Shirika la SEMA lapongezwa kwa kuunga mkono juhudi za JPM Singida


  
Serikali mkoani Singida,imelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha sekta za elimu na afya.

Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na katibu tawala mkoa wa Singida,Dk.Angelina Lutambi,wakati akizungumza kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo ya siku 14 ya huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga.Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wahudumu wa afya kutoka wilaya ya Iramba na manispaa ya Singida,yapo chini ya mradi wa ‘Mwanzo Mwema’.

Alisema SEMA kwa ushirikiano na shirika la WaterAid Tanzania,Amref na RFSU,imeisaidia serikali kujenga na kukarabati majengo ya kutolea huduma za afya na shule na miundo mbinu ya maji.

“Kwa haya mafunzo ya huduma za dharura za uzazi na mtoto wachanga,ni muhimu sana kuliko jambo lo lote,kwa vile yanalenga kulinda uhai wa mwanadamu.Kwa hiyo nawapongeza na kuwashukuru kwa hili pia”,alisema Dk.Lutambi.

Akisisitiza,alisema mafunzo hayo yatakuwa na tija zaidi, iwapo kila halmashauri za wilaya na manispaa,zitahakikisha vifaa muhimu vya huduma za dharula za uzazi na watoto wachanga, vinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

Aidha,katibu tawala huyo ametoa wito kwa serikali za vijiji, mitaa, kata na halmashauri za wilaya zote,zisimamie masuala ya afya ya mama na mtoto, na kuifanya kuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vyote vya kisheria. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ushiriki wa wanaume katika masuala ya uzazi.

Katika hatua nyingine,Dk.Lutambi alitumia fursa hiyo kuliomba shirika la SEMA, WaterAid Tanzania, Amref na RFSU, kuangalia uwezekano wa kupanua mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ ufike katika wilaya zingine.

“Nawaomba mpanue huduma zenu….. hasa haya mafunzo ya huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga.Mafunzo haya ni kipengele muhimu sana katika kupunguza vifo vya mama na watoto.Naahidi mkoa utaendelea kutoa ushirikiano kwenu na kuwapatia kila msaada utakaohitajika,” alisema katibu tawala huyo.

Awali meneja mkuu wa shirika la SEMA, Ivo Manyaku,alisema lengo la mafunzo hayo, ni utekelezaji wa lengo la taifa la kupunguza vifo vya wanawake na watoto wachanga vitokanavyo na uzazi.

“Hii ikiwa ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa malengo ya milenia (MDG 4&5), ambapo inazungumzia malengo ya kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano,mwaka moja na wale wachanga walio chini ya mwezi moja,” alisema Manyaku.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo,Dk.Ridhiwan Kiluvia,alitaja baada ya mada zilizotolewa kwenye mafunzo hayo, kuwa ni huduma muhimu kwa mama na mtoto (uzazi salama)uzazi pingamizi, utokaji wa damu nyingi wakati wa ujifungua na baada ya kujifungua na kifafa cha mimba.

Na Nathaniel Limu, Singida
Shirika la SEMA lapongezwa kwa kuunga mkono juhudi za JPM Singida Shirika la SEMA lapongezwa kwa kuunga mkono juhudi za JPM Singida Reviewed by WANGOFIRA on 11:52:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.