Kwa Wafipa marehemu amebadili tu mtindo wa maisha


LEO tunaendelea na mfululizo wa simulizi za tamaduni za kabila la Wafipa kama ilivyoandikwa na Januari Mbalamwezi kwenye kitabu chake cha Utamaduni wa Wafipa. Kwa Wafipa mtu akifa anakuwa ni kama mtu aliyepotea au aliyeondoka au amesafiri.
Mtu aliyesafiri au aliyetoka mahali fulani, mtu wa namna hiyo anakuwa bado yuko hai. Hivyo kwa Wafipa mtu aliyekufa kwa kweli anakuwa bado yuko hai ila amebadilisha mtindo wa kuishi.
Na hata kumtendea maiti Wafipa humtendea kama mtu aliye hai bado, wanapoosha maiti huchemsha maji ili maiti asione baridi na maji yenyewe lazima yawe ya moto kiasi ili maiti asiungue.
Maiti akishaogeshwa hupakwa mafuta na kuvalishwa nguo safi kama mtu aliye hai, hufanya hivyo ili maiti aonekane nadhifu kama mtu aliye hai. Katika kuzika kama hakuna sanduku, Wafipa humtengenezea ‘selelwa’ yaani ndani ya kaburi hutengeneza kama nyumba ndogo na hutandika kirago au majani ili marehemu alale mahali pazuri na kwenye mlango huziba kwa miti.
Zamani siku ya kwanza baada ya kuzika, marehemu alikokewa moto kule makaburini ili asione baridi.
Aliyezikwa husemekana kuwa amelala. Mtu anapokufa Kwa Wafipa waliweza kuona mtu kuwa katika kifo kwa kuangalia macho yake ambapo sehemu nyeupe ya macho hugeuka rangi kama ya kijivu ‘ikola iitwi’ au wengine hukodoa sana macho na wengine huwa na aibu.
Akinamama huwa ndio wa kwanza kushuhudia kuzaliwa kwa mtoto na ndio huwa wa kwanza kushuhudia kifo.
Kabla ya kuanza maombolezo, mtu anapokufa mtu wa kwanza kupelekewa taarifa huwa ni mkuu wa ukoo anayeitwa ‘umweenekashi’ kwa kuwa huyo ndio kiongozi wa kilio.
Kama mtu huyo hayupo kutokana na kuumwa, basi hutumwa mwakilishi wa kupeleka neno, na neno kubwa ambalo husubiriwa ni nani anayerithi na hapo watu wote wa upande wa baba au mama hupewa taarifa. Maziko Endapo kifo kimetokea usiku au asubuhi, maziko hufanyika siku hiyo hiyo.
Mchakato wa maziko huanza kwa kuchimba kaburi. Zamani kaburi lilichimbwa na watu wawili na ndio waliobeba maiti na kufukia, baada ya hapo walipewa kuku “i’ chipulupuso” maana ni kifutajasho. Na baada ya kutoka kwenye maziko walinawa dawa ili wasivimbe mwili. Kabla ya kuchimba kaburi walihakikisha mazishi yanafanyika kwani kwa Wafipa ilikuwa ni mwiko kaburi kulala wazi na ikitokea hivyo waliweka kitu fulani mfano mgomba wa ndizi.
Mtu alivyozikwa Kwa Wafipa wakati wa kuzika, marehemu alilazwa kwa ubavu wa kushoto ili ‘apaape i’ ndaaka’ maana yake abebe jua mgongoni. Wafipa wanaamini jua ni Mungu mwenye uwezo wa kuleta uzima. Kwa watu waliooa au kuolewa, baada ya marehemu kushushwa kaburini, walifanya taratibu za kumuaga mwenzake ‘mwidu’.
Kama mwanamume ndiye aliyefiwa, alimwagiwa maji baada ya kufukia kaburi kama alama ya kumsafisha na ‘kiswa’ yaani balaa.
Baada ya kufukia kaburi nusu, watoto wa marehemu (walioruhusiwa ni watoto wakubwa pekee) walimuaga baba au mama pale kaburini kwa kusimama kaburi likiwa nyuma yao. Baada ya kuambiwa waseme maneno ya kuaga waliondoka kurudi nyumbani bila kuangalia nyuma.
Baada ya hapo kaburi lilifunikwa na kufukiwa lote na baadaye alipanda majani kwenye pembe ya kaburi ili fisi wasije kuchimbua maiti (hii haifanywi siku hizi).
Kwa sasa wanapanda miti kama alama ya kutambulisha marehemu wao walipolala. Zamani kama marehemu alikuwa mwanamume, majembe yaliyotumika kumzikia yaliachwa juu ya kaburi kwa sababu Wafipa wote walikuwa wakulima na kama marehemu alikuwa ‘silungu’ mfua chuma aliwekewa upande wa kichwa chuma.
Baada ya maziko Baada ya maziko kama mfiwa alikuwa mwanamume, alimwagiwa maji palepale kaburini na kama ni mwanamke basi alimwagiwa maji baada ya kurudi kwenye nyumba ya maombolezo.
Wakirudi nyumbani baada ya maziko, mama aliyefiwa na baba haingii nyumbani na badala yake wifi wa mama mfiwa hupewa kibuyu cha kunywea maji kikiwa na mbegu za kila aina ambazo marehemu alikuwa ikizipanda.
Mama mfiwa husimama kwenye kibambaza cha mlango akiwa amejifunika blangeti au nguo nyingine. Wifi humwagiwa majina na mbegu na baada ya hapo humvuta mfiwa kinyume nyume na kumwambia hana mume tena.
Kibuyu kilichovunjwa ni alama ya mume na zile mbegu ni alama ya kilimo na mazao aliyokuwa anazalisha. Baada ya kuingia ndani, mama mfiwa alitandika majani na kukaa hapo wakati wote wa kilio (siku hizi hawatandiki majani lakini mfiwa anakaa hapo mpaka kilio kiishe).
Kwa upande wa mwanamume yeye alitandikiwa majani nje ya nyumba karibu na mlango, alikaa pale pale mpaka mwisho wa kilio.
Pia baada ya maziko (zamani hadi sasa) ni lazima kunawa dawa hata kwa watoto na ndugu wengine wa marehemu, dawa hizi zilikuwa ni za kujizindika au kuwapatia chakula kingi na kuzuia kama waliotendewa mabaya yasiwapate.
Na inaaminika mpaka sasa kuwa kama hawatanawa dawa wanaweza kufa kumfuata marehemu.
Kwa Wafipa marehemu amebadili tu mtindo wa maisha Kwa Wafipa marehemu amebadili tu mtindo wa maisha Reviewed by WANGOFIRA on 20:23:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.