Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Apokea Zaidi Ya Sh. Bil. 1.4 Kwa Ajili Ya Maafa Ya Tetemeko La Kagera

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania kwa ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.

Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 hadi leo na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Akizungumza katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao jana Jumanne, 13 Septemba, 2016 Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango yao ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema tetemeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.

Alisema tetemeko hilo limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za sekondari za Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na tetemeko hilo.

“Serikali itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa na tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida,” alisema.

Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa kufanya thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Mawaziri wengine walioko mkoani Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Alisema Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB kwa ajili ya kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti hiyo ya Kamati ya Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.

Pia Waziri Mkuu aliwapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua kutoa posho zao za kikao cha jana kwa ajili ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango yao.

Wakati huo huo viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil wameahidi kujenga shule mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya miundombinu yake imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha siku 30.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk. Aziz Mlima
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Apokea Zaidi Ya Sh. Bil. 1.4 Kwa Ajili Ya Maafa Ya Tetemeko La Kagera Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Apokea Zaidi Ya Sh. Bil. 1.4 Kwa Ajili Ya Maafa Ya Tetemeko La Kagera Reviewed by WANGOFIRA on 20:51:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.