Kafulila Akwaa kisiki cha mwisho mahakamani.......Ubunge wampita Kushoto baada ya Mahakama ya Rufaa Kutupilia Mbali Maombi Yake


Hatimaye mbio za David Kafulila kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa Kigoma Kusini ya Oktoba mwaka jana uliompa ushindi Husna Mwilima (CCM) zimefika ukingongoni baada ya mahakama ya rufaa kutupilia mbali maombi yake.

Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa waliokaa mjini Tabora, jana lilitoa maamuzi yake kuhusu rufaa ya Kafulila na kueleza kuwa wameyatupilia mbali maombi hayo kwakuwa yamekosa nguvu yenye uhalali wa Kisheria.

Aidha, Mahakama hiyo ya Rufaa imemtaka Kafulila ambaye hakuhudhuria mahakamani hapo, kulipa gharama zote za shauri hilo la madai namba 212 la mwaka 2016.

Akizungumza baada ya maamuzi hayo ya Mahakama ya Rufaa, Mbunge wa Kigoma Kusini, Mwilima alisema Kafulila alijua kuwa hakuwa na madai yoyote mahakamani na kwamba alicholenga ni kumsumbua ili akose muda wa kuwatumikia wananchi wake.

“Kafulila alijua fika kuwa hakuna kesi ya yeye kukata rufaa. Lakini alikata rufaa kunisumbua ili nikose muda wa kuwatumikia wananchi waliniingiza bungeni,” alisema Mwilima.

Kafulila alifungua shauri la madai namba 2 la mwaka 2015 katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, akipinga ushindi wa Mwilima. Katika shauri hilo, Kafulila aliwalalamikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Msimamizi wa uchaguzi na Husna Mwilima.

Mahakama Kuu iliyatupilia mbali maombi ya Kafulila ya kutaka kutengua ubunge wa Mwilima ndipo Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kusini alipoamua kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ambayo ni Mahakama ya juu zaidi nchini.

Kesi hiyo iliyovuta umakini wa wananchi wengi jimboni humo na huenda ndio kesi ya uchaguzi iliyovuta watu wengi zaidi tangu kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka jana, imefikia ukingoni kwa kuhalalisha ubunge wa Mwilima.
Kafulila Akwaa kisiki cha mwisho mahakamani.......Ubunge wampita Kushoto baada ya Mahakama ya Rufaa Kutupilia Mbali Maombi Yake Kafulila Akwaa kisiki cha mwisho mahakamani.......Ubunge wampita Kushoto baada ya Mahakama ya Rufaa Kutupilia Mbali Maombi Yake Reviewed by WANGOFIRA on 22:58:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.