Wezi fedha za TASAF kikaangoni


SERIKALI imetoa siku 30 kukamatwa kwa watumishi waliosababisha matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) III, kwa kuingiza majina ya watu masikini wasiostahili ili kujipatia fedha za mradi huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akizungumza na baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi, jana alisema ni lazima watumishi wa umma waliohusika katika kuisababishia hasara Serikali wawajibishwe.

Februari mwaka huu, TASAF ilitekeleza maagizo ya Serikali na kufanya uhakiki wa kaya masikini ziliopo kwenye mpango wa kupata fedha na kuziondoa zile zilizokosa sifa na kuziondoa kaya 32,456.

“Katika msako huo tulibaini, waliokufa ni 7,819, viongozi waliojipachika 2,999, waliohama sehemu ambapo mpango haujaanza 3,948, wasiojitokeza au wasiofahamika 9,342 na wasiokuwa na sifa 8, 348,” alisema Simbachawene.

Aidha alisema kuwa, zoezi hilo ni endelevu na kwamba utaratibu wa kutoa taarifa za walengwa waliofariki au kuhama unapaswa kufanyika ili fedha za serikali zisitumike ovyo nje ya malengo yaliyokusudiwa.

Simbachawene alisema, kuingizwa kaya zisizo na sifa katika mpango huo na kuachwa kwa kaya ambazo ni maskini zaidi, kumetokana na baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao pia wamekuwa wakipunguza malipo ya walengwa.

Watu 6.5 milioni, katika kaya maskini na zinazoishi katika mazingira hatarishi wanatarajiwa kunufaika na mradi wa fedha za TASAF katika awamu ya sasa.

Hata hivyo, Simbachawene aliwashauri wakurugenzi wa halmashauri zote nchini pamoja na wakuu wa wilaya, kutoogopa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwani suala hilo litaepusha hasara na mianya ya wizi.

Mhandisi Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alimuahidi waziri Simbacahwene kuwa, hawatofumbia macho ubadhirifu katika halmashauri na kusema watazishauri, kuzikumbusha na hata kuingilia kati pale mambo yanapoenda ndivyo sivyo katika halmashauri.
Wezi fedha za TASAF kikaangoni Wezi fedha za TASAF kikaangoni Reviewed by WANGOFIRA on 13:29:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.