Weinstein alitaka kulala na Lupita Nyong'o
Mwigizaji huyo mashuhuri kutoka Kenya anaeleza jinsi
ambavyo Harvey Weinstein, meneja ya kampuni ya utengenezaji filamu, alimnyanyasa
kijinsia. Weinstein anasakatwa na sakata la unyanyasaji wa wanawake kadhaa.
Lupita ameliambia gazeti la New York Times kuwa
alikutana na Harvey Weinstein kwa mara ya kwanza Berlin, Ujerumani, katika
sherehe ya tuzo za filamu mwaka 2011. Kipindi hicho Lupita akiwa bado
mwanafunzi katika chuo cha uigizaji nchini Marekani. Alikuwa na ndoto ya kuwa
muigizaji mashuhuri duniani hivyo alipotambuliswa kwa Weinstein alifurahi.
Lakini mwanamke
mmoja ambaye naye alikuwa mtaalamu wa filamu alimuonya Lupita kwamba Weinstein
ni mtu mzuri lakini wakati mwingine anaweza kuwa mwenye mabavu. Lupita alimpa
Weinstein mawasiliano yake, akitumaini kwamba atashirikishwa kwenye kazi za
mtayarishaji huyo.
Muda mfupi baada ya kukutana Berlin Weinstein
alimualika Lupita nyumbani kwake Connecticut, Marekani, kuangalia filamu.
Dereva aliyeagizwa kumchukua Lupita kutoka nyumbani kwake alimtaarifu kuwa
wanaelekea katika mgahawa ambapo Weinstein alikuwa akimsubiri kwa chakula cha
mchana kabla hawajaelekea nyumbani kwake.
Wakiwa hapo Lupita aliagiza kinywaji kisicho na
kilevi, jambo ambalo halikumfurahisha Weinstein. Baada ya mzozano Weinstein
alimwambia mhudumu amletee Lupita kinywaji chenye kilevi kwani yeye ndiye
anayelipia. Lupita hakupendezwa na hilo hivyo akaamua kunywa maji yaliyokuwa mezani.
Walipofika nyumbani kwake Lupita na watoto wa Weinstein walikaa na kuanza
kuangalia filamu.
Baada ya dakika kumi na tano Weinstein alimuita Lupita
akisema angependa kumuonyesha kitu. Lupita alikataa kwani alitaka kufanya kile
alichoalikwa kufanya lakini alipoona Weinstein anamshinikiza sana alikubali ili
kutobishana mbele ya watoto wa Weinstein.
Wanawake wasema walibakwa na Weinstein
Weinstein ni mtengeneza filamu mwenye mafanikio na
ushawishi mkubwa
Weinstein alimpeleka chumbani kwake na kumwambia kuwa
anataka kumkandakanda. Lupita alidhani Weinstein anatania lakini baada ya kuona
kuwa Weinstein anamaanisha anachosema ilimbidi kuwaza kwa haraka jinsi ambavyo
ataweza kujitoa katika sehemu hiyo tata. Akikumbuka alivyojifunza shuleni jinsi
ya kumkanda mtu, Lupita alimshawishi Weinstein amruhusu amkande.
Baada Lupitaya kumkanda mgongo, Weinstein alisema
kwamba anataka kuvua suruali yake.
Lupita alipatwa na hofu na kumwambia Weinstein
kwamba hatafurahishwa na jambo hilo lakini Weinstein aliinuka na kuanza kuvua
suruali yake. Hapo ndipo Lupita alipopata mwanya wa kutoroka na kusimama
mlangoni. Lupita alimwambia Weinstein kama hawaendelei kuangalia filamu ile ni
bora arudi zake shule.
Pamoja na hayo, Lupita anasema upo wakati mwingine
ambapo Weinstein alimwambia anataka kulala naye. Alipokataa, Weinstein
alimtishia kwamba jambo hilo litakuwa na athari kwa kazi yake kama mwigizaji.
Lupita si mwanamke wa kwanza kudai kwamba Weinstein alimnyanyasa
kijinsia. Katika wiki zilizopita, wanawake kadhaa, wakiwemo nyota wa Hollyowood
kama vile Gwyneth Paltrow wamejitokeza kusema kwamba Harvey Weinstein
aliwanyanyasa kijinsia, alijaribu kuwabaka ama aliwabaka. Weinstein ni mmiliki
wa kampuni ya filamu inayofanya vizuri sana nchini Marekani. Kampuni ya
Weinstein imetengeneza filamu maarufu kama Django Unchained, The Fighter na
Mandela: Long Walk to Freedom.
Weinstein alitaka kulala na Lupita Nyong'o
Reviewed by WANGOFIRA
on
21:20:00
Rating:
No comments: