FIKRA ANGAVU; Magufuli usihamie Dodoma kabla hujatembelea Bahi



NA GORDON KALULUNGA

MHESHIMIWA Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, ameutangazia ulimwengu kuwa anakusudia kuhamia mkoani Dodoma ili kutimiliza kauli ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipoutangaza mkoa huo kuwa ndiyo makao makuu ya Chama na Serikali mwaka 1973.

Uamuzi huo baadhi waliushangilia na baadhi kuutilia mashaka kwasababu mbalimbali zikiwemo sababu za kiuchumi, kiusalama na kimazoea.

Fikra zangu Angavu zimeona zimpe mtihani Rais Magufuli. Tena mtihani wa kuchagua kati ya A. au B.

Sehemu (A) ni kwamba Rais Magufuli achague kutohamia Dodoma kwa usalama wa Afya za viongozi na wananchi kwa ujumla na sehemu (B) ni kwamba asihamie mpaka hapo atakapotoa tamko la kufuta vibali vya uchimbaji wa madini hatari aina ya URANI yaliyopo katika wilaya ya Bahi mkoani humo.


Madini haya yakichimbwa, vumbi lake lenye gesi ya radon litasafiri na kuleta madhara  makubwa Dodoma ambapo kwa taarifa za kitaalamu, gesi ya radon husafiri kilomita zaidi ya 59 na umbali wa kutoka Bahi mpaka Dodoma mjini ni mfupi.
 Bahi District


District
Bahi District's location within Dodoma Region.
Bahi District's location within Dodoma Region.
Coordinates: 05°57′10″S 35°18′43″ECoordinates05°57′10″S 35°18′43″E
CountryTanzania
RegionDodoma Region
Population (2012)
 • Total221,645


Katika mtihani huo binafsi naanza kumwonesha jibu moja wapo ambalo linaweza kumfaa yeye pamoja na Taifa kwa ujumla kwamba ni vema kuchagua kutoa tamko la kupiga marufuku uchumbani wa madini hayo.

Sababu moja wapo ni kwamba vumbi la urani liko katika mfumo wa gesi inayoitwa RADON 222, lenye mionzi hatari inayosababisha  kansa kwa wanyama na binadamu, linaua  mimea  na lina uwezo mkubwa wa kusafiri kwa njia ya upepo na hivyo kuna uwezakano mkubwa kudhuru wakazi wa makao yetu hayo makuu ya nchi yetu.
Fikra Angavu kutoka hapa Nyikani haielezi haya kwasababu ya Rais Dkt. Magufuli kukusudia kuhamia Dodoma, la hasha, bali madhara ya madini hayo yanaweza kuwakumba hata wananchi wa kawaida endapo tu yakiruhusiwa kuchimbwa hata kama Rais hatohamia huko.

Kwa taarifa za Nyikani ni kwamba, kuna kampuni moja iliyokuwa na nia ya kuchimba madini ya hayo kule Bahi inayoitwa URANEX kutoka nchini Australia. Inasemekana kuwa kampuni hiyo ilijitoa  katika sekta  hiyo ikidai kuwa imegundua madini ya graphite.

Kampuni hiyo ilibadilisha jina lake na sasa inajulikana kwa jina la
“Magnis Resources.” Kampuni nyingine ambayo imekuwa ikijihusisha na
utafutaji wa urani katika eneo hilo hilo ni  MANTRA ambayo  pia
inatoka nchini Australia. Itakumbukwa kuwa ni kampuni hii hii ya
MANTRA iliyogundua urani katika eneo la Mto Mkuju ndani ya hifadhi ya Pori la Selous na baadaye kuiuzia kampuni nyingine ya uchimbaji wa
urani kutoka nchini Urusi.


Kwa mfano, kampuni ya  MANTRA kutoka  Australia ndiyo inayodai
kugundua  urani katika eneo la Mto Mkuju ndani ya Hifadhi ya Pori la
Selous. Kama wote tunavyofahamu, pori hili ni Eneo la Urithi wa Dunia uliotangazwa na UNESCO mwaka 1982.

Hata hivyo, mwaka 2014  shirika la UNESCO  lilitahadharisha
kuwa kuna hatari ya wanyama kutoweka na hadhi ya hifadhi hiyo kushuka kutokana na ongezeko la kutisha la matukio ya ujangili.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, lilionyesha kuwa  wakati fulani
hifadhi ya Selous iliongoza kwa kuwa na tembo wengi zaidi duniani. Kwa mfano, katika mwaka 1976, Pori la Akiba la  Selous lilikuwa na tembo 110,000.

Hata hivyo, kutokana na ujangili kupamba moto, ilipofika mwaka 2014,
idadi ya tembo katika pori hilo ilipungua   kwa  karibu  asilimia 90
na kufikia tembo 15,000! Hivi sasa katika eneo hilo, tayari kuna
kampuni kutoka Urusi ambayo ina mpango wa kuanza kuchimba urani katika eneo la Mto Mkuju.



Ikiwa uchimbaji utaanza,ni wazi utakuwa na changamoto kubwa kwa pori hilo . Kwa kifupi, kama ilivyo hatari kwa Bahi, uchimbaji wa urani
katika Mto Mkuju utakuwa ni hatari kwa watu, wanyama na mimea katika Pori la Akiba la Selous.

Pia, kutokana na uwepo wa maeneo makubwa yenye maji chini ya ardhi, maji ambayo ni urithi mkubwa kwa Tanzania, maji hayo yanaweza kuharibiwa ikiwa uchimbaji huo wa urani utaruhusiwa.

Sanjari na hayo, taarifa za utafiti wa uchumi zinabainisha wazi kuwa hakuna nchi ambayo imeweza kuendelea kutokana na uchimbaji wa madini. Madalali pamoja na matajiri wao wanawekeza katika kampuni wakijifanya wanafanya utafiti wa madini wakati ukweli wanaujua nyuma ya pazia. Madini hayaozi.

Taarifa za kisayansi kutoka Ujerumani, kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, imetumia zaidi ya Euro bilioni saba kusafisha eneo la machimbo ya urani  katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki.

Machimbo hayo ya urani yalikuwa yakichimbwa na kampuni ya Kirusi na
baada ya Ujerumani Mashariki na Magharibi kuungana Oktoba 3, 1990,
kazi ya kusafisha ardhi ya maeneo ya machimbo hayo ilianza.

Hata hivyo wataalamu wa urani wanasema mionzi ya urani bado iko ijapokuwa imepunguzwa sana.Ikumbukwe kuwa suala hili linahusu nchi tajiri, yenye teknolojia na sayansi ya juu sana hapa duniani tofauti na Tanzania.

Kwasababu Rais, Dkt. Magufuli ni mtaalam wa masuala ya sayansi naamini atakuwa ameisikia na kuielewa sauti hii kutoka hapa Nyikani.
FIKRA ANGAVU; Magufuli usihamie Dodoma kabla hujatembelea Bahi  FIKRA ANGAVU; Magufuli usihamie Dodoma kabla hujatembelea Bahi Reviewed by WANGOFIRA on 13:36:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.