Makonda: Tume ya maadili na Magufuli wanamdanganya nani?

Image result for photos of makonda and magufuli


Pamoja na kwamba katiba yetu inasema wazi kuwa Tanzania itaongozwa kwa misingi ya usawa; bila ubaguzi, uonevu na upendeleo, kinachoendelea kuhusiana na baadhi ya watu ni kinyume kabisa na maagizo ya katiba.

 Katiba yetu imekuwa ikivunjwa kirahisirahisi na baadhi ya watawala kiasi cha kugeuka kama kitabu cha hadithi tofauti na inavyopaswa kuwa. Mfano wa hivi karibuni ni pale baadhi ya waheshimiwa, tena wakiwa mbele ya bunge, walimtuhumu Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda kwa kujilimbikizia mali nyingi na kufuja fedha kama kusafiri ughaibuni tofauti na katazo la rais tena kwa muda mfupi aliokuwa madarakani. 

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alikaririwa akiliambia bunge akisema “Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa shilingi milioni 600, Makonda amempa mke wake gari aina ya Mercedez Benz lenye thamani ya  Dola 250 za Marekani (shilingi milioni 550) kama zawadi ya birthday.” Hizi tuhuma si ndogo; na wala si za kupuuzia. Je rais Magufuli au washauri na wasaidizi wake hawasomi magazeti kiasi cha kutojua tuhuma hizi nzito?  Je Magufuli, kama mamlaka iliyomteua Makonda amechukua hatua gani ukiachia mbali kutotoa maelezo yoyote?

            Kwa upande wake, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeonyesha wazi uhovyo kwa kujitenga na kile kilichopaswa kuinyima usingizi kama kweli ipo kwa misingi ya kulinda uwajibikaji na kupambana na ufisadi na wizi wa fedha za umma.  Je Tume hii imepigwa ganzi kama anavyosema Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Rushaku (Msukuma) ambaye alikaririwa akihoji “utawala bora, Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria…kwanini mmepigwa ganzi?”

Msukuma aliongeza kumwaga mtama akisema “anatumia (Makonda) Lexus ya petroli ya Sh milioni 400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi wa Serikali. Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi? Na hawa mawaziri tulionao humu kwanini wamepigwa ganzi?”

Kwa wanaojua uchungu na kasi ya Magufuli vya kupambana na uoza, walidhani kuwa angechukua hatua mara moja bila kukaa kimya kama ilivyo. Je ina maana ni kweli kuwa rais na taasisi nyingine kama vile polisi, Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) wamepigwa ganzi kiasi cha kufumbia macho uoza na tuhuma hizi? Je hii inajenga picha gani kwa watanzania wa kawaida? Je kwanini Makonda, kama yanayosema ni uongo, amekaa kimya bila kutoa maelezo wala kwenda mahakamani kusafisha jina lake?

Kwa wanaojua matatizo ya kiutawala ya taifa letu watakumbuka kuwa, ukimuondoa marehemu baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere, karibia waliomfuata wote walikuwa na mizigo yaani kukingia kifua watu wao wa karibu kiasi cha kujengeka dhana kuwa walikuwa wakiwatumia kuliibia taifa. Mifano ni mingi. Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alikuwa naye marehemu Kighoma Malima. 

Hakutaka aguswe; na ilipotokea akaguswa, Mwinyi alijifanya haoni wala hasikii. Benjamin Mkapa alikuwa nao akina Basil Mramba na Daniel Yona wakati Jakaya Kikwete alikuwa na akina Shukuru Kawambwa na Hawa Ghasia na wengine. Sasa rais Magufuli ameanza kujenga picha kuwa anaye Makonda. Hii ni tofauti na alivyomshughulikia rafiki na waziri wake wa zamani Charles Kitwanga kwa ulevi. 

Ajabu ya maajabu, Magufuli alipomtimua kazi Kitwanga hakuchelewa wala kueleza kama tuhuma zake za ulevi zilithibitishwa na mkemia mkuu. Kwanini anasitasita kwa Makonda’ na kunani? Sitaki niamini kuwa Magufuli hajui tuhuma za mkuu wake wa mkoa wala kukerwa na tuhuma hizi kiasi cha kuzinyamazia. Je rais anafanya uchuguzi ili achukue hatua au ana-buy time ili mambo yapowe na ulaji uendelee? 

Je Makonda atanusirika na tuhuma hizi ambazo zinakolezwa moto na ukimya wake pamoja na ule wa rais ukiachia vyombo husika kuonekana kumgwaya? Je huku si kuvunja na kudharau katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ameapa kuilinda na kuitetea kama sheria mama inayompa madaraka aliyo nayo?

Kwa vile tuhuma dhidi ya Makonda ni nzito na zimetolewa wazi na watu wazito, itakuwa jambo la aibu na ajabu kama wahusika wataendelea kulinyamazia au kutafuta visingizio kama ilivyoonyesha Tume husika. Inashangaza kuona Tume husika ikijificha nyuma ya sheria wakati kila kitu kiko wazi. 

Sasa nini maana ya sheria kumtaka kila mtanzania atakayeshuhudia au kujua kuwa kosa la jinai limetendekea alipoti polisi au kwenye mamlaka zinazohusika? Je TAKUKURU nao wanangoja wapelekewe maombi? Kwanini watuhumiwa wa biashara haramu ya mihadarati hawakupewa fursa hii; na badala yake walikamatwa na wengine kuwekwa ndani baada ya kupokea tuhuma?

 Je hapa polisi, TAKUKURU, Tume na Magufuli wanataka kumdanganya nani; na ili iweje? Je Makonda ni nani katika Tanzania? Mbona Mwl. Nyerere alipotuhumiwa na marehemu Oscar Kambona alitoa maelezo na utetezi haraka bila kujali nafasi yake tena ambayo kwa mfumo wa chama kimoja uliokuwepo, angejinyamazia na mambo kuisha?


Chanzo: Tanzania Daima
Makonda: Tume ya maadili na Magufuli wanamdanganya nani? Makonda: Tume ya maadili na Magufuli wanamdanganya nani? Reviewed by WANGOFIRA on 19:20:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.