Utashi wakwamisha maendeleo ya sayansi


NA ANASTAZIA ANYIMIKE

MBALI na tatizo la kiuchumi, utashi wa wanasiasa kutotilia mkazo asilimia moja ya Pato la Taifa kutumika kwenye tafiti na ubunifu ndio moja ya sababu ya kushindwa kuwaendeleza wanasayansi hapa nchini.


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangala wakati wa kufunga mkutano wa siku tatu wa wanasayansi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema serikali inafahamu changamoto nyingi ambazo zinawakabili wanasayansi kama changamoto ya fedha, fursa za kujiendeleza, uchumi mdogo na utashi wa kisiasa.

“Chanzo cha matatizo tuliyonayo kinaeleweka kuwa ni uchumi wetu kuwa mdogo, lakini pia utashi wa sisi wanasiasa, kwa sababu kama tungeamua kutenga walau asilimia moja ya GDP kama ilivyoelezwa miaka kadhaa iliyopita nina uhakika tungeweza kuendeleza kwa kiasi kikubwa, wanasayansi wa ndani kwa kutumia fedha zetu,” alisema.

Dk Kigwangala aliongeza kuwa, “pia tungeweza, kuwekeza fedha zetu kwenye kufanya tafiti, ambazo zinalenga kutatua matatizo yanayotusibu kila siku, kuliko tafiti ambazo zinatokana na fedha za wafadhili jambo ambazo masharti ni kufanya utafiti kulingana na malengo ya watoa fedha.”

Aidha alisema wataendelea kufanywa ushawishi ili itengwe bajeti ya kutosha, kwa ajili wanasayansi wa ndani ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanya tafiti na ubunifu kwani Tanzania ya kesho itategemea sayansi na ufumbuzi.

“Niwahakikishie kuwa tunathamini kazi mnayofanya wanasayansi na tutaendelea kuwaunga mkono kwa kufanya jitihada mbalimbali ndani ya serikali,” alisema.

Dk Kigwangala alisema mapendekezo sita yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), yatafanyiwa kazi kwa sababu serikali inaamini kwenye kupanga mipango na kutunga sera, ambazo zinatokana na ushahidi wa kiutafiti na mijadala ya kisayansi.

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mwele Malecela alisema kongamano hilo lililoshirikisha washiriki 320, limekuja na mapendekezo kadhaa ambayo ni kuanzishwa kwa kituo cha kupambana na magonjwa ya virusi yanayoenezwa na mbu, kuimarisha maabara katika afya msingi, ikiwa ni njia ya kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema pia mkutano huo umependekeza umuhimu wa kuwapo juhudi za makusudi za kuongeza utafiti na uvumbuzi miongoni mwa watanzania, na pia kutolewa elimu sahihi ya namna ya kutuza, kuandaa mazao na chakula na namna ya kulisha.

Utashi wakwamisha maendeleo ya sayansi Utashi wakwamisha maendeleo ya sayansi Reviewed by WANGOFIRA on 13:24:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.