Vijana watakiwa kuanzisha miradi
Muleba. Vijana wilayani Muleba, mkoani Kagera wametakiwa kujenga tabia ya kuthubutu katika uwekezaji kwa kuanza na mitaji midogo wakitumia nguvu zao ili kuharakisha maendeleo na kujikwamua na umaskini.
Ofisa Vijana wilayani Muleba, Simi Nyamberwa alitoa wito huo juzi baada ya kukagua jengo la kijana aliyeanza na mtaji wa kuuza kuni na dagaa kwa rejareja.
Nyamberwa alisema kijana huyo, Naftari Tibendelana baada ya kuongezeka mtaji wake alianzisha biashara nyingine ya ujasiriamali, hivi sasa amekuwa mwekezaji anayesaidia wenzake kupata ajira.
Alisema vijana wana fursa za kutumia akili na nguvu zao kwa kutumia ubunifu na kufanya mambo makubwa yanayoweza kuwainua, hatimaye kujikwamua na umaskini kuanzia ngazi ya familia.
“Vijana mkiongeza jitihada ya kujiajiri, halmashauri za wilaya kwa kutumia mapato yake ya ndani zitawaongezea mitaji,” alisema Nyamberwa.
Alitoa mfano wa vijana 20 walioko Izigo Talanta Saccos Ltd, walioanza na mtaji wa Sh100,000 hadi sasa wamekuza mtaji wao hadi Sh80 milioni, huku vikundi vikiongezeka.
Tibendelana alisema licha ya kujenga hoteli kwa gharama ya Sh950 milioni, vijana wanahitaji kusaidiwa na Serikali kupata elimu ya ujasiriamali kujiongezea mitaji.
Alisema baada ya mtaji wake kuongezeka, alihamia mjini Muleba na kuanzisha biashara nyingine, huku akijipanua na kujifunza kutoka kwa watu wengine
Vijana watakiwa kuanzisha miradi
Reviewed by WANGOFIRA
on
05:03:00
Rating:
No comments: