Wadau wa haki za binadamu nchini waendelea kusisitiza adhabu ya kifo ifutwe

Licha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutotekeleza adhabu ya kifo kwa zaidi ya miaka 20. Imeendelea kusisitizwa kuifuta sheria ya adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa makosa ya mauaji kwa kuwa haisaidii kupunguza makosa hayo na kwamba iangalie chanzo cha tatizo hilo kwa lengo la kufanyia marekebisho.

Ushauri huo umetolewa jana na wadau mbalimbali wa haki za binadamu katika kongamano la kuijadili adhabu ya kifo nchini, lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN).

Wadau hao walisema kuwa, falsafa ya ukuaji wa adhabu huzingatia vigezo viwili ambavyo ni kutoa funzo kwa jamii pamoja ma kumrekebisha mkosaji. Wadau hao waliitumia hoja hiyo kuisisitiza serikali kufuta adhabu ya kifo kwa kuwa endapo mtuhumiwa akiuawa hatopata fundisho na pia kifo chake kinatafsiriwa sawa na kosa hilo kujirudia.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Hellen Kijo-Bisimba alisema kituo hicho hakitaacha kuishauri serikali kuifuta adhabu hiyo kwa kuwa haisaidii kutokomeza matukio ya mauaji na pia huenda ikaathiri watu wasio na hatia.

“Inabidi serikali iangalie chimbuko la matukio ya mauaji ili litokomezwe na si kuhukumu watu kwa adhabu ya kifo, hatumaanishi wasihukumiwe bali watafutiwe adhabu nyingine kwa kuwa tangu kuanza kutumika adhabu hii matendo ya mauaji hayajapungua,” alisema.

Aliongeza kuwa ” Kumuua mtu si suluhisho bali kosa hilo linazidi kufanyika na si sahihi. LHRC tunaendelea kuipinga adhabu hii sababu haisaidii kupunguza mauaji,”

Bisimba alidai kuwa, asilimia kubwa ya wanaohukumiwa adhabu ya kifo ni watu wasio na kipato na kwamba hali hii huonyesha adhabu hiyo hutekelezwa kitabaka zaidi.

Mwakilishi wa UN, Roeland Van de Geev alisema kuwa shirika hilo halitailazimisha serikali kuifuta sheria hiyo bali litawezesha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) yanayohusika na haki za binadamu nchini kuishauri serikali kufuta adhabu hiyo.

“Nchi zaidi ya 140 duniani zimefuta adhabu hiyo, na hakuna matukio ya kutisha ya mauaji katika nchi husika, mfano Marekani inatekeleza adhabu ya kifo lakini matukio ya mauaji bado yanaendelea. Hii inamaanisha kwamba suluhu pekee ni kutibu au kuzuia vyanzo vya matukio hayo,” alisema.

Alishauri kuwa “Adhabu hii hafai kutekelezwa sababu inaondoa utu wa mtu. Tanzania pamoja na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki zifute sheria hiyo.”

Bahame Tom Nyanduga kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora alisema adhabu hiyo haistahili kuendelea kutekelezwa nchini kutokana kwamba ilianzishwa na wakoloni kwa lengo la kulinda utawala wao.

“Haki ya binadamu ya kuishi ndiyo msingi wa haki nyingine, katiba ya 1977 inatambua haki ya kuishi. Mahakama haiwezi futa adhabu hii bali serikali ndiyo yenye wajibu wa kuifuta sheria hiyo hivyo ni vyema ikafanya hivyo,” alisema.

Alisema ingawa serikali haijatekeleza adhabu hiyo kwa zaidi ya miaka 20 lakini inawajibu wa kuifuta sababu watu wanazidi kuhukumiwa.

“Nchi zaidi ya 20 Afrika zimefuta adhabu hii na hatusikii kama kuna kukithiri kwa matukio ya mauaji.Ni vigumu kuhusisha adhabu ya kifo kama suluhisho pekee la kutokomeza mauaji,” alisema.

Sheikh Ally Hemko kutoka Baraza Kuu la Waisilamu Tanzania (Bakwata) alishauri jamii kuepukana na vitendo vya mauaji kwa kuwa dini hairuhusu.

“Dini yetu hufundisha kuwa mtu anayeua nae aue ingawa pia inasisitiza kuua ni dhambi hivyo ili kuondokana na utata huo, jamii inawajibu wa kuacha vitendo hivyo sababu hata kama sheria hiyo ikifutwa watu wasio wema watazidi kuua,” alisema.
Wadau wa haki za binadamu nchini waendelea kusisitiza adhabu ya kifo ifutwe Wadau wa haki za binadamu nchini waendelea kusisitiza adhabu ya kifo ifutwe Reviewed by WANGOFIRA on 01:41:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.