Obama afuta mkutano na kiongozi wa Ufilipino kwa kuitwa "mwana wa kahaba"


Rodrigo Duterte akiwasili Laos kwa mkutano mkuu wa Asean

Rais wa Marekani Barack Obama amevunja mkutano wake na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, ambaye awali alikuwa amemwita "mwana wa kahaba".

Bw Obama awali alikuwa amesema kwamba angemuuliza kiongozi huyo maswali kuhusiana na mauaji ya kiholela ya watu wanaotuhumiwa kuhusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya Ufilipino.
Lakini Bw Duterte, ambaye ameunga mkono mauaji hayo, alisema iwapo hilo lingefanyika: "Putang ina (mwana wa kahaba) nitakutusi katika mkutano huo."


Maafisa wa Obama wamesema badala yake kiongozi huyo sasa atakutana na rais wa Korea Kusini.


Rodrigo Duterte akiwasili Laos kwa mkutano mkuu wa Asean


Msemaji wa baraza la taifa la usalama Marekani Ned Price ameambia wanahabari kwamba Bw Obama atakutana na Bi Park Geun-hye katika mkutano wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa bara Asia (Asean) mjini Laos, ambapo viongozi wamekusanyika kwa mkutano mkuu.
Bw Obama, aliyetua Laos baada ya kuhudhuria mkutano wa G20 mjini Hangzhou, China, alitarajiwa kuuliza maswali kuhusu ukiukwaji wa haki za kibinadamu Ufilipino.

Lakini akiongea mjini Manila Jumatatu kabla ya kuondoka kuelekea Laos, Bw Duterte alishutumu hilo na kusema ni "kukosa adabu" na akamtusi rais huyo wa Marekani. Aliongeza kwamba: "Tutagaragazana matopeni kama nguruwe iwapo utafanya hilo."
Kisha, alizungumzia kampeni ya kukabiliana na walanguzi wa dawa za kulevya ambapo washukiwa 2,400, wakijumuisha walanguzi na watumizi, wameuawa nchini Ufilipino tangu achukue mamlaka mwezi Juni.
"Kampeni dhidi ya dawa za kulevya itaendelea. Wengi watafariki, wengi watauawa hadi tuangamize mlanguzi wa mwisho na kumuondoa kutoka barabarani ... hadi mtengenezaji wa mwisho wa dawa hizi auawe, tutaendelea."
Bw Obama awali alidunisha matusi hayo na kusema aliwaomba maafisa wake kuchunguza iwapo huu ni wakati mwafaka wa kuwa na mashauriano ya kufana.
Baadaye, maafisa wake walivunjilia mbali mkutano huo.
Ziara ya mwisho ya Obama bara Asia akiwa kama rais imejaa vioja. Alipowasili Uchina, alijipata kwenye mzozo wa itifaki kati ya maafisa wa Marekani na Uchina ambapo alikosa kuwekewa zulia jekundu.

Matusi

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Duterte kutumia lugha chafu kuwarejelea viongozi mashuhuri.
Alimwita Papa Francis "mwana wa kahaba", waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Keryy "mwendawazimu" na majuzi alimweleza balozi wa Marekani nchini Ufilipino kama "mpenzi wa jinsia moja ambaye ni mwana wa kahaba".

Wachanganuzi wanasema tabia ya Duterte inamfanya kupendwa sana nyumbani lakini huenda akatengwa na jamii ya kimataifa

Wachanganuzi wanasema tabia ya Duterte inamfanya kupendwa sana nyumbani lakini huenda akatengwa na jamii ya kimataifa.
Umoja wa Mataifa tayari umeshutumu ukiukwaji wa haki za kibinadamu nchini humo.
Mwezi Agosti, wataalamu wawili wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa walisema agizo la Bw Duterte kwa polisi na umma kuwaua washukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya ni "uchochezi wa ghasia na mauaji, na ni uhalifu chini ya sheria za kimataifa."


BBC

Obama afuta mkutano na kiongozi wa Ufilipino kwa kuitwa "mwana wa kahaba" Obama afuta mkutano na kiongozi wa Ufilipino kwa kuitwa "mwana wa kahaba" Reviewed by WANGOFIRA on 22:09:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.