YAKITOKEA YA MOI NI SHULE GANI ITABAKI SALAMA?

            https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi-jWF1fPzyxh1afOBR7tG6sV2zuRB6GCAMIamrOiIl-NKsNFMFgpAT0G_gnkSy0brqKWDxCdiuTDJeeQvtvLZ87ijumztJia1li2E_Wj1bB6G2p_2dztcEHvgzXwQiJdZsAemZ6XDPyRg/s1600/549835_4891807486528_863702647_n.jpg

   
Na, BARAKA NGOFIRA
0763580901, 0716216249


Siku za nyuma ilikuwa rahisi sana kusikia wanafunzi wa shule fulani wamechoma shule au mabweni. Muda mwingine walipokuwa wakigoma tu kitu cha kwanza ambacho walikuwa wakikifanya ni uchomaji wa ofisi muhimu za shule ikiwemo stoo ya chakula, mabweni yao na hata ofisi za walimu.

Lakini kwa muda sasa matukio hayo yamekwisha na sasa hayasikiki tena na migomo mashuleni pia ni kama imekwisha kabisa. Katika matukio hayo yote ya migomo na uchomaji na uharibifu wa miundombinu ya shule kwa kiasi kikubwa hayakusababisha vifo vya wanafunzi au walimu katika shule hizo. Japo hayo yamepita na sasa hali ni shwari katika shule hizo lakini kuna umuhimu mkubwa wa viongozi waliopo kuhakikisha kuwa hali hizo hazijirudii tena.

Katika siku za hivi karibuni shule Moi sekondari iliyopo nchini Kenya iliungua na kusababisha vifo vya wanafunzi 9, ambao waliteketezwa vibaya kwa moto na kushindwa kufahamika hadi kwa vipimo vya DNA. Lakini pia wengi wao wakiwa wamejeruhiwa vibaya kwa kuuguzwa na moto. Tukio hili la ajabu na la kinyama kabisa kwa taarifa za awali linaonyeshwa kuwa lilifanywa na watoto wadogo tu tena mabinti wa takribani miaka 15 hivi. Ambao walichukua uamuzi huo baada ya kunyimwa ruhusa ya kwenda nyumbani kwa sababu walizojijua wao.

Ndipo wakachukua uamuzi huo wa kuteketeza shule na kusababisha madhira makubwa kiasi hicho. Nitumie fursa hii kuwapa pole wakenya wote kwa tukio hili lakini kwa namna ya pekee wazazi na ndugu na jamaa wa wanafunzi waliopoteza maisha katika tukio hilo. Lakini pia wale waliojeruhiwa Mwenyezi Mungu awajaalie ahueni ili waweze kupona haraka warejee katika masomo yao.

Kwa tukio hili lazima walimu na wamiliki wa shule wajitafakari waone je miundombinu ya shule zao ni rafiki kwa wanafunzi hasa majanga ya moto yakitokea. Maana kuna baadhi ya shule hasa katika mabweni wanafunzi wanapolala wanalazimika kuzima taa na kufunga Milango kwa kufuri kwa kuogopa wezi au wanafunzi kutoroka.

Jambo ambalo kwangu naliona ni mtazamo hasi kabisa, kwani kila ninapofikiria vifo vilivyotokea katika shule ya MOI roho yangu inajawa na ganzi, na kubaki na kujiuliza hadi hao wanafunzi 9 wanateketea kwa moto kiasi cha kushindwa kufahamika, wenzao walikuwa wapi kuwaokoa. Huku nikiyafikiria hayo najiuliza tena kwa nini kuna kiasi kikubwa cha wanafunzi katika bweni hilo walijeruhiwa?.

Jibu la haraka haraka linaloniijia akilini mwangu ni kuwa huenda bweni hilo lilikuwa limefungwa na hata njia mbadala za kujiokoa kama vile madirisha ya wazi au vioo ambayo ni rahisi kuvunjika na kuokoa maisha ya watu hayakuwepo. Badala yake madirisha yalikuwa ni ya nondo tena zile nzito zilizosokotwa kwa maua ndizo zilikuwepo katika bweni hilo.

Lakini pia vitanda vyao kwa kiasi kikubwa vilikuwa vya mbao, ambapo baada ya mwanafunzi huyo kuwasha moto kwenye kitanda chake ilikuwa rahisi kusambaa na kusababisha vifo na majeraha hayo ambayo hayatasahaurika.
Tuje kwenye shule zetu je mabweni yake yana miundombinu gani? Je madirisha yake ni ya namna gani? na vitanda je? Lakini mbali na hayo je ni shule ngapi ambazo katika mabweni ya wanafunzi wanalala huku mabweni yao yakiwa yamefungwa na funguo kulala nazo walezi wa wanafunzi hao au kiongozi wa bweni kwa kuhofia wezi na wanafunzi kutoroka?

Lakini ni shule ngapi ambazo kwa kuogopa gharama za umeme kuna ratiba kabisa za kuwasha na kuzima taa za mabwenini? Tukiisha jiuliza hayo yote tujitafakari je yakitokea kama yaliyotokea shule ya sekondari Moi ni shule gani itapona?

Ukiachilia mbali hayo pia kuna baadhi ya shule kwa tama za fedha hasa za binafsi na mashirika ya dini hubeba wanafunzi kupita kiasi. Na kuwalazimu wanafunzi kulala zaidi ya mmoja na wengine kulala madarasani au chini katika korido za mabweni hayo. Hivi kweli tutapona au ndiyo tutasubiri uchunguzi usiokuwa na mwisho na hatimaye inabaki historia?

Mbali na serikali kutaka kila shule au taasisi kuwa kuwa na vifaa vya kuzimia moto maarufu kama fire extinguisher lakini kuna shule hazina kabisa hata moja. Na kama zipo basi zimetunzwa katika ofisi ya mkuu wa shule au ofisi za walimu au katika maabara kama ipo. Na shule nyingine zipo tu kama mapambo maana hakuna hata mwanafunzi hata mmoja anayejua namna ya kuitumia endapo janga la moto likitokea.

Ni rai yangu kwa serikali na wadau wote wa elimu ikiwemo wamiliki wa shule kuhakikisha kuwa shule wanazozijenga zinakuwa na miundombinu rafiki ambayo majanga ya moto yatokeapo uokoaji unakuwa rahisi. Na hata kama yakitokea madhara basi yawe kidogo tu. Kwa mfano shule ya sekondari Lyamungo iliyopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro mbali na majaribio uliokuwa ukifanywa na wanafunzi wa shule hiyo lakini hawakufanikiwa hata siku moja zaidi ilikuwa wanachoma vitu vyao wenyewe na hivyo hasara ilikuwa kwa wahusika na si shule.

Pia ni lazima kwa shule zote nchini kuwa na ving’amuzi moto au fire alarm ili hata ikitoka itirafu ya umeme ambao unaweza kusababisha moto vile ving’ora vya tahadhari vitasaidia kuwaamsha hata wale walioko usingizini. Na kwa kufanya hivyo itasaidia kuokoa maisha ya wanafunzi katika shule zetu.

Na mwisho kuwepo kwa fire extinguisher kwa aina zake zote zilizowekwa maeneo ya wazi ikiambatana na  mafunzo kwa wanafunzi na walimu ili litokeapo tatizo la moto iwe rahisi kuzimwa na si kubaki kushaangaa tu na kurekodi kwa simu. Pia ni lazima serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kushirikiana na wakala wa usalama wa majengo kukagua upya shule zote ili kuona mapungufu yaliyopo na ili wamiliki wa shule wafanya marekebisho ya haraka.



YAKITOKEA YA MOI NI SHULE GANI ITABAKI SALAMA? YAKITOKEA YA MOI NI SHULE GANI ITABAKI SALAMA? Reviewed by WANGOFIRA on 20:58:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.