Salum Mwalimu na Wafuasi 18 wa Chadema wapata dhamana

Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu imewaachia kwa dhamana Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu na wafuasi wengine 18 wa chama hicho baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya siku 12.

Kiongozi huyo wa Chadema na wafuasi hao 18 walikuwa wakishikiliwa katika mahabusu za jeshi la polisi kwa tuhuma za kuandaa na kuhamasisha maandamano na mikutano ya Oparesheni ya chama hicho iliyopewa jina la UKUTA, ambayo ilipigwa marufuku na jeshi hilo.

Walifanikiwa kupata dhamana baada ya Hakimu wa Mahakama hiyo kueleza kuwa ameridhia hoja za upande wa utetezi baada ya kusikiliza pande zote mbili na kubaini mapungufu kwenye maombi ya upande wa mashtaka.

Awali, Mwendesha mashtaka aliitaka Mahakama hiyo kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa madai kuwa endapo wataachiwa wataendelea kufanya kosa hilo.

Hata hivyo, Hakimu alitupilia mbali maombi hayo akieleza kuwa wameshindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa endapo washtakiwa hao wataachiwa watafanya tena kosa hilo.

Pia, Hakimu alieleza kukubaliana na hoja ya washtakiwa hao kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka ilikuwa na mapungufu ya kisheria.

“Ninakubaliana na upande wa utetezi kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa ina mapungufu ya kisheria,” alisema Hakimu baada kupitia na kugundua kuwa aliyesaini hati hiyo sio anayeonekana kuitoa.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana kwa kuwasilisha wadhamini wawili kila mmoja ambaye ataweka dhamana ya shilingi milioni 3.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria mahakamani hapo na kuondoka na Salum na wafuasi hao ambao walifikishwa mahakamani hapo awali chini ya ulinzi mkali. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4 mwaka huu
Salum Mwalimu na Wafuasi 18 wa Chadema wapata dhamana Salum Mwalimu na Wafuasi 18 wa Chadema wapata dhamana Reviewed by WANGOFIRA on 22:02:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.