wageni. Hata hivyo Khalid Bin Barghashi hakutishika na onyo la Waingereza la kumtaka aachie madaraka kwa sababu alikuwa jasiri na aliona ana kila sababu ya kurithi kiti cha Sultan.
Wazanzibar waliona wazi kuwa Uingereza ilingiliwa uamuzi wa Khalid kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Ziliona mgogoro huo kama uvamizi dhidi ya utu wao na haki zao za kimila kwa kuwa Khalid pia alikuwa mjukuu wa muasisi ya nchi, Sultani Sayyid Said. Khalid aliungwa mkono na watu wengi na aliweza kuaminiwa na jeshi kubwa kisiwani. Hivyo baada ya kujitangaza kuwa sultan alihakikisha anatwaa ngome zote muhimu.
Kabla ya saa 10 jioni siku hiyo ya Jumanne alitimiza majaribio ya mwisho ya kurithi madaraka, alichukua Kasri/Ngome na kudhibiti bandari, Kikosi cha majahazi na sehemu kubwa ya mji mkuu.
Waingereza walikasirika. Walianza kujiandaa kwa ajili ya vita. Tayari kulikuwa na meli mbili za kivita za Kifalme zimetia nanga katika bandari wakati Sultan alipofariki. Serikali ya Uingereza ilimuagiza Mkuu wa Jeshi katika Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar haraka iwezekanavyo akiwa na meli ya bendera na meli mbili za kivita. Amri hiyo iliendelea hadi jioni ya Agosti tarehe 25, Jeshi la Kizanzibari lilipewa saa 40 za kutafakari hatima yao na kuchagua moja ama kupigana au kukimbia.
Hata hivyo walionesha msimamo wao na kuendelea kumlinda kiongozi wao mpya. Kesho yake Agosti 26 1896 majeshi ya Waingereza yalikuwa yamejiweka tayari kwa kuanza vita, yaliagiza meli na silaha nyingi za kivita kutoka Uingereza. Hata hivyo majeshi ya Zanzibar hayakutishika kwa kuwa Sultan wa zamani alikuwa na walinzi wa kasri ambao walikuwa wamejiimarisha kwa kiasi kikubwa na kujirundikia silaha kwa kipindi cha miaka michache ya utawala wake.
Jeshi hilo lililokuwa na vikosi takribani 1000 lilijumuisha Wazanzibari, Waarabu na wanamgambo wa Uajemi. Pia Khalid alikuwa na wasaidizi wapatao 300. Pia wanajeshi wengine zaidi ya 1500 walijitokeza kwa ajili ya kumuunga mkono Sultan mpya hivyo kulifanya jeshi la Khalid kuwa na jumla ya vikosi 2,800 ambavyo vilijipanga kulinda kasri na majengo mengine ya utawala wa Kifalme.
Uingereza ilitoa waraka wa maandishi wa mwisho kwa kumueleza Sultan Khalid kwamba lazima aichie Ngome na atawanyike na majeshi yake la sivyo Uingereza ingeshambulia ngome yake kwa kuwa kitendo cha kujitangaza Sultani bila kupata ushauri wa Uingereza kilikuwa sawa na uasi dhidi ya serikali tukufu ya Malkia wa Uingereza. Alijibu asingeweza kuicha “nyumba yake na nyumba ya baba yake” hivyo alikuwa tayari kwa lolote. Aliwasiliana na serikali za Ufaransa, Marekani na Ujerumani kutafuta kuungwa mkono lakini nchi hizo zilikataa.
Nchi hizo zilikuwa na mkataba na Uingereza kwamba kwa njia moja au nyingine kutojihusisha na mgogoro wa nchi nyingine ndani makoloni yao. Ingawa jitihada za kutafuta suluhu kwa njia ya kidiplomasia hazikuzaa matunda, …Khalid hakukata tamaa hivyo aliamuru meli pekee ya kivita maarufu kwa jina la H.H.S. Glasgow iingie vitani. Ingawa meli hiyo ilikuwa imezungukwa na meli tano kubwa za kivita kutoka Uingereza na zenye vifaa vya kisasa askari wa meli ya sultani hawakuogopa badala yake walifyatua mizinga yao ya zamani na wakazilenga meli mbili za Uingereza zilizokuwa karibu.
Waingereza waliona kitendo hicho ni cha ukaidi hivyo kilianza mashambulizi dhidi ya vikosi vya Sultani. Vikosi hivyo havikuchelea kujibu mapigo. Hata hivyo vilisambaratishwa baada ya dakika chache na meli ya meli H.H.S. Glasgow ilishambuliwa na kuzamishwa kwa kasi. Baadhi ya majeruhi na Sultani Khalid walikimbilia katika Ubalozi wa Ujerumani kuomba hifadhi.
Baadhi ya majengo ya Kisultani yaliharibika ikiwa ni pamoja na mnara wa saa uliokuwa katika jumba la maajabu. Baada ya vita hiyo mnara huo ulifanyiwa matengenezo na hadi leo unatumika kama alama ya kumbukumbu ya vita hiyo fupi. Ingawa jumba hilo lina historia ya kipekee, idadi kubwa ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla hawajawahi kulitembelea na kujionea urithi wa dunia.
Inasemekana kuwa kizazi cha sasa hakioni ajabu yoyote kwa kuwa umeme, mabomba ya maji ndani ya nyumba na lifti ni mambo ya kawaida katika nyumba nyingi za kisasa. Pia kuna tetesi kuwa nguzo 40 zilizopo kwenye jumba hilo ni makaburi ya watumwa ambao walizikwa wakiwa hai.
Hata hivyo hakuna taarifa sahihi zinazothibitisha madai hayo. Ni vyema kutembelea jumba hilo na kujionea maajabu yaliyopo, muundo wa kipekee wa jumba hilo pamoja na kujifunza mambo ya kale katika historia ya utamaduni wa Zanzibar na mwambao wa Waswahili
Jumba la Maajabu linavyovutia utalii Zanzibar Jumba la Maajabu linavyovutia utalii Zanzibar Reviewed by WANGOFIRA on 04:56:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.