Watakaochakachua Mitihani Kidato cha Nne Kukiona

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema haafiki uchakachuaji kwenye mitihani na kusema wakuu wa shule watakaobainika kufanya udanganyifu huo hawatapona.

Profesa Ndalichako alisema hayo kwenye kikao kati ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, Maofisa Elimu wa Mikoa, Wakuu wa shule kongwe na wakuu wa shule zilizoungua moto.

Alisema ikiwa imebaki miezi mitatu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kufanya mitihani aliwataka wakuu wa shule kujipanga kupata ufaulu mzuri.

“Bado siafiki suala la uchakachuaji kwenye mitihani wanafunzi waachwe wafanye mitihani wenyewe na si kupitia kamati za ufundi, sasa Wizara inaangalia ubora wa elimu na wakuu wa shule watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua,” alisema.

Alisema pia matokeo ya mitihani ya shule za sekondari ya mwaka jana yalimhuzunisha sana lakini anaamini wakuu wa shule watajipanga kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri zaidi.

“Nilipokuwa Baraza la Mitihani nilisema nisiulizwe kutokana na matokeo kuwa mabaya lakini sasa niko Wizara ya Elimu siwezi kukwepa hilo tena,” alisema.

Waziri Ndalichako alisema watabadilisha mfumo wa namna maofisa elimu watakavyofanya kazi zao ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule za serikali na kuwataka wakuu wa shule na maofisa elimu kila mmoja ajipange.

Aidha alisema mkuu wa shule ni mdhibiti wa taaluma katika eneo lake na hatakiwi kumuogopa mtu anayemuongoza. Waziri huyo pia alisema katika mtihani wa kidato cha sita uliopita shule 100 za kwanza shule za serikali zilikuwa tatu na kuwa nafasi ya 53 ndio ilishikwa na Ilboru ya Arusha.

“Mpaka namba 100 shule za serikali ni tatu tu, sio kitu cha kawaida hapa ndio mahali pa kuzungumza kama serikali tunashindwa kuonesha mfano tuachie sekta binafsi,” alisema
Watakaochakachua Mitihani Kidato cha Nne Kukiona Watakaochakachua Mitihani Kidato cha Nne Kukiona Reviewed by WANGOFIRA on 21:44:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.