BARUA YANGU KWA RAIS WA JAMHURI TUKUFU YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DR. JOHN POMBE MAGUFULI.
Rais mtukufu wangu popote ulipo salaam,
Ni matumaini yangu kuwa haujambo na unaendelea na
shughuli hadhimu ya kutuletea maendeleo wananchi wa Tanzania na Afrika kwa
ujumla.
Nianze barua yangu kwa kukupongeza kwa jitihada zako
zilizotukuka za kuleta maendeleo ndani ya taifa letu ambalo lilikuwa limefanywa
shamba la la bibi. Ambalo kila mtu mwenye nguvu alikuwa na uwezo wa kufanya
lolote aliloona linampendeza kufanya. Hata kama likiwa baya kiasi gani.
Nipongeze jitihada zako za utumbuaji majipu
unaoendelea nao ili kutengeneza taifa lenye nidhamu na uzalendo wa kazi na
utaifa. Na kujenga utaifa kwanza ubinafsi na starehe baadaye. Hili ndilo
tulilolitaka watanzania.
Pamoja na yote hayo nikupongeze pia kwa juhudi zako
za kuinua elimu ya mtanzania kupitia sera ya elimu bure ambapo imempa fursa
mtoto wa yule maskini na mkulima kuisoma bila shida. Lakini pia ukahakikisha
watoto hao hawapati shida ya kukaa kwenye mawe na sakafuni bali wanakaa kwenye
madawati, tena yenye ubora wa hali ya juu. Kwa hapo Mtukufu rais nakupongeza
sana.
Kwenye sekta ya afya pia ni wazi siku chache tu
baada ya kuingia madarakani ulifanya mabadiliko makubwa kwa kuhakikisha
hospitali zetu zinakuwa kwenye ubora. Na kununua vitanda ambapo haapo awali
wagonjwa na mama zetu walioenda kujifungua walikuwa wanalala chini wengine
wakilala zaidi ya watu watatu kwenye kitanda kimoja.
Mtukufu rais kwa heshima kubwa uliyonayo kwa
watanzania tunakupenda sana, kwani tunaamini unaweza kutuvusha kambo hii ambayo
ni ngumu inahitaji maombi na juhudi nyingi, ambazo kwa uwezo wa kibinadamu si
rahisi kuifikia.
Natamani kuiona Tanzania ya viwanda uliyotuahidi
ambayo naamini muda si mrefu vitaanza kujengwa, na kuifanya nchi yetu kuwa
yenye uchumi wa kati . na kuwa nchi ya kuvutia wawekezaji wakubwa na wadogo
kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini kwetu. Ili tuendelee kiuchumi
na kuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa makubwa na madogo dunia.
Kwani nauchukia umaskini na wewew pia ni imani yangu
kuwa unauchukia umaskini na ndiyo maana kila kukicha kwenye hotuba yako
unashangaa kuhusu rasilimali na madini yote tuliyonayo lakini bado ni maskini.
Mimi sijui lakini naamini kama mkuu wan chi unaweza ukawa na majibu ya kwa nini
bado tu maskini .
Kwa maana unauchukia umaskini ni imani yangu ya kuwa
muda si mrefu tanzani nchi yetu itakuwa tajiri kufautana na mikakati yako
thabiti ya kuinua uchumi na kujenga nidhamu ya kazi.
Sitosahau juhudi unazozifanya kupambana na rushwa na
ufisadi, ili kujenga taifa la watu waadilifu na wenye utu kwanza, hapa umeanzisha
mahakama ya mafisadi. Ambayo ikianza kazi itawafunga wale waliotuhujumu na
kujineemesha, kwa rasilimali za watanzania maskini ambao babu zetu walipigana
kuikomboa nchi hii kutoka mikononi mwa wakoloni.
Ambapo walilifanya kuwa taifa huru chini ya Hayati baba wa Taifa
mwalimu Nyerere Mungu amupumzishe mahala pema, maana daima tutamkumbuka kwa
harakati zake na mapenzi yake kwa taifa letu la Tanzania. Ambapo jina lake
kamwe halitasahaulika mioyoni mwa watanzani na duniani kiujumla.
Mtukufu rais pamoja na juhudi zako hizo lakini leo
imenibidi nikuandikie barua hii. Ambayo
ni kutoka chini ya uvungu wa moyo wangu, kukushauri juu ya masuala machache
ambayo ninaamini yanaweza kutuvusha ikiwa utayatilia maanani na kuyafanyia kazi
japo kwa kidogo.
Kusema kweli rais wangu imenibidi kukuandikia barua
hii ambayo naamini hata kama hautoisoma kwa kuipuuza au kuitilia maanani
naamini wasaidizi wako, au watakayoisoma watakufikishia ujumbe. Japo wengine
waweza kuogopa kwa kukufikishia kwa kuogopa kutumbulia. Lakini binafsi imenibidi
nikuandikie barua hii kama mwananchi wako na mzalendo wa nchi yangu ya Tanzania
ambapo popote nikienda najivunia utanzania wangu.
Tangu uingie madarakani novemba 5, 2015 nimekuwa
nikifuatilia hotuba zako ambazo binafsi nimekuwa nikizifurahia sana. Kwani zinalenga
kujenga taifa lenye mshikamano na umoja.
Nikianza na ile ya ufunguzi wa bunge ambayo
ilipongezwa sana na watanzania kwani nilitoa mwanga wa uongozi wako kwa kipindi
cha miaka mitano ya kwanza. Lakini hotuba nyingine pia ambazo umekuwa ukizitoa
sehemu mbalimbali. Zikionyesha kutoka moyoni na hata sura yako ikionyesha
dhaili kuwa unachukia maskini na watu wengine wa tabaka la chini kunyanyaswa na
wenye navyo.
Hapa naizungumzia hotuba yako uliyoitoa hivi
karibuni ulipokuwa jijini mwanza kwa kuwatetea wachuuzi na wafanya biashara
ndogo ndogo nchini wanaosumbuliwa na baadhi ya viongoz. Na kuwafanya watanzania hawa wa hali ya chini
kuishi maisha kama wakimbizi katika nchi yao ambayo imejawa na amani tele.
Waswahili wana msemo usemao mkubwa hakosei, lakini
pia wengine wakasema mkubwa jaa. Lakini mimi nipingane kidogo na usemi huu
ambao kwa uelewa wangu mdogo naona umepitwa na wakati. Maana binadamu
tumeumbiwa kukosea na ndiyo maana waswahili wakasema kutenda kosa si kosa bali
kurudia kosa.
Wakiwa na maana unaweza kutenda kosa mara moja
lakini baada ya kuelewa utekosea unaweza kusahisha makosa au kasoro
zilizojitokeza hapo awali ili kuepuka nkurudia kosa. Ambalo litajenga taswira
mbaya ya kibuli, chuki, wivu,majivuno na dharau miongoni mwa watu.
Nasema hivyo mkuu wangu na mtukufu rais kutokana na
kauli zako ambazo naweza sema huwa zina ukakasi japo wewe unaziona zipo sahihi.
Na nyingine ambazo huwa unazitoa japo kwa matani lakini ukumbuke kuwa
tunatofautiana mapokeo wengine wakiamini rais amesema hivyo tunabidi
tutekeleze.
Nikiachana na hilo nije kwenye kauli zako ulizo
zitoa hivi karibuni ulipokuwa kwenye ziara yako ya kuwashukru watanzania
waishio katika visiwa vya Pemba na Unguja. Ambayo watu wengi nikiwemo na mimi
mwenyewe kuwa ilikuwa imejaa kebehi, uhasama, ubabe, vitisho, vijembe na mambo
mengine kadha wa kadha ambayo kiukweli hayakupaswa kuzungumza na mtu mwenye
hadhi ya kwako.
Utakumbuka kuwa mgogoro wa Zanzibar ni wa muda mrefu
ambao kama mkuu wan chi ulipaswa kwenda kuwaunganisha wazanzibar ambao wengi
wao wamejawa na hasira kutokana na yale ambayo wanaamini hawatendewi sawa na
serikali yao.
Kauli mbalimbali ulizozitoa Zanzibar kiukweli
umetonesha donda ambalo lilikuwa limeanza kupona miongoni mwa wazanzibar. Lakini
kwa kauli zako kiukweli zinaweza kuleta mpasuko mkubwa na kurudisha hali ya
uhasama mkubwa visiwani humo kutokana na kauli zako ulizo zitoa.
Utakumbuka kuwa kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kulitafsiriwa
na mataifa makubwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kama ni uonevu. Na upendeleo
ambao ilikuwa ni dhahili faulu ya kutengenezewa upenyo wa ushindi kwa chama
tawala ili kiongoze tena kwa mara nyingine. Lakini ukweli halisi unajulikana miongoni
mwa tume ya uchaguzi ya Zanzibar.
Utakumbuka kuwa tume ilikuwa huru lakini kitendo cha
kauli yako ya kumtaka Dr. Shein kumpa tuzo Jecha Salim Jecha kumezihilisha wazi
kuwa ulikuwa mpango wa serikali kuvuruga uchaguzi ili chama tawala kiendeleze
ubabe wake visiwani humo.
Kwa kweli haikuwa kauli ya kuitoa kama Rais wan chi tena
kwenye hadhara ya watu wote wale ambapo, watu walikusanyika kuja kusikiliza
nini rais wao atawaambia na kuwashukru kwa kumpa sifa ya kuwa Rais wa jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Pia kauli yako ya kumtaka Dr. Shein Kutomsainia pesa
ya matibabu mpinzani wake Maalim Seif kwa kisa cha kutokumpa mkono, kiukweli imeonyesha
wazi kuwa haumpendi na unafurahia migogoro inayoendelea.
Nilitegemea kama mkuu wa nchi kuwaweka pamoja watu
hawa kwa kuwa uchaguzi umekwisha, waweze kushirikiana pamoja ili kujenga
Tanzania yenye amani na upendo baina ya watanzania. Lakini mkuu wangu ulienda
kutonesha donda ndugu ambalo limeuguzwa kwa muda mrefu tena kwa kulipiga na
nyundo nzito.
Itakumbukwa kuwa marudio ya uchaguzi wa Zanzibar
yaliifanya serikali ya Tanzania kusitishiwa fedha zilizokuwa zinatolewa na
mfuko wa changamoto za maendeleo kutoka Marekani MCC na nchi nyingine wahisani walisitisha
misaada yao kwa kile walichokiona ni kubanwa kwa demokrasia visiwani Zanzibar.
Ni rai yangu kwa viongozi na timu ya washauri wako
wakaona umuhimu wa kukuandalia hotuba ambayo utaisoma mbele ya kusanyiko lolote
ambalo utaenda. Ili kuepusha kutiririka kwa maneno ambayo yanaweza kupandikiza
chuki na uhasama baina ya wananchi wan chi hii na viongozi wao au baina ya
chama tawala na vyama pinzani.
Japo itakuwa vigumu kwako kusoma neno kwa neno
lakini itasaidia kuondoa maneno amabyo yanakera baadhi ya watanzania na mataifa
mengine yanayokutazama kwa mkuwa mfano bora. Maana kwa muda mchache ambao
umekaa kwenye kiti hiki mataifa makubwa yamekusifu na baadhi ya viongozi wa
kimataifa umekuwa mfano wao wa kuigwa kama kiongozi.
Ni wako katika ujenzi wa taifa hili, Baraka
Ngofira, mwananchi mzalendo wa Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Mbariki rais wetu
mtukufu John Pombe Magufuli na watanzania wote ili Amani na Upendo vikatawale
daima.
BARUA YANGU KWA RAIS WA JAMHURI TUKUFU YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DR. JOHN POMBE MAGUFULI.
Reviewed by WANGOFIRA
on
04:26:00
Rating:
No comments: