PIRAMIDI YA AFYA: Kurefusha uume na madhara yake kiafya


By Dk Shita Samwel, Mwananchi
Leo tutaona njia maarufu ambazo zipo katika matangazo mbalimbali ikiwamo magazeti, mabango ya matabibu wa kienyeji, mitandaoni pamoja na zile zilizoshindwa kukidhi vigezo vya kutumika na kuingizwa katika miongozo ya matibabu ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Nikianza na kifaa maarufu ambacho kipo mitandaoni sana na pengine waliokiingiza katika sokoni waliwahi kukutumia barua pepe na huku wakikupa maneno mazuri ya kukuvutia kununua.
Kifaa hicho kiitwacho ‘Vacuum pump’ ni mfano wa kifaa kama bomba ambalo lina uwezo wa kunyonya hewa. Kifaa hiki hupachikwa katika uume na kuanza kunyonya na kuifanya damu ya ziada iliyopo katika misuli sponji ya uume kuvutwa na kuufanya uume kusimama.
Kisha kuna kipira ambacho hufungwa ili kubana uume uendelee kusimama hivyo hivyo; ni kama vile unapofunga kamba katika kidole mishipa ya damu huminywa ili damu isirudi mwilini.
Ufanisi wake wa kuendeleza uume kusimama na kuurefusha kiasi huwa ni wakati hiyo ringi ipo ikiwa imebana, lakini kuendelea kuwapo kwake kwa dakika 20-30 inaweza kusababisha madhara katika misuli sponji ya uume.
Kifaa hiki pia kinatumiwa na watu wenye tatizo la nguvu za kiume. Hadi  sasa hakuna uthibitisho wa sayansi ya tiba kuwa kifaa hiki ni kinarefusha uume na wala hakipo katika orodha ya vifaa tiba.
Utanuaji wa uume kwa kutumia vitu vizito au mazoezi ya kutunisha misuli hayawezi kufanya kazi katika misuli ya uume ambayo maumbile ya seli zake ni tofauti na misuli ya mikono ambayo ikibebeshwa vyuma au vitu vizito huongezeka ukubwa.
Misuli ya uume huwa ni kama vile sponji, uzito wake na umbile lake huongezeka tu pale damu inapomiminika humo.
Ingawa kuning’niza vitu vizito katika uume tepetepe kunaongeza urefu kiasi, lakini pana changamoto kubwa hapa na kunahitajika uvumilivu wa ziada kutekeleza njia hii.
Utahitaji kuvaa kifaa maalumu chenye uzito katika nguo yako ya ndani kwa saa nane kwa siku kwa kipindi cha miezi sita. Mwisho wake inahitaji uwe na bahati ili kufanikiwa angalu kuongezeka inchi moja.
Vifaa vingine ambavyo vinatumika kupachikwa katika uume ambavyo hakuna uthibitisho wa kisayansi kama ni salama na endapo vina ufanisi, ni pamoja na mashine ziitwazo;  penis enlarger pump, penis extender machine na stretching machine.
Streching machine ni kifaa kinachotumiwa kukiweka katika uume na kisha kuanza kuvuta tishu za uume. Pia haina uthibitisho na ufanisi wake.
Madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja kuchanika kwa tishu za uume, maumivu sugu, kuhisi ganzi na kupasuka kwa mishipa ya damu.
Vidonge, mafuta na krimu mbalimbali navyo havifanyi kazi kwa ufanisi unaofanikisha kutatua tatizo hilo. Watengenezaji huchanganya virutubisho lishe na mitishamba na kuichanganya.
Vitu hivi vimechanganywa na homoni za kiume zenye uasili wa steroids ambazo hupakwa maeneo hayo ili kunenepesha maeneo ya mwilini.
Hata hivyo, hakuna uthibitisho wowote wa kisayansi juu ya dawa hizo kuwa na ufanisi na usalama kwa mwili wa binadamu.
Utakuta tangazo zuri lenye maneno ya kuvutia na kukupa matumaini makubwa ya kutatua tatizo, wanadiriki kuweka picha feki ambazo zinaonyesha umbile kabla na baada ya kutumia dawa hiyo.
Unapoona na kama hujui utakimbilia kuinunua, matabibu wa kweli wa afya   hawajitangazi kwa njia hiyo kwani ni kinyume na maadili yao.
PIRAMIDI YA AFYA: Kurefusha uume na madhara yake kiafya PIRAMIDI YA AFYA: Kurefusha uume na madhara yake kiafya Reviewed by WANGOFIRA on 05:03:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.