Askari wa JWTZ auawa kwa kuchomwa visu na vibaka

ASKARI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), MT 94293, aliyefahamika kwa jina la Tekeli Israel (29), ameuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka. 

Akithibitisha kuuawa kwa askari huyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa nne usiku, wakati marehemu, ambaye ni mkazi wa Mbaunda, alipokuwa akitoka kula chips. 

Alisema marehemu wakati akitoka baa ya Tarakea kwenda nyumbani kwake, alipofika eneo la Tarakea Super Car Wash, mtaa wa Simanjiro, kata ya Sombetini, asikia kelele za mtu akiomba msaada. 

Kamanda Mkumbo alisema mtu aliyekuwa anapiga kelele za kuomba msaada alifahamika kwa jina la Tumkislai Abdallah, ambaye alikuwa akiporwa simu ya kiganjani na vibaka. 

"Baada ya marehemu kufika eneo la tukio na kubaini kuwa ni vibaka, aliamua kupambana nao, lakini kwa bahati mbaya walimjeruhi kwa visu na mmoja wao alimchoma nacho kifuani,"alisema. 

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, wananchi kwa kushirikiana na polisi, walifanikiwa kumtia mbaroni kibaka mmoja, aliyefahamika kwa jina la Dickson Moses(19), maarufu kwa jina la 'Tukai', mkazi wa Olmatejoo, ambaye alimchoma kisu marehemu. 

Alisema baada ya mtuhumiwa kuhojiwa na polisi, aliwataja wenzake watatu, ambao walifanikiwa kutoroka na kwamba, polisi wanawasaka popote pale walipo. 

"Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha linawataka watuhumiwa watatu, ambao majina yao tunayo, waliokuwa na Tukai kwenye tukio la mauaji ya mwanajeshi huyo, kujisalimisha mara moja kwani mkono wa serikali ni mrefu utawatia nguvuni popote pale walipo," alisisitiza. 

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Ally Omaiy, alisema walimuona marehemu kwenye baa ya Tarakea, ambako alikula chispi kisha akaondoka. 

Alisema dakika chache baadaye, walisikia kelele za mtu anaomba msaada na baada ya kufika eneo la tukio, walimkuta marehemu akipambana na vibaka hao na ghafla walimuona ameanguka chini. 

Alisema baada ya kuanguka, vibaka hao walianza kukimbia, lakini wananchi kwa kushirikiana na madereva wa bodaboda, waliwakimbiza na kufanikiwa kumkamata mmoja wao. 

"Marehemu alipambana na vibaka hao kwa ajili ya kumsaidia Abdallah asiporwe simu, lakini kwa kuwa vibaka walikuwa wanne, walimzidi nguvu na mmoja alifanikiwa kumchoma marehemu kisu cha kifuani na kufariki dunia," alisema. 

Shuhuda mwingine, ambaye ni rafiki wa karibu wa marehemu (Jina linahifadhiwa), alisema marehemu alikuwa anajiandaa kwa ajili ya safari ya kwenda Darfur. 

"Marehemu alikuwa rafiki yangu wa karibu, tunaishi jirani hapa Mbauda, tulishirikiana kwa mambo mengi, licha ya mimi kuwa raia wa kawaida na aliniambia ameshakamilisha taratibu zote za kikosini na kwamba, alikuwa anajiandaa kwa ajili ya kwenda Darfur," alisema. 

Mwili wa marehemu Israel, umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hosptali ya Mkoa ya Mount Meru, ukisubiri taratibu za kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Mbeya kwa maziko.
Askari wa JWTZ auawa kwa kuchomwa visu na vibaka Askari wa JWTZ auawa kwa kuchomwa visu na vibaka Reviewed by WANGOFIRA on 01:25:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.