Chifu Adam Sapi Mkwawa wa Pili, kusubiri miaka 7 aongoze Wahehe


Kijana huyo si mwingine bali ni Adam Abdul, mtoto pekee wa kiume wa marehemu Chifu Abdul Adam Sapi Mkwawa wa Kabila la Wahehe wenyeji wa Mkoa wa Iringa, aliyefariki Februari, mwaka huu.
Lakini sasa watu walio katika utawala wa Wahehe, kabila lililo Nyanda za Juu Kusini, wanamtambua kijana huyo kuwa ni Chifu Adam, akiwa mwenye umri mdogo zaidi kurithi nafasi  hiyo ya kutawala kutoka ukoo wa Mkwawa akiwa mjukuu wa Chifu Adam Sapi Mkwawa aliyekuwa pia Spika wa kwanza mweusi wa Bunge nchini.
Kijana huyo amekuwa mtawala wa sita kushika mamlaka hayo, pia mwenye umri mdogo zaidi kuongoza mamilioni ya watu wa kabila hilo katika historia yao, akitanguliwa na baba yake aliyekuwa chifu wa tano.
Utawala wa Chifu Adam Mkwawa ulio mkoani Iringa, unabaki kuwa miongoni mwa tawala chache za kikabila zilizosalia Tanzania, zikionyesha picha ya hali halisi ya uongozi wa jamii za Kiafrika kabla ya ukoloni kuingia na kuharibu mfumo huo katika maeneo mengi na kusimika mfumo wake unaoendelea kutumika kwenye mataifa mengi yaliyotawaliwa na mataifa kutoka Ulaya na Amerika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za kabila hilo, Chifu Adam Mkwawa analazimika kusubiri hadi atakapofikisha umri wa miaka 20 Kabla ya kukabidhiwa rasmi uongozi. Wazee wa kimila wa Wahehe wamemweka baba mdogo wake, Hassan Mkwawa kumsaidia kazi hiyo.
Kiongozi huyo ambaye jina lake la asili ni Mfwime wa pili au Adam Abdul Adam Sapi Mkwawa, alizaliwa mwaka 2001. Anaishi na familia yake kwenye makazi yao yaliyopo eneo lenye pilika nyingi liitwalo Samora mjini Iringa, ambako marehemu baba yake aliishi kwa karibu muda wote wa maisha yake.
Kama ilivyo kwa watoto wengine wengi wa umri wake, Chifu Adam anasoma Shule ya Msingi Highland, ambayo ni ya binafsi.
Alivyozaliwa
Mama mzazi wa chifu huyo, Shamira Abdul anasema, Adam alizaliwa kwa bahati na amekuwa na bahati katika familia yao kwani haikuwa jambo lililopangwa.
Anasimulia kuwa katika maisha yake na marehemu mumewe, walijaliwa kupata watoto wanne, wote wakiwa wa kike, jambo lililowafanya kukaa kimya wakiamini hawatapata tena mtoto.
Hata hivyo, alipopata ujauzito na mtoto wa kiume kuzaliwa, kwao waliitafsiri kuwa ni bahati na baraka kubwa kutoka kwa Mungu.
“Baada ya kupata mtoto wa kwanza na pili wote wa kike, mama mkwe wangu alishauri ninywe dawa ya kiasili ili inisaidie kuwa na uwezo wa kupata mtoto wa kiume,” alisema Shamra.
Anaeleza kwamba akiwa kama amechanganyikiwa kwa yaliyotokea, alikunywa dawa hiyo ambayo hata hivyo, haikubalidi chochote kwani alipata ujauzito na kujifungua tena mtoto wa tatu wa kike na baadaye wa nne, pia wa kike.
“Nilimshukuru Mungu kwa ajili ya baraka zake kutupatia watoto hao wannne nasi kwa imani tukaamua tusizae tena, lakini kumbe Mungu alikuwa na mipango yake kwetu, kwa sababu mwaka 2001 Adam alizaliwa,” anasema Shamra na kuongeza:
“Lazima nikiri kwamba ujauzito wa Adam ulinipa wakati mgumu hata nilielezwa kwamba nitajifungua kwa njia ya upasuaji.”
Anafafanua kwamba hilo lilimtia hofu kwa kuwa watoto wote wane waliotangulia alijifungua kwa njia ya kawaida.
“Lakini mwishowe kila kitu kilikwenda vizuri, nilijifungua Adam kwa njia ya kawaida, nikasema; hii ni zawadi niliyopewa na Mungu kwani nimepitia milima na mabonde wakati wa ujauzito wa kijana huyo, nikauambia moyo wangu kwamba huyu (Adam) atakuwa mtoto wangu wa mwisho,” anasema.
Ndoto ya mama
Shamra anasema ndoto yake ni kuona Adam anapata elimu bora kama wazazi wengine wanavyopenda kwa watoto wao.
“Chifu hana mshahara, anahitaji kuwa na maarifa na nyenzo za kumwezesha kupata fedha na atakapohitajika kutekeleza majukumu yake inabidi awepo wakati wote hivyo, anahitajika kuwa na taaluma itakayomwezesha kuhimili ushindani kwa nafasi yake ya uongozi,” anasema Shamra.
Adam azungumza
Chifu huyo anayetarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwezi ujao anasema hajaona tofauti yoyote kati ya kipindi kabla ya kusimikwa kuwa chifu na baada ya kupewa wadhifa huo.
“Mimi ni yuleyule.” anasema Chifu Adam kwa sauti ya upole huku akitabasamu na kuongeza: “Hata rafiki zangu shuleni wanaona mimi ni yuleyule, tunafahamiana na kucheza pamoja kabla sijawa chifu na hata sasa. Sidhani kama cheo changu kitabanibadili nilivyo mbele ya wenzangu, kila kinachofanyika kwenye maisha yangu sasa ni kipya, lakini muda unavyokwenda nitaelewa yote kwa usahihi.”
Heshima katika familia
Mbali na umri wake mdogo, familia yake inaheshimu nafasi na nguvu za utawala kwake wa kichifu.
Mwenyewe anasema kuna mambo yanayotakiwa kuyatolea uamuzi, ambayo familia huhitaji ruhusa au uthibitisho wake na kwamba kitakachotekelezwa ni kile alichoridhia.
“Kuna mambo yanahitaji mamlaka iamue, dada zangu hutafuta ushauri na maoni yangu, hivyo huamua kwa kadiri ninavyowashauri. Naamini niyo ni namna ya kunilea kiuongozi,” anasema Chifu Adam.
Ndoto za chifu
Akizungumzia ndoto zake Chifu Adam anasema ni kuwa mhandisi na kwamba kwa sasa kipaumbele chake ni kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto hiyo.
Mshabiki wa Arsenal na Yanga
Kiongozi huyo kijana hayupo kando na ushabiki wa soka. Anabainisha kuwa ni shabiki wa timu ya Arsenal ya Uingereza na kwa hapa Tanzania anaishabikia klabu bingwa ya soka nchini, Yanga.
Mwalimu
Mwalimu wa sayansi wa chifu huyo, Musa Lwila anasema amemfahamu Adam katika miezi michache iliyopita baada ya kuhamishiwa shuleni hapo na katika kipindi hicho, amepata muda wa kutosha kufahamu ni mtoto wa aina gani.
“Ni mchapakazi hodari anayetambua majukumu yake kama mtoto na mwanafunzi, naamini atakuwa kiongozi mzuri,” anasema Lwila.
Mwanafunzi
Mwenzake wanayesoma darasa moja, Mariam Mbarak (12), anasema anajifunza mambo mengi kutoka kwake.
“Ni rafiki mwema ingawa sasa yeye ni chifu, hajabadilika. Tuliposikia amekuwa chifu, darasani tulifurahi kwa sababu ya jambo la kipekee kuwa na urafiki na chifu. Tunajua atakuwa kiongozi mzuri hapo baadaye,” anasema akibashiri.
Rafiki
Rafiki wa Chifu Adam waliyesoma pamoja kabla ya kuhamia Highland, Travis Julius (12), anasema katika miaka sita iliyopita alipomfahamu mwenzake huyo, anaamini uamuzi wa kumteua kuwa chifu ni sahihi.
“Adam ni rafiki yangu, hufanya mambo sahihi kwa wakati sahihi na anapobaini amemkosea yeyote huomba msamaha haraka. Niliposikia amekuwa chifu nilifurahia kwani anastahili kushika nafasi hiyo,” anasema Travis.
Vita ya umaskini
Kama ilivyo kwa makabila mengine Tanzania, Wahehe wanaishi katika umaskini ingawa wanaamini Chifu adam atasaidia kuondoa tatizo hilo.
“Umri wake ni ishara tosha ya mafanikio ya baadaye, tunafurahi kuwa na kiongozi kijana, tunafuata vyema mila na desturi zetu kuchagua chifu,” anasema Zuberi Witala, mfanyakazi katika Makunbusho ya Chifu Mkwawa yaliyopo Kalenga na mwanafamilia.
Chifu Adam Sapi Mkwawa wa Pili, kusubiri miaka 7 aongoze Wahehe Chifu Adam Sapi Mkwawa wa Pili, kusubiri miaka 7 aongoze Wahehe Reviewed by WANGOFIRA on 05:08:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.