Mfalme wa Morocco Kupokewa kwa ‘Mabango’ Leo Hapa Nchini

Wakati Mfalme wa Morocco, Mohamed VI akitarajiwa kuwasili leo nchini kwa ziara ya kikazi, huenda akapokewa kwa mabango baada ya vijana wanaounda kamati ya mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi (TASSC) kujipanga kufanya hivyo kushinikiza nchi hiyo kuacha kuitawala kwa mabavu Sahara Magharibi. 

Vijana hao wamefikia uamuzi huo kutokana na kile walichodai kusikitishwa kwao na kitendo cha Morocco kuendelea kuitawala kwa mabavu nchi ya Sahara Magharibi na kupuuza wito wa Umoja wa Mataifa (UN) unaoitaka kuipa uhuru nchi hiyo. 

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia msemaji wake, Hassan Abass imesema ujio huo ni muhimu kwa uhusiano wa kidiplomasia na uchumi. 

“Serikali ilishaeleza msimamo wake, kuna uhusiano wa aina nyingi, ujio huu ni muhimu kwa uhusiano wa kidemokrasia na uchumi kama hisia zitawatuma kufanya hivyo, wanapaswa kufuata sheria,” alisema Abass.

 Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa TASSC, Alphonce Lusako alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili Morocco iiache huru Sahara Magharibi lakini watawala wa nchi hiyo wamekuwa wagumu kuruhusu hilo. 

Lusako alieleza kuwa TASSC inafahamu fika kwamba Mfalme Mohamed VI amekuwa akifanya ziara katika mataifa mbalimbali akijaribu kutafuta kuungwa mkono ili Morocco iendelee kuitawala Sahara Magharibi. 

Alisema Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoitambua Sahara Magharibi inapaswa kumuonyesha wazi Mfalme Mohamed VI kuwa haiungi mkono utawala wa kimabavu.

 “Tunamtaka Mfalme wa Morocco kuacha mara moja vitendo vya kibeberu vya kuikalia Sahara Magharibi sambamba na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na wanaharakati wanaoshikiliwa magerezani katika maeneo yanayokaliwa kimabavu. 

"Ni aibu kwa nchi moja ya Kiafrika kuitawala nchi nyingine: Tunaunga mkono msimamo wa Tanzania wa kuendelea kuitambua na kuiunga mkono Sahara Magharibi kwenye vyombo vya kimataifa na tunasisitiza isiyumbishwe katika msimamo huo, ” alisema.

 Katibu wa TASSC, Jasper Hassan alisema tangu kamati hiyo ianzishwe mwaka jana imekuwa ikifanya harakati mbalimbali ikiwamo mihadhara ya wazi inayolenga kuisukuma Morocco kuacha kuitawala Sahara Magharibi.

 “Jitihada zilianza muda mrefu ila mwaka jana ndiyo vijana tukaona tuingilie kati tukiwa kama Waafrika, tunapinga kila aina ya unyonyaji tunataka Sahara Magharibi iwe huru,” alisema Hassan. 

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema ziara ya kiongozi huyo itakuwa na manufaa kwa nchi, kwani akiwa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli watasaini makubaliano 11 ya ushirikiano katika sekta za kilimo, gesi, mafuta, Reli ya Liganga na Mchuchuma na sekta ya utalii.
Mfalme wa Morocco Kupokewa kwa ‘Mabango’ Leo Hapa Nchini Mfalme wa Morocco Kupokewa kwa ‘Mabango’ Leo Hapa Nchini Reviewed by WANGOFIRA on 23:46:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.