SERIKALI ILITAFAKARI UPYA SUALA LA WAATHIRIKA WA KAGERA



                    Image result for thinking

Na, BARAKA NGOFIRA
0763580901

Septemba kumi mwaka huu tetemeko la ardhi lilikumba mikoa ya kanda ya ziwa huku janga kubwa likiwa limeachwa mkoani Kagera ambapo zaidi ya watu 17 walipoteza maisha papo hapo. Mbali na maafa hayo nyumba zaidi ya 2000 zilibomoka na kuharibiwa vibaya na kuwaacha wakazi wengi wa mkoa huo wakiwa hawana makazi.

Serikali na wadau mbalimbali walifanya kila liwezekanalo ili kupeleka misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula na mablanketi kwa waathirika ili waweze kujihifadhi. Huku serikali na wadau wengine wakikusanya nguvu ili kuwasaidia wanakagera kurudi kwenye hali yao waliyokuwa wameizoea kabla ya kukubwa na tetemeko la ardhi.

Miundombinu ikiwemo barabara, umeme, maji, shule na mingi iliharibiwa vibaya na tetemeko hilo. Shule kongwe za Ihungo na Nyakato ni moja ya taasisi ambazo ziliharibiwa vibaya sana na tetemeko la ardhi. Hali iliyosababibisha serikali kuwahamisha wanafunzi katika shule nyingine ili waweze kuendelea na masomo huku juhudi mbalimbali zikifanywa na serikali kurudisha shule hizo katika hali yake ya kawaida.

Salamu za pole kutoka kwa viongozi wan chi mbalimbali zilitumwa nchini, na msaada kidogo kama kifuta machozi kwa waathirika wa Kagera. Mashirika mbalimbali ya ndani ya nchi, taasisi za umma na watu binafsi walitoa misaada mbalimbali ili kuwasaidia waathirika wa tetemeko la Ardhi.

Mbali na juhudi zote hizo vyombo vya habari havikuwa nyuma kuuhabarisha umma kwa kila hatua iliyokuwa inaendelea juu ya makusanyo mbalimbali ya kuchangia waathirika wa tetemeko la Kagera. Viongozi mbalimbali hasa kutoka Ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa, walipewa muda mwingi na vyombo vya habari ili Kutoa tathmini yao na wapi walipofikia bila kusahau Kutoa msisitizo kwa raia watanzania na wadau mbalimbali wajitokeze kuchangia janga hili.

Kwa kufanya hivyo jamii na mashirika mbalimbali yalijitokeza kwa wingi huku baadhi ya wadau na wataalam wakiwemo wale kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam na vyuo mbalimbali walijitolea kufanya tathimini bure kabisa. Ambapo walitumia pesa zao wenyewe kutathimini na kutoa ushauri kwa serikali juu ya nini kifanyike ili kuirudisha Kagera na wakazi wake katika hali ambayo waliizoa.

Wakati hayo yote yakiendelea mwanzoni kabisa mwa zoezi hili kasoro iliingia kwa baadhi ya watumishi wa umma ambao hawakuwa waamini ambao walitaka janga hili kwa ajili ya kujishibisha. Ambapo baada ya kugundulika kufungua akaunti feki iliyokuwa na jina sawa na ile ya kupokea misaada ya Kagera walitumbuliwa mara moja na kupelekwa mahakamani ili kupambana na sheria.

Mbali na hao kutumbuliwa lawama nyingi zilisikika kuwalalamikia viongozi hao kugawa misaada hiyo kwa watu kulingana na itikadi za vyama. Ambapo wafuasi wa chama tawala walionekana kupewa upendeleo huku wenzao wa vyama vya upinzani wakibaki kula kwa macho. Jambo ambalo lilikemewa mara moja na viongozi wa ngazi ya juu ya serikali japo sina uhakika kama lilikisha au la!

Huku hayo yote yakiendelea serikali iliwatangazia wakazi wa Kagera kuwa wajijengee nyumba kwani serikali haina pesa za kujenga nyumba kwani tetemeko halikuletwa na serikali. Kauli hii iliibua maswali mengi miongoni mwa wadau na wakazi wa Kagera ambao walikuwa ni walengwa wa kauli hiyo. Lakini wajipa moyo na kupiga moyo konde na kuendelea na ujenzi japo wana hali mbaya. Ambapo mpaka leo wengi bado wanasubiri usiku uishe ndo waanze kujenga huku hawana mbele wala nyuma na kukaa pasipo kujua wapi wataanzia kujenga na chakula kubaki kukisikia  na kukiona kwa majirani.

Huku wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kujijenga kisaikolojia, mwanzoni mwa mwezi huu serikali kupitia mkuu wa mkoa huo ilipigilia msumari wa moto kwenye donda ambalo halijapona. Baada ya kuutangazia umma kuwa misaada iliyotolea na wadau na nchi wahisani zitatumika kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya mkoa huo. Ambapo alikaririwa akisema kuwa ni maamuzi ambayo yamefikiwa kwenye kikao cha kamati ya maafa ya Mkoa huo.

Lakini pia Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania alilibariki jambo hilo na kusema kuwa pesa hiyo ya maafa itatumika kujenga maghorofa mkoani humo ambayo anaamini kuwa hayatabomoka hata tetemeko la aina gani lipite. Jambo ambalo lilizua maswali mengi miongoni  mwa watanzania na kuzua gumzo kubwa mitandaoni ndani na nchi za jirani. Swali kubwa likiwa ni kwa nini serikali imeamua kuimarisha miundombinu ya mkoa huo huku watu wengi walioathirika wakiwa hawana chakula na malazi.

Ambapo wadau mbalimbali waliona ni uonevu na utapeli wa wazi wazi na kutojali wanyonge ambako kunafanywa na serikali ya Tanzania nchini ya Rais Magufuli. Itakumbukwa kuwa misaada yote iliamuliwa ikusanywe kwa mkuu wa mkoa wa Kagera ili iwe rahisi kugawanywa kwa wananchi lakini hali imekuwa tofauti na matarajio ya wengi. Kwani serikali imeamua kutumia nguvu na kuaamua kutumia nguvu na kubadilisha matumizi ya misaada ya kibinadamu kwenda kwenye matumizi ya maendeleo.

Jambo ambalo lingeweza kungoja bajeti ya mwaka mpya wa fedha au miradi ambao nchi wahisani wangeweza kusaidia nchi kama wanavyosaidia miradi mingine ya maendeleo. Kilichofanywa na serikali na sawa na msemo usemao aliyeshiba hamujui mwenye njaa, maana hata nguvu za kumsumbua hana.

Sikatai kuwa kilichofanywa na serikali ni kibaya la hasha bali naweza kusema ni kupungukiwa kwa ubinadamu na kuangalia ni nini kifanyike kwanza, maisha ya wakazi wanao lala nje na kukosa chakula au kuwajengea barabara na maghorofa ambayo wenye hela zao ndiyo watayafaidi na kupitisha magari yao. Huku maskini wanaotembea kwa miguu au wenye baiskeli zao wakiwa hawana mbele wala nyuma.

Hivyo basi ni vyema serikali ikatazama upya kuhusu misaada hiyo na kutoa misaada ya kibinadamu kwanza ikiwemo chakula na malazi kwa familia ambazo hazina uwezo au zina uwezo duni wa kipato cha kumudu kujenga nyumba na kununua chakula.

Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya kwanza ya mawasiliano kwa Umma katika Chuo kikuu cha Dar es salaam. Anapatikana kwa barua pepe ya barakangofira@gmail.com au simu 0763580901
SERIKALI ILITAFAKARI UPYA SUALA LA WAATHIRIKA WA KAGERA SERIKALI ILITAFAKARI UPYA SUALA LA WAATHIRIKA WA KAGERA Reviewed by WANGOFIRA on 05:42:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.