VYOMBO VYA DOLA MWANZA VYAPANGULIWA, WENGINE WAHAMISHWA.

 John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza 

Serikali imepangua uongozi wa vyombo vya dola mkoani Mwanza kwa kuwahamisha vituo vya kazi watendaji wakuu akiwamo Kamanda wa Polisi, Justus Kamugisha aliyehamishiwa mkoani Mbeya. Mkuu wa Mkoa John Mongella alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha utendaji wa taasisi hizo na kukabiliana na matukio ya uhalifu yaliyotikisa mkoa huo tangu kuanza kwa mwaka huu.
“Kwa kipindi kifupi cha wiki mbili tangu nihamie Mwanza, nimeshuhudia matukio kadhaa ya uhalifu, yakiwamo mawili ya ujambazi yaliyoishia kwa raia wema kupoteza maisha na mamilioni ya fedha kuporwa,”alisema Mongella. 

“RPC amehamishiwa Mbeya ambako nadhani labda kuna changamoto kidogo kulinganisha na zile za Mwanza alizoonyesha kushindwa,”alisema Mongella.

Mongella alisema pamoja na RPC, vigogo wengine waliohamishwa kutoka Mwanza ni pamoja na ofisa utumishi wa jeshi la polisi, ofisa Idara ya Usalama wa Taifa na kamanda wa mkoa wa Idara ya Uhamiaji.

Akizungumza na viongozi, watumishi na watendaji wa vyombo vya dola wilayani Magu, Mongella aliwataka kutimiza wajibu kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao, akionya watakaoshindwa watawajibishwa.

“Haiwezekani majambazi yatambe kwa kuvamia, kupora na kuua wananchi watakavyo, na vyombo vya dola na viongozi wenye dhamana ya ulinzi na usalama wapo wanashuhudia. Kila mtu atimize wajibu wake,” alisema Mongella.

Alitumia fursa hiyo kuuagiza uongozi wa polisi wilaya ya Magu kukomesha matukio ya mauaji ya kukata watu kwa mapanga yanayodaiwa kufanywa na watu wanaokodishwa.

Ndani ya kipindi cha miezi miwili ya Februari na Machi, Jiji la Mwanza limekumbwa na matukio sita ya ujambazi ambayo yamechukua maisha ya watu sita waliouawa kwa kupigwa risasi, huku mamilioni ya fedha yakiporwa kutoka maduka ya fedha kwa njia ya mitandao.
VYOMBO VYA DOLA MWANZA VYAPANGULIWA, WENGINE WAHAMISHWA. VYOMBO VYA DOLA MWANZA VYAPANGULIWA, WENGINE WAHAMISHWA. Reviewed by WANGOFIRA on 23:22:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.