UBAGUZI KWENYE UTOAJI WA MIKOPO ELIMU YA JUU CHANZO CHA KUUA VIPAJI VYA VIJANA WA KITANZANIA
Na,
BARAKA NGOFIRA
0763580901, 0716216249
Kwanza kabisa nianze
kuwashukru wadau wote wa elimu kwa kuonesha juhudi zao kubwa za kuhakikisha
wanapigana vilivyo kuhakikisha wanafunzi wote wa vyuo vikuu wanapata mikopo
bila kuzingatia fani na masomo wanayoyasoma.
Shukrani zangu za dhati ziwaendee wazazi na wadhamini
mbalimbali walioamua kuwasomesha wanafunzi ambao hawakupata mkopo kwa sababu ya
vitivo na masomo wasomayo siyo
kipaumbele “priority” au havina
kipaumbele katika kupewa mkopo wa vyuo vikuu.
Sitakuwa na maana ya kuandika makala haya pasipo
washukru watanzania wote bila kuzingatia itikadi za vyama vyao kwa kuungana na
Rais John Pombe Magufuli katika harakati zake za kutumbua majipu ambayo
yalikuwa yamegeuza nchi yetu shamba la bibi kwa kujichotea mali za watanzania
bila hata woga ambayo baadhi yao kwa sasa yameanza kutumbuliwa na wengine
wameanza kukamuliwa vilivyo ili watapike mali walizotuibia wakidhani
hawaonekani.
Inasikitisha sana lakini hamna namna nyingine zaidi ya
kutumbuliwa, kwangu nimpongeze Rais Magufuli na timu yake yote ya utendaji tu nyuma yako hatutakuangusha daima katika juhudi za kutumbua majipu ambayo
yalitutesa na kusababisha watoto wengi wa watanzania kushindwa kusoma elimu ya
juu kwa kukosa mikopo. Na wengine kusoma fani ambazo hazikuwa ndoto zao ambapo
kwa sasa wamehitimu masomo yao lakini hawajui wapi waende, kwani hata masomo yaliyoyasoma mioyo yao
haipendi bali walisoma kwa sababu tu wapate mkopo na wao kuingia kwenye orodha
ya wasomi wenye shahada.
Siwalaumu bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HESLB) kwani
wao ni watekelezaji tu na ndiyo maana muda mwingi baadhi ya watendaji wao
hutujibu vibaya kwani wao hupokea maagizo kutoka kwa wakubwa wao. Lawama na
malalamiko haya yanawapasa yawaendee wizara zote katika nchi yetu kwa wao
kutopaza kelele na kurizika na kazi walizonazo maofisini kwao, kwani wanadhani
wataishi milele kwenye ofisi hizo ambazo wengine wamezigeuza kuwa sehemu na
vijiwe vyao vya upigaji na kusahau kuwa walisomeshwa kwa kodi za watanzania
ambao leo hii wajukuu wao wanabaguliwa kuwa wao wanasoma vitivo ambavyo si
kipaumbele “non priority”.
Wamesahau kuwa kuna maisha baada ya wao kustaafu au kufariki pia hawajiulizi kuwa wakiondoka maofisini wakina nani wataiingia na watakuwa na
uwezo ganiwa kufanya kazi walizozifanya kwa weledi mkubwa kwani
walizipenda au ndo kusema kuwa
walishapiga vilivyo na ndo maana wengine ukienda maofisini kwao wanakuangalia
kana kwamba shida yako ishafanyiwa kazi kumbe ndo kwanza umeingia kuongea naye
kuhusu tatizo linalo hitaji msaada wake, au ndo kusema wakiondoka maofisini wanawarithisha
watoto wao waliowasomesha elimu ya kimagharibi, wakafundishwa kuiba na kufuzu
katika fani hizo ili waje waibe kwao na
kufaidisha wazungu mali ambazo waasisi walisema zitunzwe ili watoto wa
kitanzania waje wafaidi?
Ebu jiulize
maswali yafuatayo kisha ujijibu mwenyewe, siku ikitokea vyombo vya habari vyote
vinapiga miziki na magazeti yote kuandika udaku itakuwaje? Na ukiwauliza
wahusika wakakuambia wamekosa wataalam wenye ujuzi wa kuendesha vyombo vya
habari na wanahabari wa kufanya habari za kiuchunguzi “investigative
journalists” unajisikiaje? Na hapo ukamwona mwanao au mtu fulani aliyekuwa na
ndoto za kuwa kama Salim Kikeke ameshindwa kusoma elimu ya juu kisa fani yake
si kipaumbele “non priority”?
Jiulize wakina Ibrahim
Lipumba wa kesho ni wapi kama fani ya uchumi nayo ni “non priority” au nchi
yetu haihitaji wachumi baada ya akina Prof. Lipumba siku zao zikiwa zimepita?
Mimi sijui au ndo kusema watoto wa wakubwa waliosoma na kubobea katika masuala
ya uchumi ndo watakuja wachukue nafasi zao? Kwani wao walisoma nje na
kufundishwa kutuibia sie watanzania wanyonge ambao wengi wa wazazi wetu ni
masikini na hawawezi kutusomesha fani tulizo zitamani kuzisoma na kuishi ndoto
zetu?
Hizo ni baadhi ya fani tu
ambazo ni muhimu sana kwa taifa letu lakini wahusika wameona hawahitaji watu
wengine kwani waliopo wanatosha na watadumu milele. Inasikitisha na kuhuzunisha
sana kuona watoto wengi wa masikini kusoma fani ambazo ukiwauliza kuwa
wanazipenda wanatakujibu nilisoma hii fani ili nipewe mkopo.
Na ndio maana sishangai
kabisa kuona walimu kufanya mapenzi na wanafunzi wao kwa ufinyu wa akili
wakidhani wanaawakomoa huku wao wenyewe wakijiweka kwenye mazingira magumu ya
kazi zao, lakini si kwamba walipenda kuwa walimu bali walisoma ualimu ili tu
wapewe mkopo na wao waesabiwe kuwa ni miongoni mwa wasomi wenye shahada ya
elimu ya juu.
Pia sishangai kuona idadi
ya walimu wengi kuhitimu kila mwaka na kupangiwa mashule ya kwenda kufundisha
lakini kadri wanavyozidi kuajiliwa ndivyo idadi ya wanafunzi wanaofeli inazidi
kuongezeka kila mwaka ukilinganishwa na miaka ambayo kulikuwa na walimu
wachache waliokuwa na wito kutoka mioyoni mwao kuwa waalimu.
Huo ni baadhi ya mfano
ulio hai kabisa na kila mtu anajiuliza pasipo kupata majibu lakini kwa wahusika
watakuambia tumesoma ualimu ili tupate mikopo na ajira kwa uharaka na uhakika
wa ajira. Ndivyo hali ilivyo kwani ni
“priority”. Huwa inaumiza sana pale unapoona mwanafunzi, rafiki yako au mtu
unayekaa naye chumba kimoja anaongea kuhusu masuala ya mikopo na pengine
kukuuliza tunaenda kusaini lini “boom” huku wewe unaye ulizwa hauna, au
anakuambia twende kuangalia majina ya “boom” yamebandikwa cafeteria au Darajani
kwa wale wa chuo kikuu cha Dar es salaam huku wewe unayeambiwa hauna.
Huwa ni simanzi kubwa na huzuni kubwa kwa
wanafunzi ambao hawana mkopo kubaki kulia na mioyo yao na kubaki kuomba wenzao
wenye mikopo wabakize chakula ili na wao wapate walau makombo tu
wanayoyabakiza, lakini muda mwingine ni
vigumu kwa msomaji wangu kuamini niyaandikayo lakini ndivyo hali ilivyo na kama
unabisha omba mwanao au kama wewe ni mwanafunzi wa sekondari ukose mkopo na
wazazi wako wawe wale wenzangu na mimi utaamini niyaandikayo leo.
Nilisikitishwa sana siku
moja nilipopigiwa simu na mdau mmoja wa habari kutoka kigoma na kuniaambia kuwa
anapenda sana kuwa mwanahabari lakini alikosa mkopo kutoka elimu ya juu wa
kumwezesha kusoma elimu ya juu na hivyo ikamlazimu kusitisha ndoto zake
alizokuwa nazo awali na ndipo alikaa nyumbani na mwaka uliofuata akaamua kwenda
kusoma ualimu kwa sababu tu ya uhakika wa kupata mkopo na uhakika wa ajira.
Chonde chonde kwa
wahusika tukumbuke tuyafanyayo leo ndiyo matokeo ya kesho, na kama leo
tunapuuzia mambo ya muhimu kwa kutoona vipaumbele vyake, tukumbuke taifa la
kesho halina wataalamu wa kutosha katiak fani za habari, uchumi, mazingira,
utalii, sanaa, wataalam wa lugha na wengineo wengi na hivyo tujue tunajenga
taifa lenye waalimu wengi wanaofundisha kwa kutopenda hiyo fani na hivyo kujaza
waalimu wanaofundisha waalimu ambao kwa kesho shule nazo zitakuwa haziwahitaji
tena.
Na msije mkashangaa
vyombo vya habari vikabaki kupiga mzuki na kukosa vipindi vya uelimishaji na
kujenga taifa la watu wenye fikra chanya juu ya taifa lao, na magazeti mengi
kugeuka ya kidaku kwa kukosa watu wenye kufikiria mbali juu ya kuibua matatizo
yaliyopo ndani ya jamii zetu na kusababisha muhimili wa nne ya taifa kuvunjika
kwa sababu wataalam wengi waliokuwa na
uwezo wa kufanya kazi hizo vipaji vyao vilizikwa vikiwa hai kwa kukosa mkopo na
kukumbilia fani zenye “priority” au zenye vipaumbele wa kupata mkopo na uhakika
wa ajira mapema.
Lakini mwisho nitaendelea
kuwashukru sana wazazi na wadhamini walioamua kuwasomesha wanafunzi fani zilizo
ndoto zao bila kujalisha wamepata au wamekosa mkopo, kwenu ujira wenu utalipwa
na mwenyezi Mungu siku ile tutakapokuwa tunaulizwa uliitumiaje talanta na
kipaji ulichopewa na mwenyezi Mungu. Hivyo ni muhimu kwa wanafunzi
wanaofadhiliwa na wazazi au wafadhili wengine wana haja ya kujua kuwa
wamejinyima ili wao wasome ili waweze kuziishi ndoto zao.
Na si kama wale
waliofaidi nchi hii na kuifanya shamba la bibi ambalo kila mwenye dhamana
alifanya alivyotaka na kuamua kuweka masharti magumu yanayowalazimisha watoto
wa watanzania oye aye na wa yule mkulima
wa mihogo na mtama ambaye kwake mchicha pori na mboga za majani ambazo hazijui
mafuta wala nyanya na kitunguu ndicho chakula chake cha kila wasiishi ndoto zao
kwani hawana uwezo wa kuwasomesha watoto wao elimu ya chuo kikuu. Na kusahau
kuwa muda utafika wa wao kutapika vile walivyovila kwa uroho wao na tamaa zao
madaraka. Hongera sana Magufuli rais wa Tanzania na Kassim Majariwa mkumbukapo
kuagiza pesa za kujenga barabara tukumbukeni nasi pia wanafunzi tunaosoma fani
waziitazo ni “Non priority” tuliokosa mkopo mwaka wa masomo 2014/2015 maji
yametufika shingoni hatujapewa mkopo wakuu, ndani yauongozi wenu tunaamini
sauti zetu zitasikika na kilio chetu kitajibiwa muda si mrefuili nasi tuziishi
ndoto zetu.
Makala haya yameandikwa
na mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesoma fani ya mawasiliano kwa umma, katika
chuo kikuu cha Dar es salaam ambaye pia ni miongoni mwa wanafunzi ambao
hawajawahi kupata mkopo kutoka bodi ya mikopo ya elimu ya juu kwa miaka yote
miwili ya kuomba kwake. Anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901, 0716216249
au email ya barakangofira@gmail.com.
UBAGUZI KWENYE UTOAJI WA MIKOPO ELIMU YA JUU CHANZO CHA KUUA VIPAJI VYA VIJANA WA KITANZANIA
Reviewed by WANGOFIRA
on
00:15:00
Rating:
No comments: