VYAKULA NA MAGONJWA: Hatari ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya kopo





Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa maziwa ya mama ni chanzo kizuri cha lishe bora kwa watoto kuanzia wachanga na ni hakikisho bora la uhai na makuzi ya mtoto.
Shirika hilo linafafanua kuwa watu walionyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita, wana nafasi ndogo  ya kuwa na unene ule unaozungumziwa mitaani kama matipwatipwa, kupata ugonjwa wa kisukari na wana uelewa mkubwa wa mambo.
Licha ya umuhimu huo wa maziwa ya mama, takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) katika ripoti yake ya hali ya watoto duniani ya mwaka 2011, zinaonyesha kuwa ni asilimia 32.6  ya watoto milioni 136.7 waliozaliwa dunia nzima wanaonyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza kwa mfululizo. 
Ingawa hapa nchini takwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watoto kiasi cha asilimia 97 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wananyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi fulani cha maisha yao, taratibu za unyonyeshaji zinazotekelezwa hazikidhi viwango vya ubora vinavyopendekezwa na wataalamu wa afya na ulishaji wa watoto.
Kwa mfano, ni asilimia 49 ya wanawake wanaojifungua ndiyo wanaoanzishia watoto wao kunyonya maziwa ya mama katika muda sahihi baada ya kujifungua.
Maziwa ya kopo yanazidi kupata umaarufu duniani na hapa nchini, kutokana na ukweli kuwa kina mama wengi wanaamini kuwa maziwa hayo yanaokoa muda wao na kuwapa fursa ya kwenda kutimiza majukumu mengine nje ya nyumba zao. Kwa hiyo elimu zaidi inahitajika.
Hatari ni zipi?
Hatari ya kwanza ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya kopo ni kuwa mara nyingi hupata maambukizi ya maradhi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa maziwa ya kopo hayana kinga inayojulikana kwa kizungu kama ‘antibodies.’
 Kinga hii ipo katika maziwa ya mama na hasa yale maziwa ya kwanza anayoyatoa mama baada ya kujifungua. Pia, maziwa ya kopo hayana virutubisho vyote muhimu anavyovihitaji mtoto mchanga ili aweze kukua vizuri.
Zaidi ya hayo, mtoto anayenyonyeshwa maziwa ya kopo anaweza kupata maambukizi ya maradhi kama maziwa yataandaliwa kwa kutumia maji yasiyokuwa safi wala salama; ikiwa chupa na chuchu za kumnyonyeshea mtoto hazikusafishwa vizuri au maziwa yamewekwa kwa muda mrefu katika hali ya joto na kuwezesha vijidudu vya maradhi kuzaliana.
Hatari ya pili, mara nyingi watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya kopo hawashibi. Maziwa ya kopo ni gharama kubwa na familia nyingi hazimudu.
Kinachotokea maziwa hayo yanaongezwa maji mengi na hivyo mtoto hashibi. Au watu wengine wanampa mtoto mwenye umri chini ya miezi sita uji baada ya kushindwa kumudu gharama ya maziwa ya kopo. Kwa mfano, mtoto wa miezi mitatu anahitaji maziwa ya kopo kilo moja kila wiki.  Ni watu wachache wanaoweza kumudu gharama yake hapa nchini.
Hatari ya tatu, watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama wanaweza kupata matatizo ya kiafya kama kuharisha, pumu, kifua kisichosikia dawa, sikio, kuharisha na mzio .  Zaidi ya hayo, nchi yetu inakabiliwa na uingizaji wa vyakula vikiwamo maziwa ya kopo ambavyo siyo salama.
Hatari ya nne, mtoto anayenyonyeshwa maziwa ya kopo anaweza kukataa kabisa kunyonya maziwa ya mama pale atakapopewa.
VYAKULA NA MAGONJWA: Hatari ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya kopo VYAKULA NA MAGONJWA: Hatari ya kumnyonyesha mtoto maziwa ya kopo Reviewed by WANGOFIRA on 05:21:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.