Neno la Mwisho la Mkuu wa Mkoa wa Arusha Felix Ntibenda Aliyetumbuliwa Juzi na Rais Magufuli


Mkuu wa Mkoa wa Arusha aliyeondolewa, Felix Ntibenda amekabidhi ofisi huku akitoa neno la mwisho la kuwakaribisha Kigoma baadhi ya maofisa waliokuwapo kwenye hafla hiyo.

“Karibuni sana Kigoma,” ndiyo lilikuwa neno la mwisho kwa Ntibenda alilolitoa baada ya kukabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa mpya Mrisho Gambo, hafla iliyofanyika kwa muda mfupi.

Ntibenda aliyehamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu, baada ya kusema neno hilo alipanda gari na kuondoka. 

Kabla ya makabidhiano,alikuwa wa kwanza kufika ofisini saa 3.30 asubuhi na kulazimika kusubiri hadi 5.05 asubuhi, alipowasili mkuu mpya wa mkoa Gambo aliyeapishwa Ikulu jijini Dar es Saalam juzi na Rais John Magufuli. 

Gambo kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa wilaya ya Arusha na aliwasili ofisini akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama.

Aliingia ofisini kwake na kukutana na Ntibenda, ambapo walifanya makabadhiano na kutoka huku wakizungumza.

Makabidhiano hayo yalifanyika haraka kwa kile ambacho kilielezwa na mkuu mpya wa mkoa kutakiwa kusafiri kwenda Loliondo kupokea Mwenge wa Uhuru.

Katibu Tawala, Richard Kwitega alisema Gambo baada ya makabidhiano alikuwa na ratiba moja tu kuzungumzia mbio za Mwenge wa Uhuru ambao leo unaingia mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Gambo alisema jana alitarajia kuzungumzia mbio za Mwenge pekee na kwamba unatarajiwa kuzindua miradi yenye thamani ya Sh12.9 bilioni.

UVCCM wampokea Gambo 
Kama ambavyo, ilitarajiwa jana, viongozi wa UVCCM Mkoa wa Arusha wakiongozwa na mwenyekiti wao, Lengai ole Sabaya walijitokeza katika mapokezi ya Gambo. 

Sabaya alisema wanampongeza Rais Magufuli kwa kusikiliza kilio chao na pia kumteua kijana kuongoza mkoa.

“Sisi kama UVCCM tumekuja hapa kumpongeza mkuu mpya wa mkoa na tuna imani naye sana kuwa atasaidia maendeleo ya mkoa huu,” alisema.
Neno la Mwisho la Mkuu wa Mkoa wa Arusha Felix Ntibenda Aliyetumbuliwa Juzi na Rais Magufuli Neno la Mwisho la Mkuu wa Mkoa wa Arusha Felix Ntibenda Aliyetumbuliwa Juzi na Rais Magufuli Reviewed by WANGOFIRA on 00:24:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.